Tuesday, May 22, 2018

NAIBU WAZIRI LUGOLA APONGEZA UJENZI DAMPO LA KISASA


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (mwenye sare ya bluu) akipata maelezo jinsi mzani uliopo katika Dampo la kisasa la kuhifadhia taka lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma unavyofanya kazi kwa njia ya Kompyuta, kutoka kwa Mhandisi wa Mazingira wa Halmashauri hiyo Barnabs Faida.  
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (mwenye sare ya bluu) akifuatilia maelekezo ya jinsi maabara ya kupima kemikali kwenye maji ya ardhini katika eneo la Dampo la kisasa la Halmashauri ya  Manispaa ya Dodoma inavyofanya kazi ili kuhakikisha nuwepo wa Dampo hilo hauhatarishi vyanzo vya maji katika maeneo ya jirani. Anayetoa maelezo ni Afisa Mazingira kutoka Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu ya Halmashauri hiyo  Happynes Pastory.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (wa tatu kushoto) akiwa katika eneo la Dampo la kisasa la kuhifadhia taka lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma alipofanya ziara kukagua Mifumo ya usimamizi wa Mazingira katika Dampo hilo inavyofanya kazi. Wa pili kushoto ni Diwani wa Kata ya Ntyuka Theobald Maina.
Sehemu ya Dampo iliyoanza kutumika
Sehemu ya pili ya Dampo ambayo itatumika baada ya sehemu ya kwanza kujaa

...................................................................

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola ameipongeza Halmashauri ya Manispaa Dodoma kwa ujenzi wa Dampo la kisasa la kuhifadhia taka kwa teknolojia ya kuzizika ardhini (Sanitary Land Fill) lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu katika Halmashauri hiyo.

Alitoa pongezi hizo jana baada ya kufanya ziara katika Dampo hilo kwa lengo la kukagua mifumo ya usimamizi wa Mazingira.
“Mfikishieni Mkurugenzi wa Halmashauri salamu zangu…nimeridhika na uendeshaji wa Dampo hili na jinsi mnavyozingatia na kusimamia usalama wa Mazingira” alisema Naibu Waziri huyo.

Alisema ni fahari kubwa kwa Halamshauri ya Manispaa ya Dodoma kuwa na Miundombinu ya kisasa ya usafi na kutaka taka zote zinazozalishwa ziondolewe na kupelekwa katika Dampo hilo ili kufiki malengo ya mradi huo.

Dampo hilo lilianza kujengwa mwaka 2010 na hadi linakamilika limegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 7.1 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia kupitia Serikali Kuu ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuendeleza Miji ya Kimkakati Tanzania (TSCP) inayoratibiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Naibu Waziri Lugola alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya siku saba katika Wilaya ya Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine, anakagua jinsi mifumo ya usimamizi wa Mazingira katika taasisi mbalimbali ikiwemo Hospitali na Vyuo inavyosimamiwa na kufanya kazi.


No comments:

Post a Comment