Monday, August 21, 2017

MEYA WA MANISPAA YA DODOMA PROF DAVIS MWAMFUPE ATOA SOMO MAONESHO YA NANENANE

HALMASHAURI za Manispaa na Wilaya katika mikoa ya Kanda ya  Kati unayoundwa  na mikoa ya Dodoma na Singida kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaounga mkono shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi wameshauriwa kubuni njia rahisi inayoweza  kuwafikishia kwa wakulima na wafugaji elimu inayopatikana kwenye viwanja vya Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane.
Rai hiyo imetolewa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe  kufuatia maenesho ya Nanenane yaliyomalizika hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo amesema bado Maonesho hayo  hususan Kanda ya Kati hayajafanikiwa kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwa kiasi kinachoridhisha na kuwawezesha kubadili shughuli zao na kuzifanya kuwa na tija inayoridhisha.
Alisema Maonesho ya Nane Nane yamekuwepo kwa miaka mingi katika Kanda mbalimbali nchini na yamekuwa na mambo ya kuvutia sana hususani Teknolojia na mbinu bora za uzalishaji katika kilimo na mifugo ambazo zinauwezo wa kuleta tija kubwa lakini bado changamoto kubwa ni kwamba mambo yote bora na mazuri yanayopatikana kwenye Maonesho hayajaweza kumfikia mkulima kwenye ngazi za msingi kwa maana ya ngazi ya kaya na vijiji.
Alisema kuwa, unaweza kutoka umbali usiozidi kilomita mbili tu kutoka kituo (Uwanja) cha Maonesho kilipo utashangaa kukuta mkulima analima kilimo cha kienyeji ambacho hakina manufaa.
 “Teknolojia inayooneshwa kwenye Maonesho haya bado haijaweza kuwafikia wakulima na wafugaji wetu kwenye vijiji vyao wanakoendesha shughuli zao za kilimo na mifugo” alisema Profesa Mwamfupe na kuongeza kuwa, bado teknolojia na ubunifu unaopatikana kwenye Maonesho haya unahitaji kuwafikia wakulima wa chini kabisa.
Alitoa wito kwa Mamlaka zinazohusika kuhakikisha Kiwanja cha Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati kilichopo katika Kata ya Nzuguni Manispaa ya Dodoma  kinakuwa kituo cha Shamba Darasa la kilimo mifugo na uvuvi cha kudumu ili  wataalamu wa kilimo na mifugo wawepo kituoni hapo kipindi chote cha mwaka wakisimamia shughuli za kilimo na mifugo kituoni hapo na Halmashauri zilete Wakulima na Wafugaji wao kujifunza na kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za uzalishaji.

 
Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe (wa kwanza kulia) akishuhudia mmoja ya banda la maonesho alipotembelea Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati katika Viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma hivi karibuni.

Thursday, August 17, 2017

MANISPAA YA DODOMA YATENGA ENEO MAALUM LA MACHINGA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani la kufunga mwaka wa fedha 2016/2017 uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Manispaa ya Dodoma.

........................................................................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imetenga eneo la Makole D-Center lililoko katikati ya Mji wa Dodoma kuwa eneo rasmi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo maarufu kama Machinga kufanya biashara zao badala ya kupaga bidhaa ovyo mitaani hali inayopelekea kuharibu taswira ya mji.

Hatua hiyo pia itasaidia kuendana na kasi kubwa ya ongezeko la wafanyabiashara hao kuingia Mjini humo kutoka mikoa mbalimbali nchini tangu Serikali ilipohamia rasmi Dodoma ambako ni Makao Makuu ya Nchi.

Akizugumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani la kufunga wa fedha uliopita lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita  katika ukumbi wa Manispaa hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin aliyewajulisha wajumbe na wananchi kuwa, sasa Manispaa iko katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa  miundombinu muhimu katika eneo hilo ikiwemo vyoo ili shughuli za biashara zifanyike katika mazingira salama na rafiki.

“Tunatarajia eneo hilo litakuwa tayari kufikia mwisho wa mwezi Agosti au mwanzo wa mwezi Septemba mwaka huu mara moja tutaanza zoezi la kuwahamishia wafanyabiashara hao pale” alifafanua.

Alisema Manispaa inashirikiana kwa karibu na viongozi wa wafanyabiashara hao katika zoezi hilo, na kwamba endapo eneo hilo halitatosha, wafanyabiashara wengine watahamishiwa katika eneo la Chaduru .


Tayari Manispaa ya Dodoma ilishaanza zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wa Matunda na chakula katika maeneo yasiyo rasmi na kuwahamishia katika maeneo rasmi ya masoko ikiwemo soko la Sabasaba, Bonanza, na Tambukareli. 

Thursday, August 10, 2017

NAIBU MEYA WA MANISPAA YA DODOMA JUMANNE NGEDE ATETEA NAFASI YAKE

Mgombea aliyeshinda nafasi ya Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumannne Ngede (CCM) akitoa neno kwa wajumbe mara baada ya kushinda nafasi hiyo kufuatia uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Manispaa hiyo. Wa pili kushoto ni Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa George Mwamfupe na kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi. Kulia na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ambaye pia Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana akifautiwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme.
Mgombea aliyeshindwa nafasi ya Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Samwel Mziba  (CHADEMA) akitoa neno kwa wajumbe mara baada ya matokeo kutangazwa kufuatia uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Manispaa hiyo.
...............................................................................................
..............................................................

NAIBU Meya wa Manispaa ya Dodoma aliyemaliza muda wake Jumanne Ngede amefanikiwa kutetea nafasi yake katika uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Manispaa ya Dodoma ambapo wajumbe 56 walishiriki uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo Ngede ambaye ni Diwani wa Kata ya Chamwino kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 47 dhidi ya  mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Samwel Mziba ambaye ni Diwani wa Kata ya Hazina aliyepata kura 9.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma ambaye ni Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Dodoma Mjini Godwin Kunambi alimtangaza rasmi Ngede kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Baada ya kufanikiwa kutetea nafasi yake, Ngede aliwashukuru wajumbe kwa kumchagua kwa kura nyingi jambo linaonesha kuwa wana imani kubwa na utendaji wake na kwamba ataendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwa kushirikiana na Madiwani wote.


Kwa upande wake, mgombea aliyeshindwa Samweli Mziba aliwashukuru wajumbe na kumpongeza mshindi huku akidai uchaguzi umepita na sasa ni kuchapa kazi tu.