Monday, July 31, 2017

WANAOVAMIA MAENEO, UJENZI HOLELA MANISPAA YA DODOMA SIKU ZAO ZINAHESABIKA


Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (katikati)  akiwa na baadhi ya Wakuu wa Idara alipozungumza na wamiliki wa nyumba za kupanga Manispaa ya Dodoma (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau hao na Mkurugenzi huyo jana Katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma.

 Baadhi ya wamiliki wa nyumba za kupanga katika Manispaa ya Dodoma wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau hao na Mkurugenzi huyo jana Katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma.  


.................................................................................................

MKURUGENZI wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ametoa wito kwa wakazi wa Manispaa hiyo kuacha mara moja uvamizi wa maeneo ya wazi na yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za misitu ambapo watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha amewataka wanaojenga nyumba za makazi au za biashara katika maeneo yasiyo rasmi na ambayo hayakupimwa kusitisha shughuli za ujenzi na kubomoa majengo hayo kwa hiyari yao vinginevyo Halmashauri ya Manispaa itayabomoa.

Alisema hayo jana wakati akizungumza wa wamiliki wa nyumba za kupanga na Maofisa Watendaji wa Kata wa Manispaa ya Dodoma katika ukumbi wa Dodoma Sekondari, ambapo alisema kujenga katika maeneo yasiyopimwa ni kinyume na sheria na Manispaa ya Dodoma imejipanga kusimamia hilo kikamilifu.

Alisema Manispaa ya Dodoma imejipanga kuanza upimaji wa viwanja kwa kasi ili kuwawezesha wananchi  hususan wakazi wa Dodoma kujenga kwa kuzingatia sheria za Mipango Miji na kwamba upimaji huo utaenda sambamba na utoaji wa vibali vya ujenzi katika kipindi kisichozi siku saba kwa mmiliki wa kiwanja.

Kwa upande wa wamiliki wa nyumba za kupanga, aliwataka kuungana na kuwa na umoja na uongozi wao ili kuepukana na madalali ambao baadhi yao sio waaminifu, huku akiwapa changamoto ya kujenga nyumba zaidi za makazi na kuziimarisha zilizopo huku akiwajulisha kuwa, hivi karibuni watumishi  wa Serikali zaidi ya 2,000 wanatarajiwa kuhamia Mjini Dodoma ikiwa ni awamu ya pili ya Serikali kuhamia Dodoma hivyo mahitaji ya nyumba za kuishi yatakuwa makubwa.

Monday, July 24, 2017

NAIBU WAZIRI TAMISEMI SELEMANI JAFFO AKABIDHI HUNDI YA MILIONI 70 KWA VIJANA NA WANAWAKE, AIPONGEZA MANISPAA YA DODOMA , ATAKA HALMASHAURI ZINGINE KUIGA MFANONaibu waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jaffo akizungumza kabla ya kukabidhi mfani wa Hundi ya shilingi milioni 70 kwa wawakilishi wa vikundi vya wanawake na vijana  wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya fedha hizo zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa ajili ya vikundi hivyo leo katika ukumbi wa Manispaa hiyo Wa pili kulia ni Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe na kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi. PICHA NA RAMADHANI JUMA, OFISI YA MKURUGENZI.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) akitoa taarifa ya utangulizi kabla Naibu waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jaffo (wa pili kushoto) hajakabidhi mfano wa Hundi ya shilingi milioni 70 kwa wawakilishi wa vikundi vya wanawake na vijana  wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya fedha hizo zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa ajili ya vikundi hivyo leo katika ukumbi wa Manispaa hiyo. Wa pili kulia ni Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe. PICHA NA RAMADHANI JUMA, OFISI YA MKURUGENZI.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jaffo akikabidhi mfani wa Hundi ya shilingi milioni 70 kwa wawakilishi wa vikundi vya wanawake na vijana (kulia na kushoto) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya fedha hizo zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa ajili ya vikundi hivyo leo katika ukumbi wa Manispaa hiyo. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.  PICHA NA RAMADHANI JUMA, OFISI YA MKURUGENZI.................................................................


NAIBU Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jaffo ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa kutekeleza Sera na maelekezo ya Serikali kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa, asilimia 10 ya  fedha zinazotokana na mapato ya ndani zinatengwa na kutumika kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake na Vijana.

Naibu Waziri Jaffo ametoa pongezi hizo wakati akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 70 zilizotolewa na Manispaa hiyo kwa ajili vikundi vya Vijana na Wanawake katika hafla fupi ya makabidhianao iliyofanyika leo katika ukumbi wa Manispaa ya Dodoma.

Alisema Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeonesha mfano kwa vitendo na kwamba Halmashauri zingine zijifunze na kuiga, ambapo amedai hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri wa kazi uliopo kati ya Madiwani, Mkurugenzi, Wakuu wa Idara na Watumishi wote.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi  alisema fedha hizo zinatarajiwa kuvinufaisha vikundi 66, vikiwemo 18 vya vijana na 48 vya wanawake.

Alisema, Halmashauri hiyo imekuwa akitumia fedha za Mapato ya ndani kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ambapo pamoja na kutoa asilimia 10 kwa ajili ya vijana na wanawake, pia asilimia 30 inaelekezwa katika katika miradi ya Maendeleo ambapo mpaka sasa Kata 25 zimepatiwa sehemu ya fedha kwa ajili miradi ya maendeleo.

Aidha, Kunambi alisema kwa sasa Halmashauri hiyo inaanza kusajili vikundi vya walemavu ambavyo kwa mujibu wa Sera na Maelekezo ya Serikali vinatakiwa kupatiwa asilimia mbili ya Makusanyo ya fedha zinatokana na vyanzo vya ndani.

Wednesday, July 19, 2017

PROFESA MWAMFUPE MEYA MPYA MANISPAA YA DODOMA


Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi  akiwaonesha wajumbe wa Baraza la Madiwani Karatasi ya kura wakati wa zoezi la kuhesabu kura  kwa uwazi wakati wa uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Dodoma. PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.
Madiwani waliogombea nafasi ya Meya wa Manispaa ya Dodoma wakitambulishwa mbele ya wajumbe. Kushoto ni Mgombea wa CCM Profesa Davis Mwamfupe na Kulia ni Mgombea wa CHADEMA Yona Kusaja. PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.
Wadau mbalimbali wakifuatilia zoezi la uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Dodoma uliofanyika Julai 19 mwaka huu ambapo Profesa Davis Mwamfupe wa CCM aliibuka Mshindi.  PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.     
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde akitoa neno kwa Meya Mpya na kwa Madiwani wa Manispaa ya Dodoma wakati wa uchaguzi wa Meya wa Manispaa hiyo Julai 19 mwaka huu.  PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.


                                                              

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imepata Meya mpya kufuatia uchaguzi uliofanyika leo Julai 19, 2017 katika Ukumbi wa Manispaa hiyo ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa Davis George Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo.  

Profesa Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 50 kati ya kura zote 58 zilizopigwa na wajumbe 58, dhidi ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kikombo katika Manispaa hiyo Yona Kusaja aliyepata kura 8.

Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi aliwaeleza wajumbe utaratibu mzima wa kupiga kura kwa njia ya siri kwa kutumia karatasi maalum za kupigia kura, na kwamba wajumbe halali watakaopiga kura kwa mujibu wa sheria ni Madiwani wa Manispaa ya Dodoma tu.

Baada zoezi la kupiga na kuhesabu kura kukamilika, Msimamizi wa Uchaguzi Godwin Kunambi kwa Mamlaka aliyonayo kisheria, alimtangaza rasmi Profesa Mwafupe kuwa mshindi na kwamba ndiye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma.

Uchaguzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Anthony Mavunde, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde, wataalam wa Manispaa ya Dodoma na Wakazi wa Manispaa wa Dodoma. 


Profesa Mwamfupe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Meya  mheshimiwa Jaffar Mwanyemba ambaye aliondolewa madarakani na Baraza la Madiwani Aprili 3 mwaka huu kwa kupigiwa kura za kutokuwa na imani naye kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi.

Thursday, July 13, 2017

WATUMISHI WA ILIYOKUWA CDA WAPANGIWA VITUO VIPYA VYA KAZI SERIKALINI, WAZIRI WA TAMISEMI AWASOMEA TAASISI WALIZOPANGIWAMmoja ya watumishi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma akiuliza swali kwa Waziri wa Nchi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI  George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa mkutano na Waziri huyo jana katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma. SERIKALI imewapangia vituo vipya vya kazi watumishi 260 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) baada ya Mamlaka hiyo kuvunjwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli Mei 15 mwaka huu.

Rais Dokta Magufuli alilazimika kuivunja Mamlaka hiyo ili kuondoa mkanganyiko wa kimajukumu kati ya Mamlaka hiyo na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma hususan katika masuala ya umilikishaji wa ardhi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene alikutana na watumishi hao wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma jana na kuwasomea vituo walivyopangiwa katika taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa kujibu wa Waziri Simbachawene, watumishi 150 wamehamishiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, idadi ambayo ni zaidi ya nusu ya watumishi wote 260.
Watumishi 66 wamepangwa katika Mikoa na Wilaya mbalimbali Nchini, watumishi 16 wamehamishiwa katika Ofisi ya Rais TAMISEMI, mtumishi mmoja amepangwa katika Ofisi ya Rais Utumishi, na watumishi watatu wamehamishiwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Taasisi zingine ni Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo imepangiwa watumishi watatu, Wizara ya Ardhi watumishi wawili, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepangiwa mtumishi mmoja, watumishi wanne wamehamishiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Manispaa ya Dodoma na watumishi 14 wamehamishiwa katika kampuni inayosimamia mradi wa mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam (DART).


Kwa Mujibu wa Waziri Simbachawene, Watumishi wote waliopangiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa watakuwa wameshakabidhiwa barua zao za Uhamisho kufikia Julai 12 mwaka huu, ambapo wale waliopangiwa Serikali Kuu watakabidhiwa barua zao muda wowote kuanza sasa kabla ya kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi na kuendelea na majukumu watakayopangiwa.

Wednesday, July 12, 2017

WAZIRI SIMBACHAWENE KUOMBA JIJI LA DODOMA KWA RAIS JOHN MAGUFULI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene (wa pili kushoto) akiingia katika Ofisi za Mhandisi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Dodoma kukagua magari na mitambo iliyorithiwa na Manispaa hiyo kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) wakati wa ziara ya siku moja ya  Waziri huyo katika Manispaa hiyo jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe. 

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene wakati wa ziara ya siku moja ya  Waziri huyo katika Manispaa hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene ameahidi kumfikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli ombi la kuitangaza Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji kwani inakidhi vigizo na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kupewa hadhi hiyo.

Alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Dodoma katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Manispaa hiyo, iliyojumuisha pia ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo.

Aidha, amewataka watumishi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao (CDA) kumshukuru Rais kwa uamuzi wa kuivunja Mamlaka hiyo kwa sababu hatua hiyo imeondoa mkanganyiko uliokuwepo katika kuhudumia wananchi hususani katika sekta ya ardhi na mipango miji ambako Manispaa ya Dodoma pia ilikuwa na jukumu hilo.
Pia aliwaeleza watumishi hao wapatao 260 kuwa, sasa watapata fursa pana zaidi ya kuitumikia nchi yao katika mikoa mbalimbali watakayopangiwa kuendelea kutumikia wananchi kwani wao ni watumishi wa umma na wana haki na wajibu wa kufanya kazi sehemu yeyote nchini.