Wednesday, July 19, 2017

PROFESA MWAMFUPE MEYA MPYA MANISPAA YA DODOMA


Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi  akiwaonesha wajumbe wa Baraza la Madiwani Karatasi ya kura wakati wa zoezi la kuhesabu kura  kwa uwazi wakati wa uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Dodoma. PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.
Madiwani waliogombea nafasi ya Meya wa Manispaa ya Dodoma wakitambulishwa mbele ya wajumbe. Kushoto ni Mgombea wa CCM Profesa Davis Mwamfupe na Kulia ni Mgombea wa CHADEMA Yona Kusaja. PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.
Wadau mbalimbali wakifuatilia zoezi la uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Dodoma uliofanyika Julai 19 mwaka huu ambapo Profesa Davis Mwamfupe wa CCM aliibuka Mshindi.  PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.     
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde akitoa neno kwa Meya Mpya na kwa Madiwani wa Manispaa ya Dodoma wakati wa uchaguzi wa Meya wa Manispaa hiyo Julai 19 mwaka huu.  PICHA NA  RAMADHANI JUMA WA OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.


                                                              

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imepata Meya mpya kufuatia uchaguzi uliofanyika leo Julai 19, 2017 katika Ukumbi wa Manispaa hiyo ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa Davis George Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo.  

Profesa Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 50 kati ya kura zote 58 zilizopigwa na wajumbe 58, dhidi ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kikombo katika Manispaa hiyo Yona Kusaja aliyepata kura 8.

Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi aliwaeleza wajumbe utaratibu mzima wa kupiga kura kwa njia ya siri kwa kutumia karatasi maalum za kupigia kura, na kwamba wajumbe halali watakaopiga kura kwa mujibu wa sheria ni Madiwani wa Manispaa ya Dodoma tu.

Baada zoezi la kupiga na kuhesabu kura kukamilika, Msimamizi wa Uchaguzi Godwin Kunambi kwa Mamlaka aliyonayo kisheria, alimtangaza rasmi Profesa Mwafupe kuwa mshindi na kwamba ndiye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma.

Uchaguzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Anthony Mavunde, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde, wataalam wa Manispaa ya Dodoma na Wakazi wa Manispaa wa Dodoma. 


Profesa Mwamfupe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Meya  mheshimiwa Jaffar Mwanyemba ambaye aliondolewa madarakani na Baraza la Madiwani Aprili 3 mwaka huu kwa kupigiwa kura za kutokuwa na imani naye kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi.

No comments:

Post a Comment