Wednesday, July 12, 2017

WAZIRI SIMBACHAWENE KUOMBA JIJI LA DODOMA KWA RAIS JOHN MAGUFULI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene (wa pili kushoto) akiingia katika Ofisi za Mhandisi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Dodoma kukagua magari na mitambo iliyorithiwa na Manispaa hiyo kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) wakati wa ziara ya siku moja ya  Waziri huyo katika Manispaa hiyo jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe. 

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene wakati wa ziara ya siku moja ya  Waziri huyo katika Manispaa hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene ameahidi kumfikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli ombi la kuitangaza Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji kwani inakidhi vigizo na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kupewa hadhi hiyo.

Alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Dodoma katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Manispaa hiyo, iliyojumuisha pia ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo.

Aidha, amewataka watumishi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao (CDA) kumshukuru Rais kwa uamuzi wa kuivunja Mamlaka hiyo kwa sababu hatua hiyo imeondoa mkanganyiko uliokuwepo katika kuhudumia wananchi hususani katika sekta ya ardhi na mipango miji ambako Manispaa ya Dodoma pia ilikuwa na jukumu hilo.
Pia aliwaeleza watumishi hao wapatao 260 kuwa, sasa watapata fursa pana zaidi ya kuitumikia nchi yao katika mikoa mbalimbali watakayopangiwa kuendelea kutumikia wananchi kwani wao ni watumishi wa umma na wana haki na wajibu wa kufanya kazi sehemu yeyote nchini.


No comments:

Post a Comment