Tuesday, December 6, 2016

LAPF 'YAIPIGA TAFU' MANISPAA YA DODOMA



Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi





















MFUKO wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF) umekabidhi hundi ya Sh. 6 milioni kwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kutatua tatizo la uhaba wa maji katika maeneo ya Ihumwa na Mtumba ndani ya Manispaa hiyo.
Akikabidhi  hundi hiyo kwa Godwin Kunambi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma mjini humo, James Mlowe ambaye ni Meneja Mawasiliano na Masoko wa LAPF amesema, mfuko huo umetoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kufufua visima vya maji vilivyoharibika.

Amesema mfuko huo ulipokea maombi kutoka katika Ofisi ya Manispaa pamoja na ofisi ya mbunge
kupatiwa msaada wa kutengeneza visima vya maji katika Kata ya Ihumwa na Mtumba kutokana na visima hivyo kuharibika na kuwasababishia usumbufu wa kukosea maji wakazi hao.
Amesema LAPF kama taasisi ya serikali, imekuwa ikifanya shughuli nyingi na halmashauri mbalimbali nchini hususani shughuli za maendeleo.

“Kwa sasa Dodoma ni Makao Mkuu ya Nchi hivyo kuna watu wengi watahamia hivyo hakuna sababu ya kuwepo ukosefu wa maji.

“Kadri watu wanavyoongezeka ndivyo mahitaji yanavyoongezeka hivyo mahitaji ya maji ni makubwa zaidi katika Mji wa Dodoma na Ihumwa na Mtumba ni sehemu mahitaji hayo,” amesema Mlowe.

Hata hivyo Mlowe amesema, pesa zinazotolewa na taasisi mbalimbali pamoja na wahisani ni vyema zikatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuzibadilishia matumizi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi  wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema katika uongozi wake, atahakikisha miradi yote iliyokusudiwa inafanyika.

“Ni kweli kwa sasa Dodoma kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa maji katika maeneo ambayo yapo nje ya mji".

“Msaada ambao tumeupata kutoka LAPF utasaidia kuboresha na kukarabati visima vya maji ili wananchi waondokane na adha ya upatikanaji wa maji,”alisema Kunambi.

KWA MSAADA WA MWANAHALISI ONLINE.com


Wednesday, August 3, 2016

MICHUZI BLOG: MTOTO ATOA MSAADA WA MADAWATI DODOMA

BINTI WA KIDATO CHA SITA AUNGANA NA MH. RAIS DKT. JOHN MAGUFULI KATIKA KAMPENI YA MADAWATI, ATOA MSAADA WA MADAWATI 50 MANISPAA YA DODOMA

KATIKA hali isiyotegemewa msichana mdogo Aisha Msantu ambaye ni muhitimu wa kidato cha sita mwaka 2016 ameitikia wito wa Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli wa kuwaomba wadau kushiriki katika zoezi la kuchangia madawati kwa ajili ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari nchini ili waondokane na adha ya kujifunza wakiwa wameketi chini.

Aisha ametoa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 katika shule ya Msingi ya Mwenge iliyopo katika kijiji cha Mbabala A Kata ya Mbabala  Manispaa ya Dodoma, ambapo amesema hiyo ni ndoto yake ya muda mrefu na kwamba anafuraha kuikamilisha ili kuonesha alivyoguswa na tatizo la wanafunzi kukaa chini wakati wa kujifunza.

Mbali na msaada huo wa madawati, msichana huyo ambaye amezaliwa akiwa mlemavu, pia ametoa msaada wa mataulo maalum 84 kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule hiyo yenye thamani ya shilingi laki mbili, kama chachu ya kuwazindua wasijiingize katika masuala ya mahusiano kwa kudanganywa na wanaume kwa kuahidiwa mahitaji madogo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika shuleni hapo juzi baada ya kupokea misaada hiyo kwa niaba ya Serikali na Manispaa ya Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme alimshukuru mtoto Aisha kwa msaada huo ambapo alisema msichana huyo ameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa watoto wenzake huku akitoa wito kwa jamii kujifunza kutokana na tukio hilo.

“Hakuna fedha isiyokuwa na kazi..Aisha ana mahitaji yake na angeweza kuzitumia fedha hizi kwa matumizi mengine ya binafsi lakini yeye ameamua kusaidia wadogo zake wa shule ya Msingi..hili ni jambo la kijasiri sana kwa mschana mdogo kama huyu na ni funzo kubwa kwa jamii nzima” alisema.

Akielezea ndoto aliyokuwa nayo mtoto wake kwa muda mrefu, mama mzazi wa Aisha Bi Rehema alisema mtoto wake huyo alifungua akaunti ya ‘Jumbo Junior’ katika Benki ya CRDB Dodoma na kuanza kujiwekea akiba kidogo kidogo hadi alipofikia azima yake hiyo.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura ameahidi kukarabati darasa moja katika shule hiyo ambako madawati hayo yatatumika, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Msichana Aisha ambaye kwa sasa ni Balozi wa Elimu wa Umoja wa Mataifa (UN) kupitia programu ya ‘4 Quality Education’.


 Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mbabala Pascazia Mayala akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano.

 Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Boniface Michael akifungua shughuli kwa kuwakaribisha wageni. 

 Mama mzazi wa Aisha, Bi Rehema akielezea ndoto ya mtoto wake katika kusaidia jamii.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma Hyasinta Jonas akitoa salamu wakati wa hafla hiyo

 Wazazi wa Aisha, Mzee Msantu na Bi Rehema wakifuatilia shughuli ya Makabidhiano.

 Mwakilishi wa programu ya '4 Quality Education' iliyo chini Umoja wa Mataifa Johnbest Mwahaja akitoa neno la shukrani kwa Aisha.

 Mtoto Aisha (katikati) akitoa hotuba yake kabla ya kukabidhi madawati 50.

 Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura akizungumza katika hafla hiyo ambapo aliahidi kukarabati darasa moja katika shule ya Msingi Mwenge ambako madawati hayo yatatumika ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za msichana huyo.

 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kushoto) akimshukuru mtoto Aisha Msantu (kulia) baada ya kukabidhiwa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 kwa ajili ya shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Mbabala Manispaa ya Dodoma.

Makabidhiano

Mtoto Aisha (wa pili kushoto) na wazazi wake Mzee Msantu (wa kwanza kulia) na Bi Rehema (wa pili kulia) wakiwa wameketi katika madawati hayo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme kushoto.


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kushoto) akiwakabidhi wanafunzi wa kike mataulo maalum 84 yaliyotolewa na Aisha.

Msichana Aisha Msantu (wa kwanza kulia) akiongoza wageni kwenye shughuli ya upandaji miti ya kumbukumbu katika shule ya Msingi Mwenge Manispaa ya Dodoma baada ya kukabidhi msaada wa madawati 50 katika shule hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 5.2


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.

Mtoto Aisha Msantu akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.


Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mbabala Pascazia Mayala akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Boniface Michael akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.

Thursday, July 28, 2016

MICHUZI BLOG: Manispaa ya Dodoma yafanikiwa kukusanya asilimia 80.28 ya mapato

MANISPAA YA DODOMA YAFANYA VIZURI KWENYE MAKUSANYO YA KODI

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imefanikiwa kukusanya asilimia 80.28 ya mapato kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya ndani katika mwaka wa fedha 2015/2016 uliomalizika Juni 30 mwaka huu.

Katika mwaka huo wa fedha Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ilipanga kukusanya shilingi 4,566,075,181 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani (own sources) ambapo mpaka mwisho wa mwaka huo makusanyo halisi ni 3,665,699,279 sawa na asilimia 80.28 ya makisio.

Akizungumza katika kikao cha mwaka cha Baraza la Halmashauri ya Manispaa hiyo, Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa, mafanikio hayo yametokana na uchapaji kazi wa watendaji na madiwani wa Manispaa hiyo.

Mstahiki Mwanyemba aliwapongeza wote waliohusika kwa namna yeyote katika kufikia hatua hiyo huku akitoa wito kwa Ofisi ya Mkurugenzi na Madiwani wa kuimarishwa kwa juhudi zaidi katika ukusanyaji katika mwaka wa fedha 2016/2017.

"Mwaka mpya wa fedha umeshaanza hivyo Mkurugenzi na watendaji wako anzeni kukusanya kodi mapema...na waheshimiwa madiwani tuongeze nguvu katika kusimamia vyanzo vya mapato katika maeneo yetu" alisema.

Aidha, katika mkutano huo ambao kwa mujibu wa kanuni unakuwa na ajenda mbili tu ambazo ni kujadili taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri kwa mwaka uliopita na kupitia na kupitisha ratiba ya vikao vya Halamshauri kwa mwaka unaofuata, wajumbe walipitisha ratiba ya vikao vya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 .   

Tuesday, July 26, 2016

MAJALIWA AZUNGUMZA NA WANADODOMA KUHUSU MIKAKATI YA KUHAMIA MAKAO MAKUU.

MSTAHIKI MEYA DODOMA “TUENZI MASHUJAA KWA KUFANYAKAZI”

NA IMMACULATE MAKILIKA-MAELEZO, Dodoma
Mstahiki Meya wa mji wa Dodoma Jaffari Mwanyemba, amesema kuwa  watanzania wanatakiwa kuwaenzi Mashujaa waliopigana katika  vita mbalimbali  ikiwa ni katika harakati za kuiletea  uhuru  nchi ya Tanzania.
Hayo yamesemwa  leo saa sita usiku, wakati alipokuwa akizima Mwenge wa uhuru uliowashwa jana  Julai 24,  na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini  Mheshimiwa Christina Mndeme katika kilele cha mnara wa mashujaa mnano saa 6 kamili usiku ikiwa ni sehemu ya  maombolezo ya kumbukumbu ya Mashujaa, yaliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo mjini Dodoma.
“Watanzania tuna jukumu la kuwaenzi Mashujaa  kwa kufanyakazi kwa bidii, nidhamu na uadilifu, na kama wote tutafanya hivyo tutakuwa tumewaenzi mashujaa wetu” alisema Mstahiki Meya Mwanyemba
Ameongeza kuwa kila mwananchi atimize uwajibu wake kwa kufanyakazi, ili kila mmoja atapata haki yake na hivyo kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini.
Maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa kwa mwaka huu yamefanyika leo julai 25, mkoani Dodoma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa  mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.

VIKUNDI VYA USHIRIKA NA WAJASIRIAMALI DODOMA WATAKIWA KUJITANUA KIMIRADI


VIKUNDI mbalimbali vya wanaushirika na wajasiriamali katika Manispaa ya Dodoma wameshauriwa kuweka mipango ya kuongeza miradi zaidi ili kukuza mitaji yao na kufikia malengo ya kuundwa kwa vikundi hivyo.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jamanne Ngede wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofanywa na wajumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala katika Kata mbalimbali za Manispaa hiyo.
Aliwataka wanaushirika na vikundi vingine vya wajasiriamali kuunda vikundi vidogo miongoni mwao na kupeana mitaji ili kukuza wigo wa kazi zao na hivyo kujiongezea kipato zaidi.
Miongoni mwa vikundi vilivyokaguliwa na Kamati hiyo ni kikundi cha Kasi Mpya kilichopo katika Kata ya Msalato ambacho ni cha akina mama wanaojishughulisha na ufugaji wa kuku wa mayai na utengenezaji wa batiki.
Kikundi hicho chenye wanachama kumi kina kuku 300 wa mayai ambapo kwa siku moja hukusanya kati ya trei sita hadi kumi za mayai, huku trei moja ya mayai ikiwa na thamani ya shilingi 8,500.
Katika kukiongezea nguvu kikundi hicho cha akina mama, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imekipatia mkopo wa shilingi 806,450 kwa ajili ya kununua chakula cha kuku na madawa ambapo tayari kimeanza kufanya marejesho ya mkopo huo kwa kutoa shilingi 148,000.

 Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jamanne Ngede (mwenye kaunda suti) na ujumbe wake wakitazama kuku waliopo katika moja ya mabanda ya wajasiriamali wa kikundi cha akina mama cha Kasi Mpya kilichopo katika Kata ya Msalato katika Manispaa hiyo. Akina mama hao wanafuga kuku wa mayai wapatao 300.


  Baadhi ya kuku wanaofugwa na akina mama hao

 Kati ya trei 6 hadi 10 za mayai huokotwa kwa siku


 Baadhi ya akina mama ambao ni wanachama wa kikundi hicho


 Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jamanne Ngede (kulia) akipokea zawadi ya mayai kwa niaba ya Kamati ya Fedha na Utawala kutoka kwa wajasiriamali hao.

 Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jamanne Ngede (kulia) akivishwa zawadi ya batiki aliyopewa na wajasiriamali wa kikundi cha akina mama cha Kasi Mpya kilichopo katika Kata ya Msalato katika Manispaa hiyo. 


Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jamanne Ngede (aliyejifunika batiki katikati waliokaa) na wajumbe wengine wa Kamati ya Fedha na Utawala wa Manispaa ya Dodoma John Matonya (kushoto) na Jamal Ngalya (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na kikundi wajasiriamali cha akina mama cha Kasi Mpya kilichopo katika Kata ya Msalato katika Manispaa hiyo, na baadhi ya wataalam wa Manispaa hiyo. 

Wednesday, July 20, 2016

 MAJALIWA AWEKA JIWE LA MSINGI LA UPANUZI NA UKARABATI UWANJA WA NDEGE DODOMA

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KUWEKA JIWE LA MSINGI UKARABATI WA UWANJA WA NDEGE WA DODOMA


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANI

                                                  WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO                                                     
MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim M. Majaliwa kesho, tarehe 20/07/2016, anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Dodoma.
Ukarabati huo utajumuisha urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege hadi kufikia urefu wa kilometa 2.5 kutoka Kilometa 2 za awali.
Kurefushwa kwa barabara hiyo, sasa kutatoa fursa kwa ndege kubwa Bombardier Q400, Gulfstream 550, ATR 72 n.k zenye uwezo wa kubeba abiria 90.
Ukarabati huo unafanyika kwa fedha za Serikali ya Tanzania na unasimamiwa na Wahandisi wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Nchini kwa ushirikiano  na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
Ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma ni miongoni  mwa Miradi mbali mbali inayotekelezwa na Mamlaka ya viwanja Vya Ndege nchini kama vile Viwanja vya Tabora, Bukoba, Kigoma na Mwanza ambayo imekwisha anza na miradi mipya ya viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga itakayoanza hivi karibuni.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ni wakala wa viwanja vya ndege iliyoanzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 404 la mwaka 1999, chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997.
Dira:           Kuwa mtoaji wa Huduma za Viwanja vya Ndege kwa kiwango cha Kimataifa
                        Dhima:         Kutoa Huduma Bora na Viwezeshi katika Viwanja vya Ndege kwa kuzingatia ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo
Imani kuu za Mamlaka:
Kuwajali Wateja
Kuwaendeleza Wafanyakazi wa Mamlaka
Ulinzi na Usalama Viwanjani
Kufanya kazi kwa pamoja
Kuwa na Uongozi wa Mabadiliko
Uadilifu
IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO TAA
CHANZO: FULLSHANGWE BLOG

Monday, July 11, 2016

HALMASHAURI ZAPATA WAKURUGENZI WAPYA- Uteuzi wa Ra...

Halmashauri Zapata Wakurugenzi Wapya- Uteuzi wa Ra...: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli l...

Friday, June 24, 2016


MANISPAA YA DODOMA YAPOKEA 'CONTAINERS' 60 ZA KUTUNZIA TAKATAKA ZITAKAZOSAMBAZWA KATIKA MITAA MBALIMBALI IKIWA NI HATUA MUHIMU YA KUUWEKA MJI KATIKA HALI YA USAFI ZAIDI. VIFAA HIVYO NI SEHEMU YA UTAKELEZAJI WA MRADI WA KUBORESHA MIJI TANZANIA UNAOFADHILIWA NA BENKI YA DUNIA










Tuesday, June 21, 2016

MADAWATI DODOMA KUKAMILIKA HIVI KARIBUNI NA KUFIKIA MAHITAJI


Mafundi wa madawati kwa ajili ya shule za Manispaa ya Dodoma wakiwa katika eneo lao la kazi ndani ya karakana ya Mhandisi wa Ujenzi

MAADHIMISHO SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI; DODOMA WAASWA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI



WANANCHI wanaoishi katika maeneo yenye vyanzo vya maji ikiwemo mabwawa katika Manispaa ya Dodoma wametakiwa kuyalinda na kuyatunza maeneo hayo ili yawe endelevu na kutumiwa na vizazi vya sasa na vijavyo.

Rai hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma Jaffar Mwanyemba wakati alipotembelea bwawa la Matumburu lililopo katika kijiji cha Matumburu Kata ya Matumburu Manispaa ya Dodoma wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya mazingira duniani inayoadhimishwa Juni tano kila mwaka.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika kata hiyo kwa ngazi ya Wilaya ya Dodoma yalienda sambamba na zoezi la upandaji wa miti kuzunguka bwawa la Matumburu ili kuboresha mazingira yake na kutunza chanzo hicho muhimu kinachotegemewa na wananchi zaidi ya 9,000 wa kata hiyo na maeneo ya jirani kwa matumizi yao ya kila siku.

Akizungumza na wakazi wa kata hiyo, Mstahiki Meya amewataka wakazi wa Dodoma kutambua umuhimu wa vyanzo hivyo vya maji kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Dodoma unapata mvua kidogo katika kipindi cha mwaka mzima.

“Ndugu zangu sisi hapa Dodoma tunapata mvua kidogo sana tena ndani ya kipindi kifupi katika mwaka..ni juzi tu tulikuwa na mafuriko katika baadhi ya maeneo ikiwemo kata hii ya Mpuguzi lakini leo ni pakavu utadhani hapakuwa na mafuriko” alisema.

Katika maadhimisho hayo yaliyochagizwa na kaulimbiu isemayo “Tunza vyanzo vya maji kwa uhai wa Taifa letu”, wadau mbalimbali wa utunzaji wa mazingira walipatiwa vyeti vya kutambuliwa ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu kama Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Mipango, na Cho cha Mtakatifu John vilivyopo Manispaa ya Dodoma.
Diwani wa kata ya Mpunguzi John Matonya (kulia) akitoa maelezo kuhusu bwawa la Matumburu lililopo katika kata yake ambapo takribani wakazi 9,000 wanategemea maji ya bwawa hilo kwa matumizi mbalimbali
                                   Shughuli ya maadhimisho ya siku ya Mazingira ikiendelea
 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma Jaffar Mwanyemba akipanda mti katika hifadhi ya bwawa la Matumburu kata ya Mpunguzi jana ikiwa ni maadhimisho ya siku ya mazingira duniani. Takribani wakazi 9,000 wa kata hiyo na maeneo ya jirani wanategemea maji ya bwawa hilo kwa matumizi mbalimbali.

 Wadau mbalimbali wa mazingira wakiwa katika zoezi la upandaji miti katika hifadhi ya bwawa la Matumburu Manispaa ya Dodoma jana.
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede akipanda mti katika hifadhi ya bwawa la Matumburu kata ya Mpunguzi jana ikiwa ni maadhimisho ya siku ya mazingira duniani. Picha zote: Ramadhani Juma-Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Dodoma