Tuesday, July 26, 2016

MSTAHIKI MEYA DODOMA “TUENZI MASHUJAA KWA KUFANYAKAZI”

NA IMMACULATE MAKILIKA-MAELEZO, Dodoma
Mstahiki Meya wa mji wa Dodoma Jaffari Mwanyemba, amesema kuwa  watanzania wanatakiwa kuwaenzi Mashujaa waliopigana katika  vita mbalimbali  ikiwa ni katika harakati za kuiletea  uhuru  nchi ya Tanzania.
Hayo yamesemwa  leo saa sita usiku, wakati alipokuwa akizima Mwenge wa uhuru uliowashwa jana  Julai 24,  na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini  Mheshimiwa Christina Mndeme katika kilele cha mnara wa mashujaa mnano saa 6 kamili usiku ikiwa ni sehemu ya  maombolezo ya kumbukumbu ya Mashujaa, yaliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo mjini Dodoma.
“Watanzania tuna jukumu la kuwaenzi Mashujaa  kwa kufanyakazi kwa bidii, nidhamu na uadilifu, na kama wote tutafanya hivyo tutakuwa tumewaenzi mashujaa wetu” alisema Mstahiki Meya Mwanyemba
Ameongeza kuwa kila mwananchi atimize uwajibu wake kwa kufanyakazi, ili kila mmoja atapata haki yake na hivyo kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini.
Maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa kwa mwaka huu yamefanyika leo julai 25, mkoani Dodoma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa  mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment