Monday, July 30, 2018

JIJI LA DODOMA LATOA MILIONI 950 KWA WANAWAKE NA VIJANA, WAZIRI JAFO AKABIDHI HUNDI

....................................................................

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 950 zilizotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoka katika Mfuko wa Wanawake, Vijana, na Walemavu kwa ajili ya vikundi 234 vya Wanawake na Vijana huku akitoa wito kwa Jiji hilo kutafuta masoko ya bidhaa  zinazozalishwa na vikundi hivyo kwani imekuwa moja ya changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Hafla ya kukabidhi hundi hiyo kwa Wanavikundi hao imefanyika hivi karibuni katika Viwanja vya Nyerere vilivyopo katikati ya Jiji la Dodoma.

‘’Viongozi muandae Mpango Mkakati wa kuwa na masoko ya kuuza bidhaa za wajasiriamali hawa, nimeona wana bidhaa nzuri sana ambazo unaweza usiamini kama zinatoka Dododma, lakini kila mmoja ukimuuliza soko anakwambia hana soko maalumu’’ Alisema Waziri Jafo.

Aliongeza ‘’Mbali na kuwapa fedha lakini pia nakuagiza Mkurugenzi wa Jiji (Godwin Kunambi ) na Mstahiki Meya (Profesa David Mwamfupe) mtafute eneo la kimkakati kwa ajili ya hawa mnaowapatia mkopo na vikundi vyote vilivyowezeshwa na Halmashauri hii, kwa kufanya hivi tunaweza kuwa na eneo moja maalumu ambalo litakuwa linafanya maonyesho kwa mwaka mzima’’ Alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alimweleza Waziri Jafo kuwa, fedha hizo zinatokana na ukusanyaji bora wa mapato ya ndani na kwamba kwa sasa Halmashauri inatoa mikopo mikubwa kuanzia Shilingi milioni moja hadi milioni kumi na kutoa wito kwa wajasiriamali kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kukidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.

Alisema fedha hizo zinatolewa kwa vikundi 234 vya Wajasiriamali, vikiwemo 168 vya Wanawake pamoja na vikundi 66 vya Vijana.


Thursday, July 12, 2018

MKATABA WA KIHISTORIA DODOMA YA KIJANI WASAINIWA

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo wakisaini hati ya makubaliano ya kupanda na kustawisha miti, na kuhifadhi misitu iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuikijanisha Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania  (TFS) Professa Dos Santos Silayo wakikabidhiana hati ya makubaliano.


Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) akifafanua jambo mbele ya Mtendaji Mkuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo kuhusu maeneo waliyokubalina kupanda na kustawisha miti, na kuhifadhi misitu iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuikijanisha Dodoma. 

........................................................................
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zimesaini hati ya makubaliano (MOU) ya upandaji, ustawishaji, na utunzaji wa miti na uhifadhi wa misitu iliyopo katika Jiji hilo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Dodoma ya Kijani iliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais  Mhe. Samia Saluhu Hassan kwa kupanda miti kwenye eneo la Mzakwe mwishoni mwa mwaka jana.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ambayo ni ya kwanza kufanywa na TFS Nchini ilifanyika jana katika Ofisi za Jiji, ambapo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi na Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Dos Santos Silayo walisaini makubaliano hayo ambayo utekelezaji wake unaanza katika mwaka huu wa fedha.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali, Mkurugenzi Kunambi alisema Jiji linawakabidhi TFS hekta 150 za msitu katika eneo la Mahomanyika ili kustawisha miti na kulihudumia.
“Lakini pia kwa makubaliano haya, TFS watahifadhi maeneo yote ya vilima vilivyopo ndani ya Jiji la Dodoma na kustawisha misitu midogo katika maeneo ya makazi yaliyotengwa kwa ajili hiyo” alisema Kunambi.
Alisema hizi ni juhudi za kutekeleza kampeni ya Dodoma ya Kijani ambayo ina lengo la kulifanya Jiji la Dodoma na Mkoa mzima kustawisha miti ya kutosha ili kuhifadhi mazingira yatakayokuwa rafiki zaidi kwa maisha ya binadamu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Silayo alisema kuwa tayari taasisi yake imetenga Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mpango huo alioutaja kuwa wa Kihistoria kwani haujawahi kufanyika katika Halmashauri yeyote Nchini, na kwamba utalipa hadhi kubwa Jiji la Dodoma kwenye Jumuiya ya Kimataifa.
“Makubaliano haya yataliweka Jiji la Dodoma katika ramani ya dunia katika kwenda na mahitaji ya maendeleo endelevu ya dunia kupitia mpango uendelevu wa Miji, lazima tujipange kukabiliana na ongezeko la watu na ukuaji wa Miji, Mpango huu utalifanya Jiji hili kwenda sambamba na kuweka uwiano sawia wa kiikolojia.” Alisema Profesa Silayo.
Makubaliano hayo yamesainiwa ikiwa ni takribani wiki mbili baada ya Jiji la Dodoma kuingia makubaliano na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) ya utunzaji wa mizunguko mitatu mikubwa ya barabara iliyopo Jijini humo, ambapo Mamlaka hiyo itahudumia bustani za maua na kuweka sanamu za Wanyama ikiwemo ya Tembo ili kupendezesha Mji na kutangaza vivutio vya kitalii vilivyopo Nchini.