![]() |
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo wakikabidhiana hati ya makubaliano. |
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) akifafanua jambo mbele ya Mtendaji Mkuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo kuhusu maeneo waliyokubalina kupanda na kustawisha miti, na kuhifadhi misitu iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuikijanisha Dodoma.
........................................................................
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma na Wakala ya
Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zimesaini hati ya makubaliano (MOU) ya upandaji,
ustawishaji, na utunzaji wa miti na uhifadhi wa misitu iliyopo katika Jiji
hilo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Dodoma ya Kijani
iliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Saluhu Hassan kwa kupanda miti kwenye eneo la Mzakwe mwishoni mwa mwaka
jana.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ambayo
ni ya kwanza kufanywa na TFS Nchini ilifanyika jana katika Ofisi za Jiji,
ambapo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi na Mtendaji Mkuu wa TFS
Profesa Dos Santos Silayo walisaini makubaliano hayo ambayo utekelezaji wake
unaanza katika mwaka huu wa fedha.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa
na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali, Mkurugenzi Kunambi alisema Jiji
linawakabidhi TFS hekta 150 za msitu katika eneo la Mahomanyika ili kustawisha
miti na kulihudumia.
“Lakini pia kwa makubaliano haya, TFS watahifadhi
maeneo yote ya vilima vilivyopo ndani ya Jiji la Dodoma na kustawisha misitu
midogo katika maeneo ya makazi yaliyotengwa kwa ajili hiyo” alisema Kunambi.
Alisema hizi ni juhudi za kutekeleza kampeni ya
Dodoma ya Kijani ambayo ina lengo la kulifanya Jiji la Dodoma na Mkoa mzima
kustawisha miti ya kutosha ili kuhifadhi mazingira yatakayokuwa rafiki zaidi
kwa maisha ya binadamu.
Kwa upande
wake, Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Silayo alisema kuwa tayari taasisi yake
imetenga Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mpango huo alioutaja
kuwa wa Kihistoria kwani haujawahi kufanyika katika Halmashauri yeyote Nchini,
na kwamba utalipa hadhi kubwa Jiji la Dodoma kwenye Jumuiya ya Kimataifa.
“Makubaliano haya yataliweka Jiji la Dodoma
katika ramani ya dunia katika kwenda na mahitaji ya maendeleo endelevu ya dunia
kupitia mpango uendelevu wa Miji, lazima tujipange kukabiliana na ongezeko la
watu na ukuaji wa Miji, Mpango huu utalifanya Jiji hili kwenda sambamba na kuweka
uwiano sawia wa kiikolojia.” Alisema Profesa Silayo.
Makubaliano hayo yamesainiwa ikiwa ni takribani
wiki mbili baada ya Jiji la Dodoma kuingia makubaliano na Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCA) ya utunzaji wa mizunguko mitatu mikubwa ya barabara iliyopo
Jijini humo, ambapo Mamlaka hiyo itahudumia bustani za maua na kuweka sanamu za
Wanyama ikiwemo ya Tembo ili kupendezesha Mji na kutangaza vivutio vya kitalii
vilivyopo Nchini.
No comments:
Post a Comment