Thursday, June 8, 2017

'KITIMOTO' MARUFUKU MAKAO MAKUU DODOMA

DAKTARI wa Mifugo Wilaya ya Dodoma Mjini Innocent Kimweri  kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na Kifungu Namba 17 cha sheria ya magonjwa ya Mifugo Namba 17 ya mwaka 2003 ametangaza rasmi kwamba Wilaya ya Dodoma Mjini inamlipuko wa ugonjwa wa Homa ya nguruwe na kwa sasa ameweka zuio la biashara ya Nguruwe na mazao yake hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo. 
Katika kipindi cha zuio: 
  • Hakuna mnyama yeyote jamii ya nguruwe (Ngiri, nguruwe pori au nguruwe wa kufugwa) ataruhusiwa kuingia, au kutoka nje ya eneo la Wilaya ya Dodoma pasipokuwa na ruhusa ya maaandishi kutoka kwa Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Dodoma.
  • Pia hakuna bidhaa inayotokana na nguruwe, ikiwemo mbolea, kinyesi, mkojo na damu kitakacho ruhusiwa kuingia au kutoka nje ya Wilaya ya Dodoma pasipokuwa na ruhusa ya maandishi kutoka kwa Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Dodoma Mjini.
  • Aidha, hakuna mnyama yeyote wa jamii iliyotajwa hapo juu atakayekusanywa kwa ajili ya biashara pasipokuwa na ruhusa ya maandishi kutoka kwa Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Dodoma. 
  • Uchinjaji wa nguruwe ndani ya Wilaya ya Dodoma, utafanyika chini ya usimamizi madhubuti wa mtaalam wa afya za mifugo mwenye dhamana.

MKUU WA WILAYA YA DODOMA CHRISTINE MNDEME KUVILEA VIKUNDI VYA USAFISHAJI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA MANISPAA YA DODOMA


MKUU wa wilaya ya Dodoma Mheshimiwa Christine Mndeme akihutubia wadau wa Mazingira (hawapo pichani) katika sherehe za maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani Juni 5 mwaka huu katika viwanja vya Nyerere Square Mjini Dodoma .
MKUU wa wilaya ya Dodoma Mheshimiwa Christine Mndeme akikagua mabanda ya wadau wa utunzaji wa Mazingira kwa njia ya ufugaji nyuki. 
MKUU wa wilaya ya Dodoma Mheshimiwa Christine Mndeme akikagua mabanda ya wadau wa utunzaji wa Mazingira kwa njia ya kuchoma mkaa bila kukata miti badala yake wanatumia pumba. 
MKUU wa wilaya ya Dodoma Mheshimiwa Christine Mndeme akikabidhi vifaa vya usafishaji wa mazingira kwa viongozi wa vikundi vya usafishaji wa Mazingira Manispaa ya Dodoma 
MKUU wa wilaya ya Dodoma Mheshimiwa Christine Mndeme akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanavikundi vya usafishaji na utunzaji wa Mazingira Manispaa ya Dodoma. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI

MKUU wa wilaya ya Dodoma Mheshimiwa Christine Mndeme amekubali jukumu la kuwa mlezi wa vikundi mbalimbali vya usafi na utunzaji wa Mazingira vilivyopo katika Manispaa ya Dodoma, hatua ambayo pia itamuweka karibu zaidi na vikundi hivyo  katika kazi muhimu ya kuuweka mji  huo katika hali ya usafi na kuvutia ikizingatiwa kuwa ndio Makao Makuu ya Nchi na tayari Serikali imeshahamia mjini humo.

Mheshimiwa  Mndeme alitangaza hatua hiyo wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani Juni 5 mwaka huu kwa ngazi ya Wilaya yaliyofanyika katika viunga vya Bustani ya Nyerere Square mjini Dodoma.

Katika sherehe hizo, Mkuu huyo wa Wilaya pia alikagua mabanda ya wadau wa utunzaji wa Mazingira na  kugawa  vifaa mbalimbali vya kufanyia usafi  kwa vikundi nane vya usafi  vyenye thamani ya shilingi milioni 4.


Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede, Ofisa Mazingira wa Manispaa hiyo Dickson Kimari amabaye alimuwakilisha pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi, Ofisa Mazingira kutoka Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais Timotheo Mande pamoja na wadau wengine. 

Monday, June 5, 2017

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAPONGEZA JUHUDI ZA KUTUNZA MAZINGIRA MANISPAA YA DODOMA


Ofisa Mazingira wa Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais Timotheo Mande alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kwa ngazi ya Wilaya katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ Manispaa ya Dodoma.


Wawakilishi wa vikundi mbalimbali vya usafi na utunzaji wa Mazingira ktika Manispaa ya Dodoma wakiwa na vifaa vyao walivyokabidhiwa na Manispaa hiyo ili kuimarisha shughuli za Usafi na Utunzaji wa  Mazingira katika Manispaa hiyo. Vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 4 vilitolewa. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUAM-OFISI YA MKURUGENZI




OFISI ya Makamu wa Rais imepongeza jitihada zinazofanywa na Manispaa ya Dodoma katika kuuweka mji wa Dodoma katika hali ya usafi ikiwemo kuimarisha vikundi vya usafi kwa kuwapatia vifaa mbalimbali vya kufanyia usafi.

Pongezi hizo zilitolewa jana na Ofisa Mazingira wa Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais Timotheo Mande alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kwa ngazi ya Wilaya katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ Manispaa ya Dodoma.

Alielezea kufurahishwa na namna Manispaa inavyoshirikiana na kuvisaidia vikundi vya usafi na utunzaji wa Mazingira ambapo katika maadhimisho hayo alishuhudia vikundi nane vikikabidhiwa vifaa mbalimbali vya usafi vyenye thamani ya shilingi milioni 4.

WAFANYABIASHARA BUSTANI YA UHURU KUONDOLEWA



Bustani ya 'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma inavyoonekana kwa sasa ikiwa imezungukwa na wafanyabiashara ndogo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi Rasmi wa Bustani ya  'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 5.  Kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na kulia ni Meneja wa Benki ya Akiba inayohudumia Bustani hiyo John  Magigita.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya hafla ya Ufunguzi
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa hafla hiyo
Ofisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa  hiyo Godwin Kunambi akijibu  maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari wakati wa Hafla hiyo. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA



MKUU wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme amesema wafanyabiashara ndogo waliozunguka eneo la bustani ya Uhuru katika Manispaa ya Dodoma wataondolewa na kuhamishiwa katika masoko ya Sabasaba na Bonanza ili eneo hilo libaki wazi kwa ajili ya kuupezesha mji wa Dodoma na kuufanya uvutie zaidi ili kufikia lengo la kuboreshwa kwa bustani hizo.

Alitoa ahadi hiyo alipokuwa akifungua rasmi bustani hiyo leo Juni 5, 2017 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ Manispaa ya Dodoma.

Bustani hiyo inahudumiwa na Benki ya Biashara ya Akiba (ACB) kwa makubaliano maalum na Manispaa ya Dodoma, ambapo meneja wa tawi la Benki hiyo John Magigita imeeleza kuwa changomoto kubwa ni kuwabustani hiyo imezungukwa na wafanyabiashara ndogo hali inayopelekea kupoteza mvuto wake na kutoonekana vizuri.

Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede amesema Manispaa ya Dodoma itashirikiana na Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya katika kuwahamisha wafanyabiashara hao na kutafutia nafasi katika masoko mengine baada ya soko la majengo kujaa hali iliyopelekea wao kupanga bidhaa zao katika viunga vya bustani hiyo.

Naye Ofisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa  ya Dodoma ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika Hafla hiyo fupi ya ufunguzi, alisema kuwa Manispaa imejipanga kuhakikisha mji wa Dodoma unakuwa katika hali ya usafi muda wote kwani tayari Dampo jipya la kisasa la kuzika taka lililopo katika eneo ya Chidaya limeshaanza kazi na kwamba watendaji wa Kata watashirikishwa kikamilifu katika kusimamia sheria za usafi na mazingira katika maeneo yao.