Monday, June 5, 2017

WAFANYABIASHARA BUSTANI YA UHURU KUONDOLEWA



Bustani ya 'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma inavyoonekana kwa sasa ikiwa imezungukwa na wafanyabiashara ndogo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi Rasmi wa Bustani ya  'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 5.  Kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na kulia ni Meneja wa Benki ya Akiba inayohudumia Bustani hiyo John  Magigita.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya hafla ya Ufunguzi
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa hafla hiyo
Ofisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa  hiyo Godwin Kunambi akijibu  maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari wakati wa Hafla hiyo. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA



MKUU wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme amesema wafanyabiashara ndogo waliozunguka eneo la bustani ya Uhuru katika Manispaa ya Dodoma wataondolewa na kuhamishiwa katika masoko ya Sabasaba na Bonanza ili eneo hilo libaki wazi kwa ajili ya kuupezesha mji wa Dodoma na kuufanya uvutie zaidi ili kufikia lengo la kuboreshwa kwa bustani hizo.

Alitoa ahadi hiyo alipokuwa akifungua rasmi bustani hiyo leo Juni 5, 2017 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ Manispaa ya Dodoma.

Bustani hiyo inahudumiwa na Benki ya Biashara ya Akiba (ACB) kwa makubaliano maalum na Manispaa ya Dodoma, ambapo meneja wa tawi la Benki hiyo John Magigita imeeleza kuwa changomoto kubwa ni kuwabustani hiyo imezungukwa na wafanyabiashara ndogo hali inayopelekea kupoteza mvuto wake na kutoonekana vizuri.

Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede amesema Manispaa ya Dodoma itashirikiana na Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya katika kuwahamisha wafanyabiashara hao na kutafutia nafasi katika masoko mengine baada ya soko la majengo kujaa hali iliyopelekea wao kupanga bidhaa zao katika viunga vya bustani hiyo.

Naye Ofisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa  ya Dodoma ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika Hafla hiyo fupi ya ufunguzi, alisema kuwa Manispaa imejipanga kuhakikisha mji wa Dodoma unakuwa katika hali ya usafi muda wote kwani tayari Dampo jipya la kisasa la kuzika taka lililopo katika eneo ya Chidaya limeshaanza kazi na kwamba watendaji wa Kata watashirikishwa kikamilifu katika kusimamia sheria za usafi na mazingira katika maeneo yao.


No comments:

Post a Comment