Tuesday, November 28, 2017

UPIGAJI CHAPA MIFUGO WAENDELEA KUSHIKA KASI MANISPAA YA DODOMA


Ofisa mifugo wa Kata ya Chahanga katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma William Gervas akimpiga chapa Ng'ombe wakati wa zoezi la upigaji chapa mifugo linaloendelea katika Halmashauri hiyo.
                                                 

Monday, November 27, 2017

RC MAHENGE ATAKA MAMBO MATANO KUIPAISHA DODOMA

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamoga (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya kujitambulisha ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (wa tatu kulia) Wilayani humo. Wa kwanza kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Rehema Madenge na wa pili ni Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe. Kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Rehema Madenge  akizungumza wakati wa ziara ya kujitambulisha ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge katika Wilaya ya Dodoma ambapo alizungumza na watumishi wa Manispaa katika ukumbi wa Manispaa Novemba 24 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Dodoma kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (aliyevaa miwani katikati) wakati wa ziara ya kujitambulisha ya Mkuu huyo wa Mkoa katika Wilaya ya Dodoma. Wa kwanza kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Rehema Madenge na wa pili ni Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe. 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wakati alipokuwa katika ziara ya kujitambulisha katika Wilaya ya Dodoma Novemba 24 mwaka huu. Wa kwanza kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Rehema Madenge na wa pili ni Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA

.......................................

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge amewataka watumishi na viongozi wa Halmashauri Mkoani humo kuhakikisha wanayapa kipaumbele  mambo matano ikiwemo kudumisha hali ya Ulinzi na Usalama ambayo  ndiyo nguzo muhimu  inayopelekea shughuli nyingine za maendeleo kufanyika kwa ufanisi ili kuifanya Dodoma ikue kwa kasi.

Mambo mengine aliyoyayaorodhesha Mkuu huyo wa Mkoa kama dira ya kuharakisha maendeleo ni pamoja na utayari wa kubadilika kwa watumishi na kutofanya kazi kwa mazoea, utoaji wa huduma bora na zenye viwango kwa wananchi, kudumisha dhana ya Ushirikishwaji baina ya Taasisi na miongoni mwa watumishi, na kuepuka migogoro baina ya watumishi ndani ya Taasisi hali inayoweza kudumaza malengo ya Serikali katika kuwadumia wananchi.

Mkuu wa Mkoa Mahenge aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma alipofanya ziara ya kujitambulisha katika Wilaya ya Dodoma Novemba 24 mwaka huu.


Awali alipokea taarifa ya maendeleo ya Wilaya iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi kwa niaba ya Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamoga.

MACHINGA MANISPAA YA DODOMA KUKABIDHIWA ENEO RASMI HIVI KARIBUNI, BIBI KIZEE AISHUKURU MANISPAA

Bibi aliyejengewa nyumba na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma baada ya kuondolewa kwenye eneo la Makole D-Center lililotengwa na Manispaa kwa ajili ya Wafanyabiashara wadogo 'Machinga'  Elizabeth Sonyo mwenye umri wa miaka zaidi ya 75 akiwa nje ya makazi yake mapya katika Kata ya Makole Mjini Dodoma...........................................

WAFANYABIASHARA wadogo maarufu kama Machinga katika Manispaa ya Dodoma wanatarajiwa kupewa eneo lililotengwa  rasmi na Halmashauri ya Manispaa hiyo kwa ajili ya biashara zao lililopo katika Kata ya Makole mjini humo.

Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma chini ya Mkurugenzi Godwin Kunambi imekamilisha uwekaji wa miundombinu muhimu katika eneo hilo maarufu kama ‘Makole D-Center’ ikiwemo choo, ambapo wakati wowote wafanyabiashara hao watahamishiwa kwa utaratibu utakaoratibiwa na Manispaa kwa kushirikiana na uongozi wa wafanyabiashara hao.

Katika hatua za awali za maandalizi ya  eneo hilo, Halmashauri pamoja na mambo mengine, iliondoa makazi ya Bibi Elizabeth Sonyo aliyekuwa akiishi katika eneo hilo kinyume cha Sheria.

Hata hivyo, kutokana na Bibi huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 75 kutokuwa na uwezo wa kujenga, Manispaa ilibeba jukumu la kumjengea makazi mapya na bora zaidi katika eneo jingine, ambapo amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa kitendo hicho kwani hakuwa na uhalali wa kisheria wa kuishi katika hilo na kwamba angeweza kuondolewa bila kupewa msaada wowote.  

Kwa mujibu wa Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Ludigija Ndwata, kazi iliyobaki ni kuweka mawe maalum (gravels) katika eneo hilo ili livutie zaidi na liwe rafiki kwa wafanyabiashara na wateja, kabla ya matumizi kuanza.


Halmashauri ya Manispaa pia inaandaa eneo la ‘Chaduru D-center’ kwa ajili ya kulirasimisha kwa matumizi ya wafanyabiashara wadogo hususan akina mama wanaouza vyakula, mbogamboga, na matunda. 

Thursday, November 16, 2017

WAKAZI 8570 MKONZE MANISPAA YA DODOMA WAPATIWA HUDUMA YA MAJI SAFI YA BOMBA


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Mh. Vedasto Ngombale (wa tatu kushoto) akizungumza wakati Kamati hiyo ilipotembelea mradi wa Maji katika Kata ya Mkonze Manispaa ya Dodoma jana.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (wa pili kulia) akitoa ufafanuzi wakati alipowasilisha taarifa ya mradi wa Mkonze mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilipotembelea na kukagua mradi huo jana.

...............................................

WANANCHI 8570 wakazi wa Kata ya Mkonze katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wananufaika na huduma ya maji safi ya bomba kufuatia kukamilika kwa mradi wa Maji katika Kata hiyo ulitekelezwa na Manispaa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi iliyowasilishwa kweye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), mradi huo uliotekelezwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya kwanza, ulianza kujengwa Septemba, 2012 na kukamilika Machi, 2014 kwa gharama ya Shilingi 497,263,970 ukiwa na vituo 15 vya kutolea maji.

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilitembelea mradi huo jana na kuishauri Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kuharakisha taratibu za kukabidhi mradi huo kwa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) ambayo kwa mujibu wa sheria ndiyo yenye dhamana ya kutoa huduma ya Maji mjini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Vedasto Ngombale aliwaogoza wajumbe  wa Kamati yake katika ziara ya kukagua ufanisi wa mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati katika eneo la mradi, Mheshimiwa Ngombale ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kilwa Kaskazini, alisema ni muhimu mradi huo kuwa chini ya DUWASA kwani umeshakamilika na uko eneo la mjini, badala ya kuwa chini ya Manispaa na kusimamiwa na Jumuiya ya Watumiaji Maji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi aliahidi kutekeleza ushauri na maelekezo yote ya Kamati hiyo kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi yakamilike.


Tayari Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma iko katika hatua za mwisho za kukakabidhi mradi mwingine wa maji kwa DUWASA uliotekelezwa katika Kata ya Ng’hong’ona ukiwa katika hatua ya mwisho ya ukamilishwaji ambapo wananchi 8318 watanufaika na mradi huo wenye vituo 20 vya kutolea maji. 

Thursday, November 2, 2017

HALMASHAURI ZA DODOMA ZAPEANA SOMO, SHUGHULI YAANZIA MANISPAA YA DODOMA


Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wakifuatilia mkutano wa Baraza jana katika ukumbi wa Manispaa.
Baadhi ya Wageni Waalikwa wakifuatilia Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Robert Mwinje, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Dodoma White Zuberi (wa pili kushoto), na Mwneyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Danford Chisomi (wa pili kulia).  Kushoto ni Meya wa Jiji la Mbeya Mstahiki David Mwasilindi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Dodoma  Mheshimiwa White Zuberi Mwanzalila akitoa akijitambulisha kwa wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma jana.


..................................................
HALMASHAURI zote nane za Mkoa wa Dodoma zimekubaliana kuwa na utaratibu wa ziara za kubadilishana uzoefu hususan katika uendeshaji wa vikao na mikutano ikiwemo Baraza la Madiwani.

Hayo yalisemwa jana na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe wakati akiwatambulisha baadhi ya Wenyeviti na Wataalam wa Halmashauri za Wilaya za Mkoani humo waliohudhuria mkutano wa Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Dodoma ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wa ushirikiano huo.

Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Dodoma, ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa White Zuberi Mwanzalila ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mheshimiwa Danford Chisomi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mheshimiwa Samweli Kaweya na  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Rachel Chuwa.

Halmashauri zinazounda Mkoa wa Dodoma ni Manispaa ya Dodoma, Bahi, Chamwino, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa Mji, Kondoa Vijijini, na Chemba.