Wednesday, March 28, 2018

STENDI KUU DODOMA SASA RASMI NANENANE

Shughuli za usafirishaji zikiendelea katika iliyokuwa Stendi Kuu ya Mabasi Mjini Dodoma kabla ya Stendi hiyo kuhamishiwa katika eneo la Nanenane kuanzia leo Machi 29, 2018. Picha: Mtandao.


...............................................

HATIMAYE Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imetekeleza azimio la Mamlaka na wadau wa Usafirishaji katika ngazi ya Wilaya na Mkoa la kuhamishia Stendi Kuu ya mabasi katika eneo la Nanenane Kata ya Nzuguni Barabara Kuu ya Dodoma-Dar es Salaam, ambapo kuanzia leo Machi 29, 2018 huduma za mabasi hayo zimeanza kutolewa katika eneo hilo.

Uamuzi huo umefikiwa kufuata eneo lililokuwa likitumika kwa muda mrefu kama Stendi Kuu kuchukuliwa na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Nchini (RAHCO), kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafiri wa Reli.

Kufuatia hali hiyo, wadau mbalimbali wa usafirishaji wakiwemo Jeshi la Polisi, Wafanyabiashara ya Usafirishaji, Mamlaka inayosimamia usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA), Serikali ya Mkoa na Wilaya, pamoja na Manispaa walijadili suala hilo kwa nyakati tofauti na kukubaliana eneo la Nanenane litakidhi mahitaji ya huduma hiyo kwa sasa.

Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi aliteua ‘timu’ ya kushughulikia suala hilo na kumshauri eneo litakakidhi kutoa huduma ya usafiri wa Mikoani kwa Wananchi ili lipendekezwe, kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu ya msingi kama Maji na Vyoo, ambapo eneo la Nanenane lilipendekezwa kwani lilishawahi kutumika kama stendi katika miaka ya nyuma.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Ludigija Ndatwa amesema kuanzia leo mabasi yote ya Mikoani ni lazima yapakie na kushusha abiria wao katika stendi hiyo teule na kwamba wadau wote wameahidi kutoa ushirikiano.

“Hivi tunavyoongea nipo hapa Nanenane na wadau wote wapo hapa…wanatoa ushirikiano wa hali juu kwa kweli na kila kitu kinaenda sawa… mpaka muda huu mabasi yote yako huku kwa ajili ya kufanya safari zao” alisema Mhandisi Ludigija.


Thursday, March 8, 2018

MPANGO MKAKATI UCHUMI WA WANAWAKE DODOMA WAZINDULIWAMgeni Rasmi ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Fatma Tawfiq akionesha Mpango Mkakati wa kuwawezesha Wanawake Kiuchumi Manispaa ya Dodoma mara baada ya kuuzindua jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia iliyofanyika kwa ngazi ya Mkoa katika Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma. PICHA-OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Fatma Tawfiq akikata utepe Mpango Mkakati wa kuwawezesha Wanawake Kiuchumi Manispaa ya Dodoma mara baada ya kuuzindua jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia iliyofanyika kwa ngazi ya Mkoa katika Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma. PICHA-OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.
Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Manispaa ya Dodoma Hidaya Mizega (kulia) aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika maadhimisho ya kilele cha siku wa Wanawake Duniani iliyofanyika Kimkoa katika Kata ya Msalato Mjini Dodoma akizungumza wakati wa sherehe hizo. 
Diwani wa Kata ya Msalato Ally Mohamed akitoa neno wakati wa sherehe hizo
Kaimu wa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Dodoma Rukia Nyange akitoa neno.
Kikosi Maalum kikiongoza maandamano ya akina mama kutoka taasisi na wadau mbalimbali wakati wa sherehe za Maadhimisho ya kilele  cha Siku ya Wanawake duniani yaliyofanyika katika Kata ya Msalato Mnaispaa ya Dodoma jana kwa ngazi ya Mkoa
Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Fatma Tawfiq (wa pili kuhoto) akikagua maband ya Wajasiriamali Wanawake jana wakati wa Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Dunia iliyofanyika kwa ngazi ya Mkoa katika Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma. PICHA-OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA.

..................................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imezindua Mpango Mkakati wa kuwawezesha kiuchumi Wanawake na akina Mama wa Manispaa hiyo ili wajikwamue katika changamoto mbalimbali za maisha yao ya kila siku.

Mpango Mkakati huo unaotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018, ulizinduliwa jana Machi 8, 2018 ambapo sherehe za uzinduzi zilienda sambamba na maadhimisho ya kilele cha siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika katika Kata ya Msalato Mjini Dodoma.

Akizindua Mpango Mkakati huo, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Dodoma Fatma Tawfiq alitoa wito kwa Wanawake kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuwa kimoja ili kupambana na changamoto zinazowakabili ikiwemo za kiuchumi.
Aliwataka pia kuwa tayari kugombea na nafasi mbalimbali za uongozi ili wawe katika nafasi za maamuzi, na kwamba waanze na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Mwakani kabla ya ule Mkuu wa mwaka 2020.

Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi wa Manispaa ya Dodoma Hidaya Mizega ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika sherehe hizo alisemakuwa, Mpango Mkakati huo ndio dira ya kuwainua wanawake wa Manispaa ya Dodoma kiuchumi na kwamba yataandaliwa majukwaa mbalimbali ya Wanawake ili kuutambulisha kwa wadau.

“Wanawake wataongozwa jinsi ya kuunda vikundi vingi vya kuichumi ili kupata fursa mbalimbali wakiwa pamoja…kwa sasa Dawati la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi limeanzishwa katika kila Kata ya Manispaa ya Dodoma” alisema Mizega.

Alisema kuwa miongoni mwa malengo mahsusi ni kuwa na SACCOS ya akina mama wote wa Wilaya ya Dodoma, hivyo baada ya kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati huo kumalizika, itafanywa tathmini ya kina kuhusu mafanikio na changamoto zilizojitokeza ili zifanyiwe kazi.