Thursday, July 13, 2017

WATUMISHI WA ILIYOKUWA CDA WAPANGIWA VITUO VIPYA VYA KAZI SERIKALINI, WAZIRI WA TAMISEMI AWASOMEA TAASISI WALIZOPANGIWA



Mmoja ya watumishi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma akiuliza swali kwa Waziri wa Nchi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI  George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa mkutano na Waziri huyo jana katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma. 



SERIKALI imewapangia vituo vipya vya kazi watumishi 260 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) baada ya Mamlaka hiyo kuvunjwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli Mei 15 mwaka huu.

Rais Dokta Magufuli alilazimika kuivunja Mamlaka hiyo ili kuondoa mkanganyiko wa kimajukumu kati ya Mamlaka hiyo na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma hususan katika masuala ya umilikishaji wa ardhi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene alikutana na watumishi hao wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma jana na kuwasomea vituo walivyopangiwa katika taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa kujibu wa Waziri Simbachawene, watumishi 150 wamehamishiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, idadi ambayo ni zaidi ya nusu ya watumishi wote 260.
Watumishi 66 wamepangwa katika Mikoa na Wilaya mbalimbali Nchini, watumishi 16 wamehamishiwa katika Ofisi ya Rais TAMISEMI, mtumishi mmoja amepangwa katika Ofisi ya Rais Utumishi, na watumishi watatu wamehamishiwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Taasisi zingine ni Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo imepangiwa watumishi watatu, Wizara ya Ardhi watumishi wawili, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepangiwa mtumishi mmoja, watumishi wanne wamehamishiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Manispaa ya Dodoma na watumishi 14 wamehamishiwa katika kampuni inayosimamia mradi wa mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam (DART).


Kwa Mujibu wa Waziri Simbachawene, Watumishi wote waliopangiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa watakuwa wameshakabidhiwa barua zao za Uhamisho kufikia Julai 12 mwaka huu, ambapo wale waliopangiwa Serikali Kuu watakabidhiwa barua zao muda wowote kuanza sasa kabla ya kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi na kuendelea na majukumu watakayopangiwa.

No comments:

Post a Comment