Monday, August 8, 2016
Wednesday, August 3, 2016
BINTI WA KIDATO CHA SITA AUNGANA NA MH. RAIS DKT. JOHN MAGUFULI KATIKA KAMPENI YA MADAWATI, ATOA MSAADA WA MADAWATI 50 MANISPAA YA DODOMA
KATIKA hali
isiyotegemewa msichana mdogo Aisha Msantu ambaye ni muhitimu wa kidato cha
sita mwaka 2016 ameitikia wito wa Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli wa
kuwaomba wadau kushiriki katika zoezi la kuchangia madawati kwa ajili ya
wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari nchini ili waondokane na adha ya
kujifunza wakiwa wameketi chini.
Aisha ametoa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 katika shule ya Msingi ya Mwenge iliyopo katika kijiji cha Mbabala A Kata ya Mbabala Manispaa ya Dodoma, ambapo amesema hiyo ni ndoto yake ya muda mrefu na kwamba anafuraha kuikamilisha ili kuonesha alivyoguswa na tatizo la wanafunzi kukaa chini wakati wa kujifunza.
Mbali na msaada huo wa madawati, msichana huyo ambaye amezaliwa akiwa mlemavu, pia ametoa msaada wa mataulo maalum 84 kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule hiyo yenye thamani ya shilingi laki mbili, kama chachu ya kuwazindua wasijiingize katika masuala ya mahusiano kwa kudanganywa na wanaume kwa kuahidiwa mahitaji madogo.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika shuleni hapo juzi baada ya kupokea misaada hiyo kwa niaba ya Serikali na Manispaa ya Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme alimshukuru mtoto Aisha kwa msaada huo ambapo alisema msichana huyo ameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa watoto wenzake huku akitoa wito kwa jamii kujifunza kutokana na tukio hilo.
“Hakuna fedha isiyokuwa na kazi..Aisha ana mahitaji yake na angeweza kuzitumia fedha hizi kwa matumizi mengine ya binafsi lakini yeye ameamua kusaidia wadogo zake wa shule ya Msingi..hili ni jambo la kijasiri sana kwa mschana mdogo kama huyu na ni funzo kubwa kwa jamii nzima” alisema.
Akielezea ndoto aliyokuwa nayo mtoto wake kwa muda mrefu, mama mzazi wa Aisha Bi Rehema alisema mtoto wake huyo alifungua akaunti ya ‘Jumbo Junior’ katika Benki ya CRDB Dodoma na kuanza kujiwekea akiba kidogo kidogo hadi alipofikia azima yake hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura ameahidi kukarabati darasa moja katika shule hiyo ambako madawati hayo yatatumika, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Msichana Aisha ambaye kwa sasa ni Balozi wa Elimu wa Umoja wa Mataifa (UN) kupitia programu ya ‘4 Quality Education’.
Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mbabala Pascazia Mayala akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Boniface Michael akifungua shughuli kwa kuwakaribisha wageni.
Mama mzazi wa Aisha, Bi Rehema akielezea ndoto ya mtoto wake katika kusaidia jamii.
Wazazi wa Aisha, Mzee Msantu na Bi Rehema wakifuatilia shughuli ya Makabidhiano.
Mwakilishi wa programu ya '4 Quality Education' iliyo chini Umoja wa Mataifa Johnbest Mwahaja akitoa neno la shukrani kwa Aisha.
Mtoto Aisha (katikati) akitoa hotuba yake kabla ya kukabidhi madawati 50.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura akizungumza katika hafla hiyo ambapo aliahidi kukarabati darasa moja katika shule ya Msingi Mwenge ambako madawati hayo yatatumika ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za msichana huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kushoto) akimshukuru mtoto Aisha Msantu (kulia) baada ya kukabidhiwa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 kwa ajili ya shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Mbabala Manispaa ya Dodoma.
| Makabidhiano |
| Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kushoto) akiwakabidhi wanafunzi wa kike mataulo maalum 84 yaliyotolewa na Aisha. |
| Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo. |
| Mtoto Aisha Msantu akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo. |
| Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mbabala Pascazia Mayala akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo. |
| Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Boniface Michael akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo. |
Thursday, July 28, 2016
MANISPAA YA DODOMA YAFANYA VIZURI KWENYE MAKUSANYO YA KODI
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imefanikiwa kukusanya asilimia 80.28 ya mapato kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya ndani katika mwaka wa fedha 2015/2016 uliomalizika Juni 30 mwaka huu.
Katika mwaka huo wa fedha Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ilipanga kukusanya shilingi 4,566,075,181 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani (own sources) ambapo mpaka mwisho wa mwaka huo makusanyo halisi ni 3,665,699,279 sawa na asilimia 80.28 ya makisio.
Akizungumza katika kikao cha mwaka cha Baraza la Halmashauri ya Manispaa hiyo, Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa, mafanikio hayo yametokana na uchapaji kazi wa watendaji na madiwani wa Manispaa hiyo.
Mstahiki Mwanyemba aliwapongeza wote waliohusika kwa namna yeyote katika kufikia hatua hiyo huku akitoa wito kwa Ofisi ya Mkurugenzi na Madiwani wa kuimarishwa kwa juhudi zaidi katika ukusanyaji katika mwaka wa fedha 2016/2017.
"Mwaka mpya wa fedha umeshaanza hivyo Mkurugenzi na watendaji wako anzeni kukusanya kodi mapema...na waheshimiwa madiwani tuongeze nguvu katika kusimamia vyanzo vya mapato katika maeneo yetu" alisema.
Aidha, katika mkutano huo ambao kwa mujibu wa kanuni unakuwa na ajenda mbili tu ambazo ni kujadili taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri kwa mwaka uliopita na kupitia na kupitisha ratiba ya vikao vya Halamshauri kwa mwaka unaofuata, wajumbe walipitisha ratiba ya vikao vya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 .
Subscribe to:
Posts (Atom)