Friday, April 7, 2017

BANKI YA DUNIA YAKAGUA MIRADI MANISPAA YA DODOMA




 Mhandisi wa Mazingira Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida (katikati) akifafanua jambo wakati wa ziara ya ukaguzi wa Dampo la kisasa la kuhifadhi taka ngumu iliyofanywa na maafisa kutoka  Benki ya Dunia jana Aprili 6, 2017.


Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia  (katikati) akishudia kazi ya kumwaga na kuhifadhi taka ngumu katika Dampo la kisasa lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma wakati yeye na ujumbe wake walipofanya ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo jana April 6.  Wa pili Kulia  (mwenye suti) ni Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Lusako Kilembe na wa pili kushoto ni Mhandisi wa Mazingira Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida. 

Kazi ya umwagaji na uhifadhi wa taka ngumu ikiendelea katika Dampo la Chidaya


Kazi ya umwagaji na uhifadhi wa taka ngumu ikiendelea katika Dampo la Chidaya.


Barabara ya 'Independence Square' ni miongoni miradi ya barabara za mji wa Dodoma iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya Dunia


TIMU ya maafisa kutoka Benki ya Dunia wamefanya ziara ya kukagua mradi  wa dampo la kisasa na Barabara zinazofadhiliwa na Benki hiyo katika Manispaa ya Dodoma chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Miji Tanzania (TSCP).

Ziara hiyo ilifanyika jana April 6, 2017 ambapo timu hiyo ilitembelea eneo la Chidaya unakotekelezwa mradi wa dampo la kisasa linalotumia teknolojia ya kuzika taka (Land Fill) na kufurahishwa na maendeleo ya mradi ambao umeashaanza kufanya kazi huku ujenzi ukiwa katika hatua za mwisho.

Aidha ujumbe huo ulitembelea barabara zilizojengwa chini ya mradi huo unaotekelezwa katika Manispaa Saba Tanzania Bara pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).



Awali ujumbe huo ulikutana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi na kufanya nae mazungumzo mafupi, ambapo aliishukuru Benki ya Dunia kwa kusaidia kuboresha miundombinu katika Manispaa ya Dodoma huku akiiomba kuendelea kutoa ufadhili zaidi ili kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa kisasa zaidi hivyo kuendana na hadhi yake ya kuwa makao makuu ya Nchi.



Monday, April 3, 2017

MEYA WA MANISPAA YA DODOMA AVULIWA MADARAKA

                                                                           

 Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa mkutano maalum cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo jana Aprili 3 ambapo uamuzi wa kumvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo ulifikiwa. Kulia ni Mbunge wa dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi Ajira na Vijana Mh. Anthony Mavunde na wa pili Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Christina Mndeme. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.

Wajumbe wakifuatilia mkutano



BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Dodoma limemvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba kwa tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi yaliyopelekea upotevu wa shilingi milioni 30 za mradi wa Maji wa Kata ya Zuzu zilizotolewa na Serikali ya Japan kupitia ubalozi wake nchini Tanzania.

Hatua hiyo ilifikiwa katika mkutano wa dharura wa Bazara hilo ulioitishwa jana Aprili tatu katika ukumbi wa Manispaa ili  kupokea na kujadili taarifa ya Tume Maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana kuchunguza tuhuma hizo.

Baada ya Katibu wa mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi kuwasilisha taarifa hiyo, wajumbe waliazimia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya huyo, ambapo kati ya kura 48 zilizopigwa, kura 43 ziliunga mkono hoja hiyo huku kura 4 zikipinga na moja ikiharibika.


Kufuatia hali hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede atakaimu nafasi ya Meya kwa mujibu wa Kanuni katika kipindi cha mpito kisichozidi siku 60, ambapo uchaguzi wa kumpata Meya mpya utafanywa.

Wednesday, March 29, 2017

MLYAMBATE Blog : WAKURUGENZI WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA WACHAG...: Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa kote nchini kwa kauli moja wameridhia na kuwachagua viongozi watakaowawakilisha katika ku...
MLYAMBATE Blog : TOVUTI ZA SERIKALI HEWANI RASMI: TOVUTI ZA SERIKALI KUBORESHA USIMAMIZI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI Sekretarieti za mikoa yote 26 ya Tanzania Bara  na Halmashauri zake 18...

Wednesday, March 8, 2017

AUSTRIA KUWEKEZA DODOMA

Naibu Meya wa Jiji la Linz Austria Detlef Wimmer (aliyesimama) akitoa hotuba yake

Mtaalam wa ujenzi katika dampo la taka la kisasa lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma akitoa maelezo ya mradi kwa Naibu Meya wa jji la Linz la Austria Detlef Wimmer (wa pili kushoto). Kushoto ni Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Jaffar Mwanyemba na wa  pili kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi



Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Jaffar Mwanyemba akizungumza na Wanahabari kuhusu ushirikiano wa Manispaa hiyo na jiji la Linz la Austria


Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi  akizungumza na Wanahabari kuhusu ushirikiano wa Manispaa hiyo na jiji la Linz la Austria


Ziara katika shamba la zabibu


Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Jaffar Mwanyemba na Naibu Meya wa jiji la Linz la Austria Detlef Wimmer wakisaini hati ya makubaliano ya mashirikiano.

Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Jaffar Mwanyemba na Naibu Meya wa jiji la Linz la Austria Detlef Wimmer wakionesha hati ya makubaliano ya mashirikiano mara baada ya kusaini.

Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Jaffar Mwanyemba (wa pili kulia waliokaa) na Naibu Meya wa jiji la Linz la Austria Detlef Wimmer (wa pili kushoto waliokaa) wakiwa katika picha pamoja na baadhi ya watumishi manispaa hizo. Wa kwanza kulia waliokaa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi na kwanza kushoto waliokaa  ni Kamishna Mkuu wa Jeshi la Zimamoto Tanzania Thobias Andengeye.  PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI, DMC






RAMADHANI JUMA
OFISI YA MKURUGENZI, DMC

Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na jiji la Linz la nchini Austria zimesaini hati ya makubaliano (Memorandum of Understanding) ya ushirikiano katika nyanja za Utunzaji wa Mazingira, kuimarisha huduma za kijamii, uwekezaji wa kibiashara, kuimarisha miundombinu na teknolojia, na kuimarisha huduma ya kupambana na majanga ya moto na uokozi.

Maeneo mengine ambayo mamlaka hizo mbili zimekubaliana kushirikiana ni pamoja kutoa mafunzo mbalimbali wa watumishi wake na Madiwani wa pande zote mbili, kubadilishana watumishi pamoja na kushirikiana katika jambo lolote litakaloonekana kuwa na manufaa kwa wananchi wa pande zote.

Makubaliano hayo yalifikiwa hivi karibuni wakati wa  ziara ya siku moja ya  Naibu Meya wa jiji la Linz Detlef Wimmer na ujumbe wake katika Manispaa ya Dodoma ambapo alitembelea maeneo kadhaa ikiwemo Dampo la kisasa la takataka lililopo katika kijiji cha Chidaya kata ya Ntyuka Manispaa ya Dodoma na shamba la zabibu katika kata ya Mtumba ili kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Akisaini makubaliano hayo kwa niaba ya Manispaa ya Dodoma, Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba alisema ushirikiano huo umekuja wakati muafaka na kwamba utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa miji hiyo huku akitoa wito kwa marafiki na wawekezaji wengine  kujitokeza kwani mji wa Dodoma kwa sasa umefunguka na kwamba ni wakati muafaka wa kuwekeza Dodoma.

 Kwa upande wake Naibu Meya wa jiji la Linz Detlef Wimmer ambaye alisaini hati hiyo kwa niaba ya mamlaka ya jiji hilo alielezea kuvutiwa kwake na mji wa Dodoma na kwamba amejifunza mengi katika ziara yake huku akiahidi ushirikiano wa dhati katika maeneo waliyokubaliana.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alisema ushirikiano kati ya Manispaa ya Dodoma na Jiji la Linz ni mwanzo tu wa juhudi zinazofanywa na Manispaa katika kuweka mazingira rafiki  kwa wawekezaji mbalimbali ili kuhakikisha Manispaa hiyo inakua kwa kasi huku huduma za kijamii zikipewa kipaumbele kwa manufaa ya wakazi wake na hata wa mikoa ya  jirani.



Tuesday, December 6, 2016

LAPF 'YAIPIGA TAFU' MANISPAA YA DODOMA



Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi





















MFUKO wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF) umekabidhi hundi ya Sh. 6 milioni kwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kutatua tatizo la uhaba wa maji katika maeneo ya Ihumwa na Mtumba ndani ya Manispaa hiyo.
Akikabidhi  hundi hiyo kwa Godwin Kunambi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma mjini humo, James Mlowe ambaye ni Meneja Mawasiliano na Masoko wa LAPF amesema, mfuko huo umetoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kufufua visima vya maji vilivyoharibika.

Amesema mfuko huo ulipokea maombi kutoka katika Ofisi ya Manispaa pamoja na ofisi ya mbunge
kupatiwa msaada wa kutengeneza visima vya maji katika Kata ya Ihumwa na Mtumba kutokana na visima hivyo kuharibika na kuwasababishia usumbufu wa kukosea maji wakazi hao.
Amesema LAPF kama taasisi ya serikali, imekuwa ikifanya shughuli nyingi na halmashauri mbalimbali nchini hususani shughuli za maendeleo.

“Kwa sasa Dodoma ni Makao Mkuu ya Nchi hivyo kuna watu wengi watahamia hivyo hakuna sababu ya kuwepo ukosefu wa maji.

“Kadri watu wanavyoongezeka ndivyo mahitaji yanavyoongezeka hivyo mahitaji ya maji ni makubwa zaidi katika Mji wa Dodoma na Ihumwa na Mtumba ni sehemu mahitaji hayo,” amesema Mlowe.

Hata hivyo Mlowe amesema, pesa zinazotolewa na taasisi mbalimbali pamoja na wahisani ni vyema zikatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuzibadilishia matumizi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi  wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema katika uongozi wake, atahakikisha miradi yote iliyokusudiwa inafanyika.

“Ni kweli kwa sasa Dodoma kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa maji katika maeneo ambayo yapo nje ya mji".

“Msaada ambao tumeupata kutoka LAPF utasaidia kuboresha na kukarabati visima vya maji ili wananchi waondokane na adha ya upatikanaji wa maji,”alisema Kunambi.

KWA MSAADA WA MWANAHALISI ONLINE.com