Tuesday, February 6, 2018

MANISPAA YA DODOMA YAWEKA MKAKATI KUFAULISHA WOTE SHULE ZA MSINGI KUANZIA 2018


Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mwikongi Kigosi (kushoto) akiwasilisha taarifa ya ya maendeleo ya Elimu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta  Binilith Mahenge wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa katika Manispaa ya Dodoma hivi karibuni. 

 .................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imeweka mkakati kabambe utakaowezesha kufikia lengo la ufaulu wa asilimia 100 kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi kuanzia mwaka 2018.

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya Manispaa hiyo iliyowasilishwa na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Manispaa ya Dodoma Mwikongi Kigosi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Elimu na Afya hivi karibu katika Manispaa hiyo.

Kwa kujibu wa taarifa hiyo, miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wote wanamudu stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu katika madarasa ya chini kabla ya kujiunga na madarasa yanayofuata.

Kigosi alisema mkakati mwingine ni kusimamia mahudhurio ya Walimu na Wanafunzi pamoja na kudhibiti matumizi ya simu kwa Walimu wawapo darasani.
Aidha, alisema Idara ya Elimu Msingi itateua shule 25 za serikali ambazo zitashindanishwa na shule za binafsi ili kubadilishana uzoefu na kuinua ufaulu katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Vilevile alisema Idara imejipanga kuimarisha ufuatiliaji wa ufundishaji na kusimamia utendaji kazi wa walimu, sambamba na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri.

“Pia tutakuwa na mitihani, mazoezi na majaribio ya kufikirisha, pamoja na kambi za masomo… haya yote tutayafanya na tunaamini yatatupa matokeo tunayotarajia” alisema Kigosi.

Kwa mwaka 2017 jumla ya Wanafunzi 9,509  wakiwemo Wavulana 4,500 na Wasichana 5,009 walifanya mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi katika Manispaa ya Dodoma ambapo Wanafunzi 6,488  wakiwemo Wavulana 3034 na Wasichana 3454 walifaulu, sawa na asilimia 68.

No comments:

Post a Comment