 |
| Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani la kufunga mwaka wa fedha 2016/2017 uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Manispaa ya Dodoma. |
........................................................................................
HALMASHAURI ya Manispaa
ya Dodoma imetenga eneo la Makole D-Center lililoko katikati ya Mji wa Dodoma kuwa
eneo rasmi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo maarufu kama Machinga kufanya
biashara zao badala ya kupaga bidhaa ovyo mitaani hali inayopelekea kuharibu
taswira ya mji.
Hatua hiyo pia
itasaidia kuendana na kasi kubwa ya ongezeko la wafanyabiashara hao kuingia
Mjini humo kutoka mikoa mbalimbali nchini tangu Serikali ilipohamia rasmi Dodoma
ambako ni Makao Makuu ya Nchi.
Akizugumza katika
mkutano wa Baraza la Madiwani la kufunga wa fedha uliopita lililofanyika
mwishoni mwa wiki iliyopita katika
ukumbi wa Manispaa hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin aliyewajulisha
wajumbe na wananchi kuwa, sasa Manispaa iko katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi
wa miundombinu muhimu katika eneo hilo ikiwemo
vyoo ili shughuli za biashara zifanyike katika mazingira salama na rafiki.
“Tunatarajia eneo hilo
litakuwa tayari kufikia mwisho wa mwezi Agosti au mwanzo wa mwezi Septemba
mwaka huu mara moja tutaanza zoezi la kuwahamishia wafanyabiashara hao pale”
alifafanua.
Alisema Manispaa inashirikiana
kwa karibu na viongozi wa wafanyabiashara hao katika zoezi hilo, na kwamba
endapo eneo hilo halitatosha, wafanyabiashara wengine watahamishiwa katika eneo
la Chaduru .
Tayari Manispaa ya
Dodoma ilishaanza zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wa Matunda na chakula
katika maeneo yasiyo rasmi na kuwahamishia katika maeneo rasmi ya masoko
ikiwemo soko la Sabasaba, Bonanza, na Tambukareli.