Friday, September 29, 2017

MANISPAA YA DODOMA YAANZA KUANDAA HATI MILIKI ZA ARDHI ZA MIAKA 99 KWA KASI, BARAZA LA MADIWANI LAPONGEZA


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi


.........................................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imekamilisha uandaaji wa hati 912 za umiliki wa ardhi za miaka 99 kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli Mei 15 mwaka huu wakati akitoa tamko la kuivunja iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na shughuli zote kuhamishiwa katika Manispaa ya Dodoma.

Akizungumza katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichopokea taarifa rasmi ya makabidhiano ya majukumu ya iliyokuwa CDA kuhamia Manispaa ya Dodoma jana, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi aliwaambia Madiwani na wananchi kwa ujumla waliohudhuria Baraza hilo kuwa, hatua hiyo imefikiwa katika kipindi cha miezi miwili ya Julai na Agosti, huku akiahidi  kuwa,Manispaa hiyo itaendelea kutoa huduma hiyo na nyingine kwa kasi inayoendana na matarajio ya wananchi.

Alisema kati ya hati hizo, hati 674 zilizowasilishwa kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi zimeshasajiliwa na zipo tayari kwa ajili ya kukabidhiwa kwa wananchi husika, huku hati 238 zikiwa katika hatua ya kukaguliwa ili zisainiwe.
Alifafaua zaidi kuwa, uandaaji huo wa hati unaenda sambamba na utoaji wa vibali vya ujenzi kwa haraka, ambapo mchakato wa kutoa kibali cha ujenzi unakamilishwa ndani ya siku saba tu baada ya maombi kupokelewa mpaka muombaji anakabidhiwa kibali chake.

Kufuatia taarifa hiyo, wajumbe wa Baraza la Madiwani wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe wameipongeza Menejimenti ya Halmashauri na watumishi wote na kuwataka waendelee na juhudi hizo ili pamoja na mambo mengine kuufanya mji wa Dodoma ukue kwa kasi kwa kuwawezesha wananchi na wadau wengine kujenga.



Monday, September 25, 2017

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA SEMINA YA SIKU MOJA YA WENYEVITI NA WATENDAJI WA MITAA MANISPAA YA DODOMA SEPTEMBA 16, 2017 KATIKA UKUMBI WA ST GASPER MJINI DODOMA

Baadhi ya Wakuu wa Idara na wajumbe wengine wakifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo.
Baadhi ya Wenyeviti na Watendaji wakifuatilia Semina. 
Afisa kutoka Idara ya Utumishi na Utawala Agatha Kalesu akitoa mada kuhusu majukumu ya Wenyeviti wa Mitaa.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Joachim Henjewele akitoa mada.

Mchumi wa Manispaa Shaaban Juma akitoa mada.

Mganga Mkuu wa Manispaa Thom Mtoi akitoa mada.
Mmoja ya wajumbe akichangia mada.

Mmoja ya Wajumbe akitoa mchango wake.

Monday, September 18, 2017

WENYEVITI NA WATENDAJI WA MITAA NA VIJIJI MANISPAA YA DODOMA WAPIGWA MSASA


Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (aliyesimama kulia) akizungumza wakati alipoongoza semina elekezi ya siku moja kwa Wenyeviti na Watendaji wa Mitaa na Vijiji wa Manispaa ya Dodoma Septemba 16 mwaka huu katika Ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma. PICHA NA OFISI YA MKURUGENZI 



Monday, September 4, 2017

ARDHI YOTE MANISPAA YA DODOMA KUPIMWA NDANI YA MIAKA MIWILI


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Manispaa juzi ambapo alizungumzia mambo mbalimbali ikiwemo malengo ya upimaji wa ardhi/viwanja.

..................................................................

KAZI ya upimaji wa eneo lote la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili ijayo hali itakayoufanya mji wa Dodoma kuwa katika mandhari bora na ya kuvutia.

Mpango huo umewekwa wazi na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alipozungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Manispaa juzi.
Alisema miradi ya upimaji wa ardhi katika utekelezwaji wa lengo hilo haitafanywa na Manispaa pekee bali  itashirikisha taasisi mbalimbali zenye uzoefu wa miradi ya aina hiyo.
Alifafanua kuwa, mbali na kushirikisha taasisi za Umma na binafsi, Manispaa ya Dodoma ina mkakati wake wa upimaji na tayari baadhi ya Kata zimeshaanza kupimwa ambapo pia, upo mkakati wa kuongeza nguvu kazi kwa upande wa watumishi kwa kuajiri wataalamu wa ardhi kwa mikataba ya muda ili kufikia lengo lililowekwa kwa wakati.

Manispaa ya Dodoma inaundwa na Kata 41, ambapo ina jumla ya eneo la mraba 2,769, ambapo zaidi ya nusu ya eneo hilo bado halijapimwa.



Monday, August 21, 2017

MEYA WA MANISPAA YA DODOMA PROF DAVIS MWAMFUPE ATOA SOMO MAONESHO YA NANENANE

HALMASHAURI za Manispaa na Wilaya katika mikoa ya Kanda ya  Kati unayoundwa  na mikoa ya Dodoma na Singida kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaounga mkono shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi wameshauriwa kubuni njia rahisi inayoweza  kuwafikishia kwa wakulima na wafugaji elimu inayopatikana kwenye viwanja vya Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane.
Rai hiyo imetolewa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe  kufuatia maenesho ya Nanenane yaliyomalizika hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo amesema bado Maonesho hayo  hususan Kanda ya Kati hayajafanikiwa kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwa kiasi kinachoridhisha na kuwawezesha kubadili shughuli zao na kuzifanya kuwa na tija inayoridhisha.
Alisema Maonesho ya Nane Nane yamekuwepo kwa miaka mingi katika Kanda mbalimbali nchini na yamekuwa na mambo ya kuvutia sana hususani Teknolojia na mbinu bora za uzalishaji katika kilimo na mifugo ambazo zinauwezo wa kuleta tija kubwa lakini bado changamoto kubwa ni kwamba mambo yote bora na mazuri yanayopatikana kwenye Maonesho hayajaweza kumfikia mkulima kwenye ngazi za msingi kwa maana ya ngazi ya kaya na vijiji.
Alisema kuwa, unaweza kutoka umbali usiozidi kilomita mbili tu kutoka kituo (Uwanja) cha Maonesho kilipo utashangaa kukuta mkulima analima kilimo cha kienyeji ambacho hakina manufaa.
 “Teknolojia inayooneshwa kwenye Maonesho haya bado haijaweza kuwafikia wakulima na wafugaji wetu kwenye vijiji vyao wanakoendesha shughuli zao za kilimo na mifugo” alisema Profesa Mwamfupe na kuongeza kuwa, bado teknolojia na ubunifu unaopatikana kwenye Maonesho haya unahitaji kuwafikia wakulima wa chini kabisa.
Alitoa wito kwa Mamlaka zinazohusika kuhakikisha Kiwanja cha Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati kilichopo katika Kata ya Nzuguni Manispaa ya Dodoma  kinakuwa kituo cha Shamba Darasa la kilimo mifugo na uvuvi cha kudumu ili  wataalamu wa kilimo na mifugo wawepo kituoni hapo kipindi chote cha mwaka wakisimamia shughuli za kilimo na mifugo kituoni hapo na Halmashauri zilete Wakulima na Wafugaji wao kujifunza na kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za uzalishaji.

 
Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe (wa kwanza kulia) akishuhudia mmoja ya banda la maonesho alipotembelea Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati katika Viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma hivi karibuni.

Thursday, August 17, 2017

MANISPAA YA DODOMA YATENGA ENEO MAALUM LA MACHINGA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani la kufunga mwaka wa fedha 2016/2017 uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Manispaa ya Dodoma.

........................................................................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imetenga eneo la Makole D-Center lililoko katikati ya Mji wa Dodoma kuwa eneo rasmi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo maarufu kama Machinga kufanya biashara zao badala ya kupaga bidhaa ovyo mitaani hali inayopelekea kuharibu taswira ya mji.

Hatua hiyo pia itasaidia kuendana na kasi kubwa ya ongezeko la wafanyabiashara hao kuingia Mjini humo kutoka mikoa mbalimbali nchini tangu Serikali ilipohamia rasmi Dodoma ambako ni Makao Makuu ya Nchi.

Akizugumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani la kufunga wa fedha uliopita lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita  katika ukumbi wa Manispaa hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin aliyewajulisha wajumbe na wananchi kuwa, sasa Manispaa iko katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa  miundombinu muhimu katika eneo hilo ikiwemo vyoo ili shughuli za biashara zifanyike katika mazingira salama na rafiki.

“Tunatarajia eneo hilo litakuwa tayari kufikia mwisho wa mwezi Agosti au mwanzo wa mwezi Septemba mwaka huu mara moja tutaanza zoezi la kuwahamishia wafanyabiashara hao pale” alifafanua.

Alisema Manispaa inashirikiana kwa karibu na viongozi wa wafanyabiashara hao katika zoezi hilo, na kwamba endapo eneo hilo halitatosha, wafanyabiashara wengine watahamishiwa katika eneo la Chaduru .


Tayari Manispaa ya Dodoma ilishaanza zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wa Matunda na chakula katika maeneo yasiyo rasmi na kuwahamishia katika maeneo rasmi ya masoko ikiwemo soko la Sabasaba, Bonanza, na Tambukareli.