Wednesday, April 11, 2018

MANISPAA YAZIDI KUING’ARISHA MAKAO MAKUU


Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro akikagua moja ya vifaa vipya vilivyowekwa katika Mtaa wa Kuu kwa ajili kutunza uchafu ikiwa ni juhudi za Manispaa hiyo kuhakikisha Mji unakuwa safi wakati wote.

Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro (kulia) akisimamia uwekaji wa vifaa vipya vya kutunzia uchafu ikiwa ni juhudi za Manispaa hiyo kuhakikisha Mji unakuwa safi wakati wote. Kushoto ni Afisa Mazingira Ally Mfinanga.



Moja ya vifaa vya kutunzia taka kilichopo mkabala na Viwanja vya Nyerere katikati ya Mji.

..................................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma kupitia Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafi kwa kuongeza vifaa vya  kutunza uchafu katika mitaa kadhaa ya Mji ili kuhakikisha Wananchi hawatupi taka ovyo wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku.

Akizungumza wakati wa uwekji wa vifaa hivyo, Mkuu wa Idara hiyo Dickson Kimaro alisema Manispaa inatarajia  kuongeza  ‘vitunza uchafu’ 11 katika mitaa mbalimbali ili kuweka mazingira rafiki ya kutunza uchafu kwa Wakazi wa Mji wanaokuwa katika shughuli zao za kila siku.

“Hizi ni juhudi za makusudi ili kuhakikisha Mji wetu unakuwa safi muda wote…natoa wito kwa Wakazi wa Manispaa yetu watumie vifaa hivi kuhifadhia uchafu mdogo wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku” alisema Kimaro.

Alisema mbali na vifaa hivyo, tayari Manispaa ilishasambaza vifaa vikubwa vya kukusanyia taka za aina zote (Skip Bucket) 61 katika Kata mbalimbali zinazotumika kama vituo vya kukusanyia taka kabla ya kubebwa na Mitambo ya Manispaa na kupelekwa katika Dampo la Kisasa lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu nje kidogo ya Mji.

No comments:

Post a Comment