Wednesday, August 3, 2016

MICHUZI BLOG: MTOTO ATOA MSAADA WA MADAWATI DODOMA

BINTI WA KIDATO CHA SITA AUNGANA NA MH. RAIS DKT. JOHN MAGUFULI KATIKA KAMPENI YA MADAWATI, ATOA MSAADA WA MADAWATI 50 MANISPAA YA DODOMA

KATIKA hali isiyotegemewa msichana mdogo Aisha Msantu ambaye ni muhitimu wa kidato cha sita mwaka 2016 ameitikia wito wa Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli wa kuwaomba wadau kushiriki katika zoezi la kuchangia madawati kwa ajili ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari nchini ili waondokane na adha ya kujifunza wakiwa wameketi chini.

Aisha ametoa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 katika shule ya Msingi ya Mwenge iliyopo katika kijiji cha Mbabala A Kata ya Mbabala  Manispaa ya Dodoma, ambapo amesema hiyo ni ndoto yake ya muda mrefu na kwamba anafuraha kuikamilisha ili kuonesha alivyoguswa na tatizo la wanafunzi kukaa chini wakati wa kujifunza.

Mbali na msaada huo wa madawati, msichana huyo ambaye amezaliwa akiwa mlemavu, pia ametoa msaada wa mataulo maalum 84 kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule hiyo yenye thamani ya shilingi laki mbili, kama chachu ya kuwazindua wasijiingize katika masuala ya mahusiano kwa kudanganywa na wanaume kwa kuahidiwa mahitaji madogo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika shuleni hapo juzi baada ya kupokea misaada hiyo kwa niaba ya Serikali na Manispaa ya Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme alimshukuru mtoto Aisha kwa msaada huo ambapo alisema msichana huyo ameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa watoto wenzake huku akitoa wito kwa jamii kujifunza kutokana na tukio hilo.

“Hakuna fedha isiyokuwa na kazi..Aisha ana mahitaji yake na angeweza kuzitumia fedha hizi kwa matumizi mengine ya binafsi lakini yeye ameamua kusaidia wadogo zake wa shule ya Msingi..hili ni jambo la kijasiri sana kwa mschana mdogo kama huyu na ni funzo kubwa kwa jamii nzima” alisema.

Akielezea ndoto aliyokuwa nayo mtoto wake kwa muda mrefu, mama mzazi wa Aisha Bi Rehema alisema mtoto wake huyo alifungua akaunti ya ‘Jumbo Junior’ katika Benki ya CRDB Dodoma na kuanza kujiwekea akiba kidogo kidogo hadi alipofikia azima yake hiyo.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura ameahidi kukarabati darasa moja katika shule hiyo ambako madawati hayo yatatumika, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Msichana Aisha ambaye kwa sasa ni Balozi wa Elimu wa Umoja wa Mataifa (UN) kupitia programu ya ‘4 Quality Education’.


 Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mbabala Pascazia Mayala akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano.

 Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Boniface Michael akifungua shughuli kwa kuwakaribisha wageni. 

 Mama mzazi wa Aisha, Bi Rehema akielezea ndoto ya mtoto wake katika kusaidia jamii.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma Hyasinta Jonas akitoa salamu wakati wa hafla hiyo

 Wazazi wa Aisha, Mzee Msantu na Bi Rehema wakifuatilia shughuli ya Makabidhiano.

 Mwakilishi wa programu ya '4 Quality Education' iliyo chini Umoja wa Mataifa Johnbest Mwahaja akitoa neno la shukrani kwa Aisha.

 Mtoto Aisha (katikati) akitoa hotuba yake kabla ya kukabidhi madawati 50.

 Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura akizungumza katika hafla hiyo ambapo aliahidi kukarabati darasa moja katika shule ya Msingi Mwenge ambako madawati hayo yatatumika ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za msichana huyo.

 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kushoto) akimshukuru mtoto Aisha Msantu (kulia) baada ya kukabidhiwa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 kwa ajili ya shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Mbabala Manispaa ya Dodoma.

Makabidhiano

Mtoto Aisha (wa pili kushoto) na wazazi wake Mzee Msantu (wa kwanza kulia) na Bi Rehema (wa pili kulia) wakiwa wameketi katika madawati hayo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme kushoto.


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kushoto) akiwakabidhi wanafunzi wa kike mataulo maalum 84 yaliyotolewa na Aisha.

Msichana Aisha Msantu (wa kwanza kulia) akiongoza wageni kwenye shughuli ya upandaji miti ya kumbukumbu katika shule ya Msingi Mwenge Manispaa ya Dodoma baada ya kukabidhi msaada wa madawati 50 katika shule hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 5.2


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.

Mtoto Aisha Msantu akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.


Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mbabala Pascazia Mayala akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Boniface Michael akipanda mti wa kumbukumbu shuleni hapo.