Monday, July 30, 2018

JIJI LA DODOMA LATOA MILIONI 950 KWA WANAWAKE NA VIJANA, WAZIRI JAFO AKABIDHI HUNDI

....................................................................

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 950 zilizotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoka katika Mfuko wa Wanawake, Vijana, na Walemavu kwa ajili ya vikundi 234 vya Wanawake na Vijana huku akitoa wito kwa Jiji hilo kutafuta masoko ya bidhaa  zinazozalishwa na vikundi hivyo kwani imekuwa moja ya changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Hafla ya kukabidhi hundi hiyo kwa Wanavikundi hao imefanyika hivi karibuni katika Viwanja vya Nyerere vilivyopo katikati ya Jiji la Dodoma.

‘’Viongozi muandae Mpango Mkakati wa kuwa na masoko ya kuuza bidhaa za wajasiriamali hawa, nimeona wana bidhaa nzuri sana ambazo unaweza usiamini kama zinatoka Dododma, lakini kila mmoja ukimuuliza soko anakwambia hana soko maalumu’’ Alisema Waziri Jafo.

Aliongeza ‘’Mbali na kuwapa fedha lakini pia nakuagiza Mkurugenzi wa Jiji (Godwin Kunambi ) na Mstahiki Meya (Profesa David Mwamfupe) mtafute eneo la kimkakati kwa ajili ya hawa mnaowapatia mkopo na vikundi vyote vilivyowezeshwa na Halmashauri hii, kwa kufanya hivi tunaweza kuwa na eneo moja maalumu ambalo litakuwa linafanya maonyesho kwa mwaka mzima’’ Alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alimweleza Waziri Jafo kuwa, fedha hizo zinatokana na ukusanyaji bora wa mapato ya ndani na kwamba kwa sasa Halmashauri inatoa mikopo mikubwa kuanzia Shilingi milioni moja hadi milioni kumi na kutoa wito kwa wajasiriamali kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kukidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.

Alisema fedha hizo zinatolewa kwa vikundi 234 vya Wajasiriamali, vikiwemo 168 vya Wanawake pamoja na vikundi 66 vya Vijana.


Thursday, July 12, 2018

MKATABA WA KIHISTORIA DODOMA YA KIJANI WASAINIWA

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo wakisaini hati ya makubaliano ya kupanda na kustawisha miti, na kuhifadhi misitu iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuikijanisha Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania  (TFS) Professa Dos Santos Silayo wakikabidhiana hati ya makubaliano.


Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) akifafanua jambo mbele ya Mtendaji Mkuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo kuhusu maeneo waliyokubalina kupanda na kustawisha miti, na kuhifadhi misitu iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuikijanisha Dodoma. 

........................................................................
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zimesaini hati ya makubaliano (MOU) ya upandaji, ustawishaji, na utunzaji wa miti na uhifadhi wa misitu iliyopo katika Jiji hilo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Dodoma ya Kijani iliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais  Mhe. Samia Saluhu Hassan kwa kupanda miti kwenye eneo la Mzakwe mwishoni mwa mwaka jana.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ambayo ni ya kwanza kufanywa na TFS Nchini ilifanyika jana katika Ofisi za Jiji, ambapo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi na Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Dos Santos Silayo walisaini makubaliano hayo ambayo utekelezaji wake unaanza katika mwaka huu wa fedha.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali, Mkurugenzi Kunambi alisema Jiji linawakabidhi TFS hekta 150 za msitu katika eneo la Mahomanyika ili kustawisha miti na kulihudumia.
“Lakini pia kwa makubaliano haya, TFS watahifadhi maeneo yote ya vilima vilivyopo ndani ya Jiji la Dodoma na kustawisha misitu midogo katika maeneo ya makazi yaliyotengwa kwa ajili hiyo” alisema Kunambi.
Alisema hizi ni juhudi za kutekeleza kampeni ya Dodoma ya Kijani ambayo ina lengo la kulifanya Jiji la Dodoma na Mkoa mzima kustawisha miti ya kutosha ili kuhifadhi mazingira yatakayokuwa rafiki zaidi kwa maisha ya binadamu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Silayo alisema kuwa tayari taasisi yake imetenga Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mpango huo alioutaja kuwa wa Kihistoria kwani haujawahi kufanyika katika Halmashauri yeyote Nchini, na kwamba utalipa hadhi kubwa Jiji la Dodoma kwenye Jumuiya ya Kimataifa.
“Makubaliano haya yataliweka Jiji la Dodoma katika ramani ya dunia katika kwenda na mahitaji ya maendeleo endelevu ya dunia kupitia mpango uendelevu wa Miji, lazima tujipange kukabiliana na ongezeko la watu na ukuaji wa Miji, Mpango huu utalifanya Jiji hili kwenda sambamba na kuweka uwiano sawia wa kiikolojia.” Alisema Profesa Silayo.
Makubaliano hayo yamesainiwa ikiwa ni takribani wiki mbili baada ya Jiji la Dodoma kuingia makubaliano na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) ya utunzaji wa mizunguko mitatu mikubwa ya barabara iliyopo Jijini humo, ambapo Mamlaka hiyo itahudumia bustani za maua na kuweka sanamu za Wanyama ikiwemo ya Tembo ili kupendezesha Mji na kutangaza vivutio vya kitalii vilivyopo Nchini.  


Monday, June 25, 2018

MATIBABU YA KIBINGWA HOSPITALI TEMBEZI YAANZA LEO JUNI 25 JIJINI DODOMA

.................................................................
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeanza rasmi zoezi la siku 5 la kutoa huduma ya matatibu kwa wagonjwa mbalimbali kwa mfumo wa Hospitali Tembezi linalofanyika katika Hospitali Teule ya Wilaya Mtakatifu Gemma iliyopo Kata ya Miyuji Jijini humo.
Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Hamad Nyembea amesema huduma ya Hospitali Tembezi ni jukwaa linalowakutanisha madaktari Bingwa wa fani mbalimbali za utabibu kama mgonjwa ya akina mama na watoto, Figo, Moyo, Koo na Pua, Kinywa na Meno, Shinikizo la Damu, Sukari, Tezi Dume, Shingo ya Kizazi, Macho, Masikio, pamoja na upasuaji wa mifupa na wa kawaida.
Ametoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na Wilaya za jirani hususan wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali kutumia fursa hiyo vizuri.
"Kuna wagonjwa wengine ambao wameandikiwa rufaa kwenda Hospitali za mbali kama Muhimbili Dare es Salaam na hawana uwezo, hii ni fursa kwao kwani hapa kuna madaktari Bingwa wa fani zote na watahudumia kwa muda wa siku tano kuanzia leo, mpaka Ijumaa Juni 29.
Alifafanua kuwa utaratibu wa matibabu ni wa kawaida ambapo wagonjwa wenye Bima za Afya za NHIF na CHF watatibiwa kwa kutumia kadi zao na wale wasio na Bima watachangia Shilingi elfu 5 kama gharama ya kuonana na Daktari, na kwa huduma ya upasuaji mgonjwa atachangia Shilingi elfu 30 tu.

Thursday, June 21, 2018

JIJI ‘LAMWAGA’ MAMILIONI KWA VIJANA, WANAWAKEKaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Dodoma Mufungo Manyama akizungumza na viongozi wa vikundi 137 vya Wanawake na Vijana wakati wa semina elekezi kwa viongozi hao kuhusu uendeshaji wa vikundi na matumizi ya fedha za mikopo kabla ya kupatiwa mkopo wa milioni 344 mapema wiki ijayo.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Dodoma Mufungo Manyama akizungumza na viongozi wa vikundi 137 vya Wanawake na Vijana wakati wa semina elekezi kwa viongozi hao kuhusu uendeshaji wa vikundi na matumizi ya fedha za mikopo kabla ya kupatiwa mkopo wa milioni 344 mapema wiki ijayo.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Dodoma Mufungo Manyama akizungumza na viongozi wa vikundi 137 vya Wanawake na Vijana wakati wa semina elekezi kwa viongozi hao kuhusu uendeshaji wa vikundi na matumizi ya fedha za mikopo kabla ya kupatiwa mkopo wa milioni 344 mapema wiki ijayo.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Dodoma Mufungo Manyama akizungumza na viongozi wa vikundi 137 vya Wanawake na Vijana wakati wa semina elekezi kwa viongozi hao kuhusu uendeshaji wa vikundi na matumizi ya fedha za mikopo kabla ya kupatiwa mkopo wa milioni 344 mapema wiki ijayo.


.....................................................
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatarajia kutoa takribani shilingi milioni 500 kwa ajili ya kukopesha vikundi vya Wajasiriamali Wanawake na Vijana kwa mwaka wa fedha unaomalizika Mwezi Juni, 2018.

Jumla ya vikundi 137 vinatarajiwa kunufaika na fedha hizo zinazotokana na makusanyo ya kodi za ndani ya Halmashauri (Own Source) ambapo  vikundi vya Wanawake ni 102 na vya vijana 37.

Akizungumza wakati akitoa semina elekezi kwa viongozi wa vikundi hivyo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma leo Juni 21, 2018, Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Dodoma Mufungo Manyama aliwaeleza wajumbe kuwa awamu ya mwisho ya mikopo kwa mwaka huu wa fedha itatolewa katikati ya wiki ijayo ambapo jumla ya Shilingi milioni 344 zitakabidhiwa kwa vikundi hivyo.

Aliwataka Wanavikundi hao kuwa makini na matumizi ya fedha wanazokopeshwa na kufanya marejesho kwa wakati ili wapate fursa ya kukopeshwa zaidi.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa vikundi hivyo waliishukuru Halmshauri ya Jiji na kuahidi kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili waweze kurejesha kwa wakati hali itakayopelekea kunufaisha vikundi vingi zaidi.Tuesday, June 5, 2018

WAKAZI DODOMA WAASWA KUKIJANISHA JIJI


Wadau mbalimbali katika Maandamano kuelekea Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 5, 2018.
Afisa Mazingira kutoka Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Takangumu Jiji la Dodoma Ally Mfinanga akitoa neno la utangulizi kwa Mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Naibu Meya wa Jiji hilo Jumanne Ngede (hayupo pichani) na wadau wengine katika Viwanja vya Nyerere Square leo Juni 5, 2018.

Mgeni Rasmi Naibu Meya Jumanne Ngede (wa pili kulia) akikagua mabanda ya wadau wa Mazingira

Mgeni Rasmi Naibu Meya Jumanne Ngede (wa pili kushoto) akikagua mabanda ya wadau wa Mazingira

....................................................................


NAIBU Meya wa Halmshauri ya Jiji la Dodoma Jumanne Ngede ametoa wito kwa kila mkazi wa Jiji hilo kuhakikisha anatunza Mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yanayomzunguka ili kuunga mkono juhudu za Serikali na wadau kuhakikisha Jiji linakuwa la kijani kwa manufaa ya viumbe vyote.
Alitoa wito huo mapema leo asubuhi alipotembelea na kukagua mabanda ya wadau mbalimbali wa Mazingira walioshiriki kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo katikati ya Jiji la Dodoma leo Juni 5, 2018.   

Mhe. Ngede aliwapongeza wadu mbalimbali hususan wanaojihusisha na nishati mbadala kama Gesi na Sola ambazo matumizi yake yanasaidia kupunguza  ukataji wa miti na uharibufu wa misitu kwa ajili ya kuchoma mkaa unaotumika kwa kazi za jikoni.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira kutoka Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Takangumu Jiji la Dodoma Ally Mfinanga alisema Halmashauri imekuwa ikishikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila kundi katika jamii linawajibika katika kutunza Mazingira.

“Kuna wadau ambao tunashirikiana nao katika kutunza Mazingira kwa maana ya kupanda miti na kutunza misitu lakini pia, kama Halmashauri tunajukumu la kusafisha Mazingira kwa kuondosha taka zinazozalishwa Mjini…haya yote tunayatekeleza kwa kuwashirikisha pia wadau kama TFS na vikundi mbalimbali, vikiwemo vya kuzoa taka” alisema Mfinanga.

Kilele cha siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa Juni 5 kila Mwaka na huambatana na jumbe mbalimbali kama sehemu ya kueleimisha Jamii, ambapo kaulimbiu ya Mwaka huu inasema “Mkaa ni gharama, tumia nishati mbadala”.


Wednesday, May 30, 2018

JIJI LA DODOMA VINARA UMISETA


Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Mwalimu Abdallah Membe akionesha kikombe cha ubingwa wa Michezo ya UMISETA Kimkoa iliyofanyika kwa siku tatu katika Viwanja vya Sekondari ya Dodoma kuanzia Mei 26 mwaka huu. 
Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Mwalimu Abdallah Membe akipokea kikombe cha ubingwa wa Michezo ya UMISETA Kimkoa iliyofanyika kwa siku tatu katika Viwanja vya Sekondari ya Dodoma kuanzia Mei 26 mwaka huu. 
Washiriki wakiwa wameketi kando ya vikombe vilivyotolewa kwa washindi


..................................................

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeibuka mshindi wa jumla baada ya kushinda michezo mingi katika michezo ya Shule za Sekondari (UMISETA) iliyofanyika kwa siku tatu kuanzi Mei 26, 2018 na kushirikisha zaidi ya Wanamichezo 700 kutoka katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma, huku Wilaya ya Kongwa ikishika nafasi ya pili na Mpwapwa nafasi ya tatu.

Timu ya Wanamichezo wa Jiji la Dodoma iliibuka bingwa wa Mkoa baada ya kushinda michezo ya Mpira wa Mikoni kwa Wavulana, Mpira wa Pete, Mpira wa Miguu kwa Wasichana, Kikapu kwa Wavulana na Wasichana, kurusha tufe, kurusha kisahani,
na riadha kwa mita 200.

Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Mwalimu Abdallah Membe amesema amefurahishwa na ushindi walioupata na kwamba wao kama Jiji walijipanga vizuri, huku akiwapongeza wote waliofanikisha mafanikio hayo wakiwemo Wanafunzi, Walimu, na wadau wengine wote.

Amesema baada ya hatua hiyo kufikia tamati, timu ya Mkoa ya Michezo hiyo itasafiri Jumapili wiki hii kuelekea Jijini Mwanza kushiriki michezo hiyo kwa ngazi ya Taifa inayotarajiwa kuanza Jumatatu Mei 4 mwaka huu Jijini humo.


Saturday, May 26, 2018

WAZIRI JAFFO: JIJI LA DODOMA NI MFANO NCHINI KUWATAMBUA WAZEE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali (TAMISEMI) Selemani Jaffo akimkabidhi kitambulisho rasmi cha kumtambua mmoja ya Wazee wa Kata ya Mkonze Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakati Waziri huyo alipozindua zoezi hilo mapema leo Mei 26, 2018. Wanaoshudia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi (kulia kwa Waziri) na Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi (mwenye shati jeupe). Kushoto kwa Waziri aliyevaa miwani ni Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Hamadi Nyembea.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali (TAMISEMI) Selemani Jaffo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na badhi ya Waze wa Kata ya Mkonze Jijini Dodoma baada ya kuzindua na kuwakabidhi vitambulisho rasmi vya kuwatambua  Wazee katika Halmashauri ya Jiji hilo mapema leo Mei 26, 2018. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi na kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi (mwenye shati jeupe). 
Baadhi ya Wazee wa Kata ya Mkonze Jijini Dodoma wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa utaoji wa vitambulisho vya Wazee uliofanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Selemani Jaffo leo Mei 26, 2018.
Diwani wa Kata ya Mkonze Jiji la Dodoma David Bochela akitoa neno wakati wa hafla ya uzinduzi wa utaoji wa vitambulisho vya Wazee uliofanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Selemani Jaffo leo Mei 26, 2018 katika Kata hiyo.

...........................................................................


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo amesema, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni ya mfano Nchini katika kuwatambua na kuwatengenezea vitambulisho maalum vya kuwatambulisha Wazee katika maeneo ya huduma mbalimbali ikwemo matibabu, akiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 inayolenga katika  kuhakikisha kuwa, Wazee wa Tanzania wanatambuliwa na wanapewa fursa ya kushiriki katika mambo yanayohusu maisha ya kila siku na kupata huduma zote za msingi.

Waziri Jaffo ameyasema hayo mapema leo Mei 26, 2018, alipokuwa akizindua rasmi zoezi la utoaji wa vitambulisho vya Wazee kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Kata ya Mkonze iliyopo umbali wa kilometa 4.7 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma.

Akizungumza wakati wa  hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi na Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi, Waziri huyo aliagiza Halmashauri za Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara  kuhakikisha zinawatambua Wazee katika maeneo yao na kuwasilisha taarifa kamili ya kila Mkoa kuhusu Wazee katika  Ofisi yake ifikapo Juni 30, mwka huu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekeleaji wa zoezi hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, Mganga Mkuu wa Jiji hilo Hamadi Nyembea alisema Halmashauri ilianza zoezi hilo kwa kuwatambua Wazee katika Kata zote 41 za Jiji la Dodoma, na kwamba mpaka sasa jumla ya Wazee 15, 854 wameshatambuliwa kutoka katika Kata 33, sawa na asilimia 80.5.

Alisema, hatua iliyofuata ni kuwapiga picha Wazee waliotambuliwa na kuwatengenezea vitambulisho, zoezi lililoanza rasmi mwezi Februari Mwaka huu, ambapo jumla ya Wazee 1,118 wameshapigwa picha katika Kata za Mkonze, Mnadani, Uhuru, Madukani, Makole na Majengo na kwamba kazi hiyo inaendelea katika Kata zilizobaki.

“Jumla ya vitambulisho 564 vya Wazee vimeshakamilika na wahusika watakabidhiwa rasmi leo kwa ajili ya kuanza kuvitumia” alisema Mganga Mkuu huyo wakati akiwasilisha taarifa hiyo.