.................................................................
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeanza rasmi zoezi la siku 5 la kutoa huduma ya matatibu kwa wagonjwa mbalimbali kwa mfumo wa Hospitali Tembezi linalofanyika katika Hospitali Teule ya Wilaya Mtakatifu Gemma iliyopo Kata ya Miyuji Jijini humo.
Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Hamad Nyembea amesema huduma ya Hospitali Tembezi ni jukwaa linalowakutanisha madaktari Bingwa wa fani mbalimbali za utabibu kama mgonjwa ya akina mama na watoto, Figo, Moyo, Koo na Pua, Kinywa na Meno, Shinikizo la Damu, Sukari, Tezi Dume, Shingo ya Kizazi, Macho, Masikio, pamoja na upasuaji wa mifupa na wa kawaida.
Ametoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na Wilaya za jirani hususan wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali kutumia fursa hiyo vizuri.
"Kuna wagonjwa wengine ambao wameandikiwa rufaa kwenda Hospitali za mbali kama Muhimbili Dare es Salaam na hawana uwezo, hii ni fursa kwao kwani hapa kuna madaktari Bingwa wa fani zote na watahudumia kwa muda wa siku tano kuanzia leo, mpaka Ijumaa Juni 29.
Alifafanua kuwa utaratibu wa matibabu ni wa kawaida ambapo wagonjwa wenye Bima za Afya za NHIF na CHF watatibiwa kwa kutumia kadi zao na wale wasio na Bima watachangia Shilingi elfu 5 kama gharama ya kuonana na Daktari, na kwa huduma ya upasuaji mgonjwa atachangia Shilingi elfu 30 tu.