Friday, October 27, 2017

WANANCHI MANISPAA YA DODOMA WATAKIWA KUHUDHURIA MIKUTANO YA MANISPAA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) akizungumza wakati wa Mkutano wa awali wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo Oktoba 25 mwaka huu. Katika ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo Jumanne Ngede na kulia ni Afisa wa Serikali za Mitaa Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Emmanuel Kuboja.   (PICHA-OFISI YA MKURUGENZI)

..............................................

WAKAZI wa Manispaa ya Dodoma wameshauriwa kuhudhuria mikutano ya Baraza la Madiwani ili kupata taarifa za miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Manispaa yao na kujua kazi inayofanywa na Madiwani waliowachagua.

Wito huo umetolewa na Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede kuelekea Mkutano wa Baraza hilo wa kisheria kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/18  utakaopokea taarifa mbalimbali za Manispaa hiyo kitakachonyika Oktoba 31 mwaka huu katika ukumbi wa Manispaa.

Naibu Meya Ngede alitoa wito huo wakati alipoongoza Mkutano wa awali wa Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo lililopokea taarifa za utekelezaji wa miradi kutoka katika Kata zote 41 za Manispaa ya Dodoma Oktoba 25 mwaka huu.

Aliiagiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuongeza matangazo kwa wananchi kuhusu tarehe ya Mkutano huo ili waweze kuhudhuria kutokana na umuhimu wa mkutano huo ambao ni wa wazi.

Tuesday, October 24, 2017

WAKUU WA IDARA MANISPAA YA DODOMA WAINGIA MTAANI KUSAKA KODI

Kiongozi wa kikosi kazi cha Wakuu wa Idara Dickson Kimaro (wa pili kushoto ) akimuhoji mmoja wa Wafanyabiashara wa Eneo la 'Mambo Poa' wakati wa zoezi la uhakiki wa nyaraka mbalimbali za biashara.

Mmoja wa wafayabiashara ya chakula maarufu Mama Lishe (kulia) akilipa kodi kwa Maafisa wa Manispaa ya Dodoma wakati wa zoezi la kuhakiki nyaraka za kisheria za kuendesha biashara.


Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mganula Mbogoni akiweka utepe ikiwa ni ishara ya kulifunga moja ya duka ambalo mmiliki wake hakukidhi masharti ya kisheria ya kufanya biashara ikiwas ni pamoja na kutokuwa na Mkataba hai wa Pango na Leseni ya Biashara.

............................................

MENEJIMENTI ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeanza zoezi la uhakiki wa nyaraka mbalimbali kwa wafanyabiashara waliopanga vibanda vya biashara vinavyomilikiwa na Manispaa hiyo, ambapo wakuu wa Idara wanatekeleza zoezi hilo kwa kupita katika vibanda vyote vilivyopangishwa kwa wafanyabiashara.

Nyaraka zinazohakikiwa ni mikataba ya upangishaji wa chumba cha biashara na leseni za biashara husika, ambapo maeneo mengine kama viwanda vya matofali, maeneo ya kuoshea magari, na maeneo ya kuchomelea vyuma pia yatahusishwa katika uhakiki huo ili kujiridhisha endapo biashara hizo zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria na taratibu kama inavyopaswa.


Zoezi hilo la siku tatu limeanza vizuri ambapo baadhi ya Wafanyabiashara ambao mikataba yao ya upangishaji ilimalizika wameonesha ushirikiano kwa kulipia huku wengine wakifungiwa maduka kwa kushindwa kufanya hivo.