Friday, April 28, 2017

HALMASHAURI ZAKARIBISHWA KUWEKEZA DODOMA




Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (wa pili kulia) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo wakiwa katika ziara ya Mafunzo katika Dampo la Kisasa linalotumia  teknolojia  ya kuzika taka ngumu (Landa Fill) katika  Manispaa ya Dodoma jana Aprili 27, 2017. Wa kwanza kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede.
Meneja wa Dampo la Kisasa linalotumia  teknolojia  ya kuzika taka ngumu (Landa Fill) katika  Manispaa ya Dodoma John Chiwanga ( kushoto ) akitoa maelezo kwa Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (wa pili kulia) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo walipokuwa katika ziara ya Mafunzo  jana Aprili 27, 2017. Wa kwanza kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede.

Mkuu wa Idara ya Usafi na Takangumu  Dickson Kimaro (aliyesimama) akitoa taarifa ya hali ya Usafi katika Manispaa ya Dodoma kwa Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (hayupo pichani) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo walipokuwa katika ziara ya Mafunzo  jana Aprili 27, 2017. Waliokaa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni Rahel Muhando na Naibu Meya wa Manispaa hiyo Amini Sambo.

Mhandisi wa Mazingira wa Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida (kulia) akitoa maelekezo kwa  Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (katikati) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo walipokuwa katika ziara ya Mafunzo  jana Aprili 27, 2017, ya jinsi mashine za kupimia uzito wa taka ngunu inavyofanya kazi katika mzani uliopo kwenye Dampo la Kisasa linalotumia  teknolojia  ya kuzika taka ngumu (Landa Fill) katika  Manispaa ya Dodoma. PICHA ZOTE: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI 


MKURUGENZI wa  Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ametoa wito kwa Halmshauri nchini kuwekeza katika Manispaa ya Dodoma kama njia mojawapo ya kujiongezea mapato ya ndani.

Ametoa wito huo jana wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya mafunzo ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa ya Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam waliyoifanya katika Manispaa ya Dodoma.

Kunambi aliwaeleza wageni  hao kuwa, Manispaa ya Dodoma ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli za kisasa, majengo ya Ofisi, na miundombinu mingine ikizingatiwa kuwa kuna rasilimali ardhi ya kutosha na sasa ni Makao Makuu ya Nchi.

Msafara wa watu 20 wakiwemo Madiwani na Wataalam kutoka Manispaa ya Kigamboni  ukiongozwa na Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki  Maabad Hoja  walifanya ziara ya mafunzo juu ya usafi wa Mazingira na uhifadhi wa taka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuzika taka ardhini (Land Filling) ambapo Manispaa ya Dodoma inafanya vizuri kupitia Dampo lililopo katika Kata ya Ntyuka katika Manispaa hiyo.


Pia ziara yao ililenga kulijifunza kuhusu suala la utozaji na ukusanyaji wa kodi mbalimbali unaofanywa na Manispaa.

Friday, April 7, 2017

BANKI YA DUNIA YAKAGUA MIRADI MANISPAA YA DODOMA




 Mhandisi wa Mazingira Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida (katikati) akifafanua jambo wakati wa ziara ya ukaguzi wa Dampo la kisasa la kuhifadhi taka ngumu iliyofanywa na maafisa kutoka  Benki ya Dunia jana Aprili 6, 2017.


Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia  (katikati) akishudia kazi ya kumwaga na kuhifadhi taka ngumu katika Dampo la kisasa lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma wakati yeye na ujumbe wake walipofanya ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo jana April 6.  Wa pili Kulia  (mwenye suti) ni Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Lusako Kilembe na wa pili kushoto ni Mhandisi wa Mazingira Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida. 

Kazi ya umwagaji na uhifadhi wa taka ngumu ikiendelea katika Dampo la Chidaya


Kazi ya umwagaji na uhifadhi wa taka ngumu ikiendelea katika Dampo la Chidaya.


Barabara ya 'Independence Square' ni miongoni miradi ya barabara za mji wa Dodoma iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya Dunia


TIMU ya maafisa kutoka Benki ya Dunia wamefanya ziara ya kukagua mradi  wa dampo la kisasa na Barabara zinazofadhiliwa na Benki hiyo katika Manispaa ya Dodoma chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Miji Tanzania (TSCP).

Ziara hiyo ilifanyika jana April 6, 2017 ambapo timu hiyo ilitembelea eneo la Chidaya unakotekelezwa mradi wa dampo la kisasa linalotumia teknolojia ya kuzika taka (Land Fill) na kufurahishwa na maendeleo ya mradi ambao umeashaanza kufanya kazi huku ujenzi ukiwa katika hatua za mwisho.

Aidha ujumbe huo ulitembelea barabara zilizojengwa chini ya mradi huo unaotekelezwa katika Manispaa Saba Tanzania Bara pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).



Awali ujumbe huo ulikutana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi na kufanya nae mazungumzo mafupi, ambapo aliishukuru Benki ya Dunia kwa kusaidia kuboresha miundombinu katika Manispaa ya Dodoma huku akiiomba kuendelea kutoa ufadhili zaidi ili kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa kisasa zaidi hivyo kuendana na hadhi yake ya kuwa makao makuu ya Nchi.



Monday, April 3, 2017

MEYA WA MANISPAA YA DODOMA AVULIWA MADARAKA

                                                                           

 Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa mkutano maalum cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo jana Aprili 3 ambapo uamuzi wa kumvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo ulifikiwa. Kulia ni Mbunge wa dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi Ajira na Vijana Mh. Anthony Mavunde na wa pili Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Christina Mndeme. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.

Wajumbe wakifuatilia mkutano



BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Dodoma limemvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba kwa tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi yaliyopelekea upotevu wa shilingi milioni 30 za mradi wa Maji wa Kata ya Zuzu zilizotolewa na Serikali ya Japan kupitia ubalozi wake nchini Tanzania.

Hatua hiyo ilifikiwa katika mkutano wa dharura wa Bazara hilo ulioitishwa jana Aprili tatu katika ukumbi wa Manispaa ili  kupokea na kujadili taarifa ya Tume Maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana kuchunguza tuhuma hizo.

Baada ya Katibu wa mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi kuwasilisha taarifa hiyo, wajumbe waliazimia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya huyo, ambapo kati ya kura 48 zilizopigwa, kura 43 ziliunga mkono hoja hiyo huku kura 4 zikipinga na moja ikiharibika.


Kufuatia hali hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede atakaimu nafasi ya Meya kwa mujibu wa Kanuni katika kipindi cha mpito kisichozidi siku 60, ambapo uchaguzi wa kumpata Meya mpya utafanywa.