Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa mkutano maalum cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo jana Aprili 3 ambapo uamuzi wa kumvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo ulifikiwa. Kulia ni Mbunge wa dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi Ajira na Vijana Mh. Anthony Mavunde na wa pili Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Christina Mndeme. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.
Wajumbe wakifuatilia mkutano
BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Dodoma limemvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba kwa tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi yaliyopelekea upotevu wa shilingi milioni 30 za mradi wa Maji wa Kata ya Zuzu zilizotolewa na Serikali ya Japan kupitia ubalozi wake nchini Tanzania.
Hatua hiyo ilifikiwa katika mkutano wa dharura wa Bazara hilo
ulioitishwa jana Aprili tatu katika ukumbi wa Manispaa ili kupokea na kujadili taarifa ya Tume Maalum
iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana kuchunguza tuhuma hizo.
Baada ya Katibu wa mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi kuwasilisha taarifa hiyo, wajumbe waliazimia
kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya huyo, ambapo kati ya kura 48
zilizopigwa, kura 43 ziliunga mkono hoja hiyo huku kura 4 zikipinga na moja ikiharibika.
Kufuatia hali hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne
Ngede atakaimu nafasi ya Meya kwa mujibu wa Kanuni katika kipindi cha mpito
kisichozidi siku 60, ambapo uchaguzi wa kumpata Meya mpya utafanywa.
No comments:
Post a Comment