Operesheni za kuhifadhi takataka zikiendelea katika Dampo la kisasa la Chidaya Jijini Dodoma. |
Muonekano wa sehemu ya Dampo la kisasa la Chidaya Jijini Dodoma ambayo bado haijaanza kutumika.
................................................................
|
MADIWANI
wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wameingia kwenye historia ya kuwa wageni wa
kwanza kufanya ziara ya kubadilishana uzoefu katika Halmashauri ya Jiji jipya
la Dodoma mara baada ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kupandishwa hadhi na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli wakati wa Sherehe za
miaka 54 ya Muungano Aprili 26, mwaka huu zilizofanyika katika uwanja ya
Jamhuri Jijini humo.
Madiwani
hao wa jiji la Mwanza wakiongozwa na Naibu Meya Mhe. Bhiku Kotecha ambaye ni
Diwani wa Kata ya Nyamagana, walitembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana
Aprili 27, 2018 ikiwa ni siku moja tangu iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kupewa
hadhi ya Jiji.
Lengo
la ziara hiyo ilikuwa ni kubadilishana uzoefu hususan katika suala la Usafi wa
Mazingira, ambapo walitembelea Dampo la kisasa la kuhifadhia takataka kwa njia
ya kuzifukia (Sanitary Land Fill) lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu
nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Wakiwa
katika eneo la Dampo, walipata maelezo ya kina juu ya mradi huo kutoka kwa Mhandisi
wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida, ambaye aliwaeleza kuwa, mradi
huo umetekelezwa kwa awamu kuanzia mwaka 2011 kwa Fedha za Serikali Kuu ikiwa
ni mkopo wa Benki ya Duniani kupitia mradi wa kuimarisha Majiji ya Kimkakati (TSCP)
na kwamba hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 7.1, huku
ukiwa tayari umeanza kufanya kazi.