Wednesday, April 4, 2018

MILIONI 993 ZA ‘P4R’ ZAIMARISHA ELIMU YA MSINGI

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imeishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kuipatia fedha kwa ajili ya kuimarisha Miundombinu ya Shule mbalimbali za Manispaa hiyo chini ya mradi wa ‘Lipa kwa Matokeo’ maarufu kama ‘P4R’.

Shukrani hizo zimetolewa na Afisa Elimu ya Msingi wa Manispaa ya Dodoma Mwisungi Kigosi alipotembelea Shule mbili za Nkuhungu na Chango’mbe ambazo kila moja inajengewa madarasa mapya nane kwa fedha za mradi huo.

Kwa mujibu wa Kigosi, mradi huo pamoja na mambo mengine, unajenga miundombinu mbalimbali katika Shule sita za Msingi ambapo jumla ya Shilingi milioni 993.1 zinatekeleza kazi hizo.

“Fedha za P4R zina kazi nyingi kama vile kusaidia kukusanya takwimu mbalimbali, kuhamisha Walimu kwa mujibu wa Ikama, na kubwa kabisa ni kujenga miundombinu kama madarasa mapya, kukarabati madarasa ya zamani, na kujenga Vyoo” Alifafanua.

Alisema mradi huo umekuwa mkombozi kwa Shule husika kwa kuongeza na kuimarisha miundombinu kama madarasa kutokana na idadi kubwa ya Wanafunzi inayopelekea upungufu wa madarasa katika baadhi ya Shule.

“Kwa mfano Shule ya Msingi Nkuhungu, mwaka huu wanafunzi walioandikishwa kuanza darasa la kwanza ni mia sita…kwa hiyo utaona ni jinsi gani madarasa yanahitajika na hii inatokana na Kata hiyo kuwa na Shule  moja tu ya Serikali” alisema Kigosi.

Aidha, alizitaja Shule nyingine nne ambako mradi huo unatekelezwa kuwa ni Mahomanyika, Mwenge, Ihumwa, na Nzasa, na kwamba Fedha hizo zimepatikana baada ya Manispaa kukidhi vigezo ikiwemo kuwa na takwimu za uhakika za masuala ya Elimu.

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule zilizopata Fedha za mradi huo wamepongeza juhudi za Serikali katika kuwatatulia chang’amoto hususani za miundombinu kama vyumba vya Madarasa na Vyoo.

Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mwisungi Kigosi akizungumza na Dada Mkuu wa Shule ya Msingi Nkuhungu Zena Yusuph alipotembelea Shule hiyo jana kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Miundombinu ikiwemo Vyumba vya Madarasa kupitia mradi wa 'P4R'. Wanafunzi wa Darasa la Saba na la nne katika Shule hiyo wanaendelea na masomo ili kujiimarisha zaidi kuelekea mitihani ya Kitaifa mwishoni mwa Mwaka huu.
Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mwisungi Kigosi (kulia) akikagua Maendeleo ya Ujenzi wa Madarsa nane alipotembelea Shule ya Msingi Nkuhungu  jana kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Miundombinu ikiwemo Vyumba vya Madarasa kupitia mradi wa 'P4R'. Kushoto ni Msimamizi wa Ujenzi kutoka Suma JKT Joseph Luya.
Moja ya jengo lenye Vyumba vya Madarasa yaliyojengwa kupitia mradi wa P4R katika Shule ya Msingi Chang'ombe. Jumla ya Vyumba vipya nane vya Madarasa vimejengwa katika Shule hiyo.
Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mwisungi Kigosi akizungumza na baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nkuhungu alipotembelea Shule hiyo jana kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Miundombinu ikiwemo Vyumba vya Madarasa kupitia mradi wa 'P4R'. Wanafunzi wa Darasa la Saba na la nne katika Shule hiyo wanaendelea na masomo ili kujiimarisha zaidi kuelekea mitihani ya Kitaifa mwishoni mwa Mwaka huu.
Moja ya jengo lenye Vyumba vya Madarasa yaliyojengwa kupitia mradi wa P4R katika Shule ya Msingi Nkhungu. Jumla ya Vyumba vipya nane vya Madarasa na matundu matano ya Vyoo vimejengwa katika Shule hiyo.

No comments:

Post a Comment