........................................
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt.
Binilith Mahenge ameelekeza matumizi ya kilichokuwa kituo Kikuu cha Mabasi
madogo maarufu kama Daladala cha Jamatini Mjini Dodoma kwa ajili ya kupakia na
kushusha abiria wanaotoka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo yaendelee
kama kawaida wakati Manispaa ikiandaa eneo mbadala.
Mkuu huyo wa Mkoa pia
ameagiza ‘ruti’ za Daladala zifupishwe kama ilivyokuwa awali, na kwamba
upangaji wa ‘ruti’ ndefu ujadiliwe upya na wadau wote wanaohusika na endapo
utakubaliwa na wengi ndipo utekelezaji wake uanze.
Dokta Mahenge ametoa
maelekezo hayo leo Aprili 3, 2018, alipokuwa akizungumza na wadau wa
usafirishaji katika kituo kikuu cha mabasi ya Mikoani cha muda kilichopo
Nanenane Manispaa ya Dodoma baada ya kituo hicho kufungwa wiki iliyopita kwa
ajili ya kupisha mradi wa Reli ya Kisasa.
Hatua hiyo imefikiwa baada
ya majadiliano na wadau wote ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu
na Majini (SUMTRA), Manispaa, Jeshi la Polisi, na Shirika la Reli ambao ndio
wamiliki wa eneo hilo, na kwamba matumizi ya stendi hiyo yataendelea kwa muda
wa miezi miwili kuanzia sasa, kipindi ambacho Manispaa itatakiwa kuwa
imeshapata na kuandaa stendi mbadala.
Akizungumza katika eneo la
tukio, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alisema
Manispaa imepokea maagizo yote na itahakikisha inaandaa eneo kwa ajili ya
Stendi ya Mabasi madogo Mjini katika kipindi cha miezi miwili kama
ilivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa.
Katika hatua nyingine, Mkuu
huyo wa Mkoa ameagiza mabasi yote yanayosafirisha abiria Mikoa mbalimbali
Nchini kupakia na kuanzia safari zao katika kituo Kikuu cha mabasi ya muda
kilichopo Nanenane na Kampuni itakayokiuka itachukuliwa hatua kali za Kisheria.
“Namuagiza Mkuu wa Jeshi la
Polisi kikosi cha Usalama Barabarani wa Mkoa kuwa, kuanzia kesho mabasi yote
yauze tiketi na kuanza safari zao hapa katika kituo hiki Kikuu cha mabasi cha
muda cha Nanenane…hakuna Mkubwa wala mdogo katika kutoa huduma kwa Wananchi”
alisisitiza Dkt. Mahenge.
No comments:
Post a Comment