.........................................................
HALMASHAURI ya Manispaa ya
Dodoma imekamilisha uandaaji wa hati 912 za umiliki wa ardhi za miaka 99 kama
ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli Mei
15 mwaka huu wakati akitoa tamko la kuivunja iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu Dodoma (CDA) na shughuli zote kuhamishiwa katika Manispaa ya
Dodoma.
Akizungumza katika kikao
cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichopokea taarifa
rasmi ya makabidhiano ya majukumu ya iliyokuwa CDA kuhamia Manispaa ya Dodoma
jana, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi aliwaambia Madiwani na wananchi
kwa ujumla waliohudhuria Baraza hilo kuwa, hatua hiyo imefikiwa katika kipindi
cha miezi miwili ya Julai na Agosti, huku akiahidi kuwa,Manispaa hiyo itaendelea kutoa huduma hiyo
na nyingine kwa kasi inayoendana na matarajio ya wananchi.
Alisema kati ya hati hizo,
hati 674 zilizowasilishwa kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi zimeshasajiliwa
na zipo tayari kwa ajili ya kukabidhiwa kwa wananchi husika, huku hati 238
zikiwa katika hatua ya kukaguliwa ili zisainiwe.
Alifafaua zaidi kuwa,
uandaaji huo wa hati unaenda sambamba na utoaji wa vibali vya ujenzi kwa
haraka, ambapo mchakato wa kutoa kibali cha ujenzi unakamilishwa ndani ya siku
saba tu baada ya maombi kupokelewa mpaka muombaji anakabidhiwa kibali chake.
Kufuatia taarifa hiyo, wajumbe
wa Baraza la Madiwani wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki
Profesa Davis Mwamfupe wameipongeza Menejimenti ya Halmashauri na watumishi
wote na kuwataka waendelee na juhudi hizo ili pamoja na mambo mengine kuufanya
mji wa Dodoma ukue kwa kasi kwa kuwawezesha wananchi na wadau wengine kujenga.