Tuesday, December 6, 2016

LAPF 'YAIPIGA TAFU' MANISPAA YA DODOMA



Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi





















MFUKO wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF) umekabidhi hundi ya Sh. 6 milioni kwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kutatua tatizo la uhaba wa maji katika maeneo ya Ihumwa na Mtumba ndani ya Manispaa hiyo.
Akikabidhi  hundi hiyo kwa Godwin Kunambi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma mjini humo, James Mlowe ambaye ni Meneja Mawasiliano na Masoko wa LAPF amesema, mfuko huo umetoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kufufua visima vya maji vilivyoharibika.

Amesema mfuko huo ulipokea maombi kutoka katika Ofisi ya Manispaa pamoja na ofisi ya mbunge
kupatiwa msaada wa kutengeneza visima vya maji katika Kata ya Ihumwa na Mtumba kutokana na visima hivyo kuharibika na kuwasababishia usumbufu wa kukosea maji wakazi hao.
Amesema LAPF kama taasisi ya serikali, imekuwa ikifanya shughuli nyingi na halmashauri mbalimbali nchini hususani shughuli za maendeleo.

“Kwa sasa Dodoma ni Makao Mkuu ya Nchi hivyo kuna watu wengi watahamia hivyo hakuna sababu ya kuwepo ukosefu wa maji.

“Kadri watu wanavyoongezeka ndivyo mahitaji yanavyoongezeka hivyo mahitaji ya maji ni makubwa zaidi katika Mji wa Dodoma na Ihumwa na Mtumba ni sehemu mahitaji hayo,” amesema Mlowe.

Hata hivyo Mlowe amesema, pesa zinazotolewa na taasisi mbalimbali pamoja na wahisani ni vyema zikatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuzibadilishia matumizi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi  wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema katika uongozi wake, atahakikisha miradi yote iliyokusudiwa inafanyika.

“Ni kweli kwa sasa Dodoma kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa maji katika maeneo ambayo yapo nje ya mji".

“Msaada ambao tumeupata kutoka LAPF utasaidia kuboresha na kukarabati visima vya maji ili wananchi waondokane na adha ya upatikanaji wa maji,”alisema Kunambi.

KWA MSAADA WA MWANAHALISI ONLINE.com