Friday, December 22, 2017

MKURUGENZI DODOMA KUWAKATIA BIMA YA AFYA 133 WANAOSAFISHA BARABARA MJINI, AWAPA ZAWADI YA KRISMASI NA MWAKA MPYA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (kulia) akimkabidhi mche wa sabuni mmoja ya wafanyakazi wanaosafisha barabara na mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma mara baada baada ya kuzungumza na wafanyakazi hao katika Viwanja vya Nyerere Mjini Dodoma jana. Mkurugenzi huyo aliwapatia wafanyakazi hao wapatao 133 zawadi ya Shilingi 10,000 na Mche mmoja wa sabuni kila mmoja ikiwa ni motisha hususan katika kipindi hiki cha Sikukuu za mwisho wa Mwaka.  PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI
Baadhi ya wafanyakazi wanaosafisha Barabara na Mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma wakifurahia hotuba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) wakati alipofanya nao mkutano katika Viwanja vya Nyerere Mjini Dodoma jana. 
 PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI

Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro (kushoto) akizungumza na wafanyakazi wanaosafisha barabara na mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi (katikati) kuzungumza na wafanyakazi hao. kulia ni msimamizi wa wafanyakazi hao John Lugendo.


Wafanyakazi 133 wanaosafisha barabara na mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma wakikabidhiwa Fedha taslim Shilingi 10,000 na mche wa sabuni kila mmoja ikiwa ni zawadi ya motisha iliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) jana katika Viwanja vya Nerere Mjini Dodoma. Wanaokabidhi ni Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro (wa pili waliokaa) na Afisa Mazingira ambaye ni Msimamzi wa Wafanyakazi hao John Lugendo (wa kwanza waliokaa). PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI
Sehemu ya wafanyakazi wanaosafisha Barabara na Mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) wakati alipofanya nao mkutano katika Viwanja vya Nyerere Mjini Dodoma jana. Kando ni maboksi ya sabuni ambapo kila mmoja alizawadia mche mmoja na fedha taslimu Shilingi 10,000 na Mkurugenzi huyo huku akiwaahidi kuwakatia Bima ya Afya.  PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI

.....................................................

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ameahidi kuwakatia Bima ya Afya wafanyakazi 133 wanaosafisha mitaa na barabara zote za Mji wa Dodoma ili wawe na uhakika wa matibabu wao na familia zao.

Alitoa ahadi hiyo jana alipofanya mkutano na wafanyakazi hao katika viwanja vya Nyerere katikati ya Mji wa Dodoma ambapo pia aliwapatia fedha taslimu Shilingi 10,000 na mche mmoja wa sabuni kila mmoja kama zawadi kuelekea mwisho wa mwaka 2017.

Mkurugenzi Kunambi alisema kuwa, yeye kwa niaba ya Uongozi wa Manispaa  ametoa zawadi na ahadi ya kuwakatia Bima ya matibabu baada ya kufurahishwa na uchapa kazi wao unaopelekea mitaa na barabara za Mji kuwa safi na kupendeza muda wote.

“Hiki tunachowapa leo hakina thamani yeyote kwa kazi kubwa mnayoifanya, bali ni kuonesha kuguswa kwetu tu kama Manispaa…ninyi ni kundi maalum na ni wafanyakazi muhimu sana” alisema Kunambi akizungumza na watumishi hao.

“Nimefurahi kukutana na kuzungumza na ninyi kipindi hiki cha mwisho wa mwaka…nawaahidi mapema mwakani Manispaa itawakatika Bima za Afya wote itakayomwawezesha kila mmoja kutibiwa yeye na wategemezi wake watatu” alifafanua.

Kwa upande wao, wafanyakazi hao ambao wengi wao ni akina Mama walimshukuru Mkurugenzi huyo kwa niaba ya Manispaa kwa kuwajali licha ya kuwa wao ni watumishi wa kada ya chini na wanaofanya kazi kwa mkataba isiyo ya kudumu.

“Tumefurahi sana leo Mkurugenzi wetu umekuja kuongea na sisi na kutupa zawadi na fedha tena katika kipindi cha Sikukuu za mwisho wa mwaka...umetujali sana na sisi tunakuombea kwa Mugu”… alisema mmoja ya akia mama hao akimshukuru Mkurugenzi wa Manispaa.



Thursday, December 21, 2017

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA DODOMA YA KIJANI, AAGIZA HALMASHAURI ZA MKOA HUO KUTUNGA SHERIA NDOGO ZITAKAZOMTAKA KILA MKAZI KUPANDA MITI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiandaa mti wake kabla ya kuupanda mara baada ya kuzindua  programu ya upandaji miti ili kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa Kijani iliyofanyika kwenye chanzo cha maji cha Mzakwe Kata ya Makutupora Mjini Dodoma jana. PICHA ZOTE: RAMADHAI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipanda mti wake mara baada ya kuzindua  programu ya upandaji miti ili kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa Kijani iliyofanyika kwenye chanzo cha maji cha Mzakwe Kata ya Makutupora Mjini Dodoma jana. PICHA ZOTE: RAMADHAI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge akipanda mti katika eneo la Mzakwe Kata ya Makutupora Manispaa ya Dodoma huku akisaidiwa na Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Dodoma FC Jamhuri Kihwelu 'Julio' (mwenye kofia ya kijani) mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kuzindua programu ya  upandaji miti na kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa wa Kijani.
Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe akinyeshea mti  alioupanda katika eneo la Mzakwe Kata ya Makutupora Manispaa ya Dodoma mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kuzindua programu ya  upandaji miti na kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa wa Kijani.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ( kulia ) akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha Cluods Hassan Ngoma wakati wa uzinduzi wa programu ya upandaji miti uliofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan  katika eneo la Mzakwe Kata ya Makutupora Manispaa ya Dodoma. 
Wananchi mbalimbali wakiendelea na zoezi la upandaji miti mara baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kuzindua programu ya  upandaji miti na kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa wa Kijani, katika eneo la Mzakwe Kata ya Makutupora Manispaa ya Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiazungumza kabla ya uzinduzi  wa programu ya upadaji miti ili kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa Kijani iliyofanyika kwenye chanzo cha maji cha Mzakwe Kata ya Makutupora Mjini Dodoma jana. PICHA ZOTE: RAMADHAI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA


......................................................................

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kutunga Sheria Ndogo zitakazomtaka kila Mkazi wa eneo katika Mkoa huo kupanda miti ili kupambana na mabadiliko ya hali tabia Nchi.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa kijani iliyofanyika Desemba 21 mwaka huu katika eneo la Mzakwe Kata ya Makutupora Manispaa ya Dodoma.

Alisema upandaji miti si kwa ajili ya kuhifadhi mazingira tu bali ni fursa ya kiuchumi, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi  ambapo alitolea mfano mti mmoja uliokomaa unaweza kunyonya kiasi cha kilogramu 150 za gesi ya hewa ya ukaa kwa mwaka na hivyo kusaidia kupunguza joto kwenye uso wa dunia, na pia kusaidia kuboresha afya ya mwili na akili.

“Ni dhahiri, kampeni hii ya kuifanya mji wa Dodoma kuwa wa kijani ni kuunga mkono uamuzi wa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamishia Makamo Makuu ya Nchi kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma kwa vitendo.” Alisema.

Akihojiwa na Vyombo vya Habari wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alisema Manispaa ya Dodoma imejipanga kuugeuza Mji wa Dodoma kuwa kivutio kikubwa kimazingira kwani pamoja na kuhakikisha inasimamia na kutekeleza kwa ukamilifu program iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, pia Manispaa itatenga eneo maalum la ukanda wa kijani (Green Belt) ili kuufanya Mji huo kuwa wa kipekee nchini.



Wednesday, December 20, 2017

RC ATEMBELEA DAMPO LA KISASA MANISPAA YA DODOMA, ASEMA DODOMA LAZIMA IWE SAFI ZAIDI


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (katikati mbele) akiwa na Mhandishi wa Mazingira wa Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida (kulia) na Meneja wa Dampo la Kisasa la Manispaa hiyo John Chiwanga (kushoto) wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipofanya ziara fupi katika Dampo hilo hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (kushoto) akipokea taarifa fupi kuhusu Dampo la kisasa la Chidaya Manispaa ya Dodoma kutoka kwa Mhandishi wa Mazingira wa Manispaa hiyo Barnabas Faida (kulia) wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipofanya ziara fupi katika Dampo hilo hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (wa pili kushoto) akipatiwa maelezo kuhusu mfumo wa upimaji uzito wa taka zinazoletwa katika Dampo la kisasa la Chidaya Manispaa ya Dodoma unavyofanya kazi kutoka kwa Mhandishi wa Mazingira wa Manispaa hiyo Barnabas Faida (wa pili kulia) wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipofanya ziara fupi katika Dampo hilo hivi karibuni. PICHA ZOTE: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI WA MANISPAA
Moja ya magari maalum kwa ajili ya kubeba uchafu ya Manispaa ya Dodoma likipimwa uzito kabla ya kuingia kumwaga uchafu katika Dampo hili la kisasa lilipo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu katika Manispaa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (kushoto) akiwa katika sehemu ya Dampo la kisasa la Chidaya Manispaa ya Dodoma iliyoanza kutumika huku akipata maelezo kutoka kwa Mhandishi wa Mazingira wa Manispaa hiyo Barnabas Faida (kulia) wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipofanya ziara fupi katika Dampo hilo hivi karibuni.
Sehemu ya pili ya Dampo la kisasa la Chidaya  katika Manispaa ya Dodoma linalotumia Teknolojia ya kuzika taka ardhini ambayo bado haijaanza kutumika kwa sasa.

 .........................................................

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge amesema Mji wa Dodoma hauna sababu ya kuwa mchafu kwa sababu Manispaa ya Dodoma imetekeleza mradi wa ujenzi wa dampo la kisasa na litakalodumu kwa miaka mingi ijayo.
 Aliyasema hayo baada ya kutembelea dampo la kisasa la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu takribani umbali wa kilometa 12 kutoka katikati ya Mji wa Dodoma.

Katika ziara hiyo fupi, Mkuu huyo wa Mkoa alioongozana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rehema Madenge pamoja na Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji wa Manispaa hiyo Dickson Kimaro aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.

Awali mara baada ya kuwasili katika eneo la dampo, Mheshimiwa Mahenge alielezwa jinsi Dampo hilo la kisasa linavyofanya kazi na Mhandisi wa Mazingira wa Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida, aliyemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, dampo hilo linatumia teknolojia ya kuzika taka ardhini (Sanitary Landfill) ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wakazi wa maeneo ya karibu na dampo.


Mhandisi Faida alimjulisha Mheshimiwa Mahenge kuwa, dampo hilo tayari limeanza kufanya kazi mapema mwaka huu, na limejengwa kwa fedha za mradi wa Kuimarisha Miji ya Kimkakati Tanzania (TSCP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kuratibiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Monday, December 18, 2017

WAKAZI WA MTAA DODOMA WALAMBA MILIONI 1 KWA KUFANYA USAFI WA MAZINGIRA KATIKA MTAA WAO

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (kulia) alipowaongoza wakazi wa Mtaa wa Zahanati Kata ya Kikuyu Kaskazini (pichani nyuma) kufanya usafi wa Mazaingira kila Jumamosi kufuatia Kmapeni ya Usafi wa Mji aliyeianzisha yeye. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi. PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI.
Wakazi wa Mtaa wa Zahanati Kata ya Kikuyu Kaskazini Manispaa ya Dodoma wakifanya usafi wa Mazaingira wa kila Jumamosi kufuatia kampeni ya Usafi wa Mji iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa huo Dokta Binilith Mahenge.
Zoezi la usafi likiendelea katika Mtaa za Zahanati Kata ya Kikuyu Kaskazini Manispaa ya  Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge (kulia) akisikiliza kero mbalimbali za Wananchi wa Mtaa wa Zahanati Kata ya Kikuyu Kaskazini Manispaa ya Dodoma baada ya zoezi la usafi wa Mazingira wa kila Jumamosi. Mkuu huyo wa Mkoa amejiwekea utaratibi wa kusikiliza kero za wakazi wa Mtaa husika baada ya kufanya nao usafi wa Mazingira. PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA.

...............................................

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge ameahidi kutoa motisha ya Shilingi 1,000,000 kwa wakazi wa mtaa wa Zahati uliopo Kata ya Kikuyu Kaskazini katika Manispaa ya Dodoma kufuatia wakazi hao kujitokeza kwa wingi katika zoezi la usafi wa Mazingira unaofanyika kila Jumamosi katika Manispaa hiyo.

Mheshimiwa Mahenge alitoa ahadi hiyo wakati alipowaongoza wakazi hao katika zoezi la usafi wa Mazingira katika Mtaa huo mwishoni mwa wiki, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya kufanya usafi wa Mazingira kila Jumamosi aliyoianzisha yeye mara tu baada ya kuhamishiwa Mkoa humo, kwa lengo la kuuweka Mji Mkuu wa Nchi katika hali ya usafi wakati wote.

Alisema fedha atakazowapa wakazi wa Mtaa huo ni motisha na kuwaunga mkono kwa juhudi walizoonesha na kwamba zitawasaidia katika kuboresha hali ya usafi katika eneo lao kwa kununua vifaa mbalimbali vya kufanyia usafi.

Alisema amefurahishwa na namna wakazi wa Mtaa wa Zahati walivyojitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo na kutoa wito kwa wakazi wa maeneo mengine katika Manispaa kuiga mfano huo ili kwa pamoja waweze kuufanya Mji wa Dodoma kuwa namba moja kwa usafi wa Mazingira nchini.  

Wednesday, December 13, 2017

KAMPENI YA USAFI DODOMA: ABIRIA WALIPONZA BASI LA IMMO EXPRESS NA SPIDER,YAKUMBANA NA RUNGU LA MANISPAA


Basi la Kampuni ya Spider lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Kanda ya Ziwa likiwa limeegeshwa jirani na mzani wa kupima uzito wa magari uliopo Kata ya Nala Manispaa ya Dodoma baada ya kuzuiwa na askari Jamii wa Manispaa hiyo kufuatia baadhi ya abiria wake kudaiwa kutupa taka ovyo nje ya basi na kuchafua mazingira. 

..................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imeendelea kuwakumbusha wakazi wa Manispaa kuendelea kuzingatia suala la usafi  wa Mazingira na kutotupa taka ovyo katika lolote ndani Manispaa hiyo kwani atakayefaya hivyo atapambana na mkono wa sheria ikiwemo kulipa faini inayoanzia shilingi 50,000 hadi 300,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Rai hiyo pia inawahusu wasafiri wote wanaoingia Mjini Dodoma au kupitia wakielekea mikoa mingine  kwamba wajiepusha kutupa uchafu ovyo nje ya vyombo vyao vya usafiri ikiwemo mabaki ya vyakula kwani wakibainika watachuliwa hatua za kisheria kama wachafuzi wengine.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji wa Halmashauri hiyo Dickson Kimaro jana wakati alipowaongoza askari Jamii wa Manispaa hiyo kukamata mabasi ya Kampuni ya Immo Express na Spider baada ya baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri na mabasi hayo kudaiwa kutupa uchafu katika eneo la Nala barabara kuu ya Dodoma-Singida, ikiwemo mifuko ya plastiki iliyokuwa na mabaki ya vyakula.

Kufuatia tukio hilo, mabasi hayo yalitozwa faini ya Shilingi 50,000 kwa kila kampuni na baada ya kulipa yaliachiwa na kuendelea na safari.

Manispaa ya Dodoma imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha Mji Mkuu wa Nchi unakuwa safi muda wote, ambapo hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge alitangaza Kampeni ya Usafi wa Mazingira mjini humo ambapo sasa usafi utafanyika Jumamosi ya kila wiki.

Katika utaratibu huo, Wananchi wote wanatakiwa kufanya usafi katika maeneo yao ya makazi, maeneo ya biashara, na maeneo ya wazi.  



Tuesday, December 12, 2017

MANISPAA YA DODOMA YATEKELEZA AGIZO LA SERIKALI KUANGAMIZA MAZALIA YA MBU WAENEZAO MALARIA


Kikosi kazi kinachofanya zoezi la kupulizia dawa ya kuua vimelea vya mazalia ya Mbu waenezao ugonjwa wa Malaria katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kikiendelea na kazi hiyo katika maeneo mbalimbali baada ya kuanza kwa zoezi hilo hilo jana.

Kikosi kazi kinachofanya zoezi la kupulizia dawa ya kuua vimelea vya mazalia ya Mbu waenezao ugonjwa wa Malaria katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kikiendelea na kazi hiyo katika maeneo mbalimbali baada ya kuanza kwa zoezi hilo hilo jana.

Kikosi kazi kinachofanya zoezi la kupulizia dawa ya kuua vimelea vya mazalia ya Mbu waenezao ugonjwa wa Malaria katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kikiendelea na kazi hiyo katika maeneo mbalimbali baada ya kuanza kwa zoezi hilo hilo jana.

Kikosi kazi kinachofanya zoezi la kupulizia dawa ya kuua vimelea vya mazalia ya Mbu waenezao ugonjwa wa Malaria katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kikiendelea na kazi hiyo katika maeneo mbalimbali baada ya kuanza kwa zoezi hilo hilo jana.


Friday, December 8, 2017

WALIOVUNJIWA VIBANDA KWENYE HIFADHI YA RELI DODOMA WAPATIWA ENEO NA MANISPAA


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (wa pili kushoto) akiteta jambo na wafanyabiashara wakati akitoka katika eneo la Stendi ya Jamatini Mjini Dodoma baada ya kuzungumza na wafanyabiashara waliovunjiwa vibanda vyao kupisha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde (wa pili kushoto) akizungumza katika mkutano na Wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma baada ya Vibanda vyao kubomolewa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) kupisha mradi wa ujenzi wa Reli kisasa. Kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi. Kushoto ni Katibu wa Wafanyabiashara hao John Banda.
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma wakifuatilia mkutano wao na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi.


                  ..............................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma inatarajia kuwapatia eneo wafanyabiashara zaidi ya 550 waliovunjiwa vibanda vyao na kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) katika stendi ya mabasi madogo ya  Jamatini ili kupisha utekelezaji wa mradi wa Reli ya kisasa, ili waendelee kufanya biashara zao kama kawaida.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa, Manispaa iko katika hatua za mwisho kuandaa eneo la Makole D-Center kwa kuweka miundombinu muhimu ikiwemo mfumo wa maji safi na maji taka ili wafanyabiashara hao waanze kufanya shughuli zao mara moja na katika mazingira rafiki na salama katika eneo hilo.

Aliyasema hayo alipotembelea eneo la Jamatini na Stendi Kuu Novemba 6 mwaka huu, akiambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira Anthony Mavunde ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, pamoja na Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Jumanne Ngede kwa lengo la kuwapa pole wafanyabiashara hao na kuwajulisha hatua zilizochukuliwa na Viongozi mbalimbali katika kuhakikisha tatizo linalowakabili linapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

 Aliwatoa hofu ya kuwa eneo hilo halitakuwa na wateja wengi kama ilivyokuwa eneo la stendi ya Jamatini, ambapo aliwaambia tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge ametoa maelekezo kwa Manispaa na Sumatra kuhakikisha daladala zinakuwa na ruti inayopita katika eneo hilo jipya la biashara ambapo abiria watakuwa na kituo cha kupanda na kushuka na hivyo kuongeza mzunguko wa wateja katika eneo hilo, na kwamba utekelezaji wa maelekezo hayo umeshaanza kufanyiwa kazi na Sumatra.

Akizungumza na wafanyabiashara ya usafiri wa mabasi katika Stendi Kuu ya mabasi ya mikoani, Mkurugenzi Kunambi aliwaambia kuwa, Manispaa kwa kushauriana na uongozi wa Mkoa na wadau kama Sumatra imepanga kuhamishia Stendi hiyo katika eneo la Chaduru au kwenye eneo la viwanja vya Nanenane vilivyopo Kata ya Nzuguni barabara kuu ya Dodoma-Dar es Salaam.

Alisema Manispaa itazungumza na uongozi wa wasafirishaji ili kupata mapendekezo yao  juu ya eneo rafiki zaidi miongoni mwa maeneo hayo mawili.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Mavunde aliwataka wote walioathiriwa na zoezi hilo la bomoabomoa wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Mamlaka na Viongozi wakifanya juhudi za makusudi kuwatafutia maeneo rafiki kwa shughuli zao huku Naibu Meya Ngede akiwahakikishia kuwa Baraza la Madiwani litasimamia kikamilifu suala la upatikaaji wa maeneo hayo.

Thursday, December 7, 2017

MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA AMALIZA HOFU YA WAFANYABIASHARA 2,500

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Sabasaba (hawapo pichani) Mjini Dodoma jana ambapo aliwahakikishia kuwa hawatahamishwa katika soko hilo. 

Sehemu ya Wafanyabiashara ya Manispaa ya Dodoma wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa Mkurugenzi huyo na wafayabiashara wa soko hilo jana.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya DodomaJumanne Ngede akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Sabasaba Mjini Dodoma jana ambapo alifuatana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi. 

Monday, December 4, 2017

USAFI WA MAZINGIRA DODOMA SASA KILA WIKI, WATAKAOKAIDI FAINI 50,000 AU JELA MIEZI 6


Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro  (kushoto) akifuatilia usafishaji wa barabara na mitaro katika barabara ya Dodoma-Singida wakati wa zoezi la usafi wa Mazingira unaofanywa kila Jumamosi ikiwa ni Kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge.
Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Uhuru Manispaa ya Dodoma Ally Kheri (kulia) akishiriki zoezi la usafi wa Mazingira katika Mtaa wa Barabara ya 8 katikati ya Mji wa Dodoma wakati wa zoezi la usafi wa Mazingira unaofanywa kila Jumamosi ikiwa ni Kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge.
........................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imepanga kutumia askari wa Mgambo 30 watakaokuwa wanafanya doria katika viunga vya Mji ili kudhibiti watu wanaochafua mazingira kwa kutupa taka ovyo ikiwa ni namna mojawapo ya kuhakikisha mji huo unakuwa safi wakati wote ikizingatiwa kuwa ndiyo Makao Makuu ya Nchi.

Hatua hiyo inafuatia kampeni ya usafi wa mazingira iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge ya kufanya usafi siku ya Jumamosi kila wiki.

Akizungumza wakati wa zoezi la usafi mwishoni mwa Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema askari Mgambo 30 waliofuzu mafunzo wako tayari na kwamba Manispaa inatarajia kuanza kuwatumia wiki hii ya kwanza ya mwezi Desemba.  


Aliwashauri wakazi wa Dodoma na wageni kujiepusha na utupaji wa taka ovyo, na kwamba atakayebainika na kuthibitika kufanya hivyo atatozwa faini kati ya Shilingi 50,000 hadi 300,000 kulingana na mazingira ya tukio papo hapo na endapo atashindwa kulipa atatumikia kifungo cha miezi sita gerezani.