Sehemu ya pili ya Dampo la kisasa la Chidaya katika Manispaa ya Dodoma linalotumia Teknolojia ya kuzika taka ardhini ambayo bado haijaanza kutumika kwa sasa. |
.........................................................
MKUU wa Mkoa wa Dodoma
Dokta Binilith Mahenge amesema Mji wa Dodoma hauna sababu ya kuwa mchafu kwa
sababu Manispaa ya Dodoma imetekeleza mradi wa ujenzi wa dampo la kisasa na
litakalodumu kwa miaka mingi ijayo.
Aliyasema hayo baada ya kutembelea dampo la
kisasa la Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma lililopo eneo la Chidaya Kata ya
Matumbulu takribani umbali wa kilometa 12 kutoka katikati ya Mji wa Dodoma.
Katika ziara hiyo fupi,
Mkuu huyo wa Mkoa alioongozana na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rehema Madenge
pamoja na Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji wa Manispaa hiyo Dickson
Kimaro aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.
Awali mara baada ya
kuwasili katika eneo la dampo, Mheshimiwa Mahenge alielezwa jinsi Dampo hilo la
kisasa linavyofanya kazi na Mhandisi wa Mazingira wa Manispaa ya Dodoma
Barnabas Faida, aliyemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa, dampo hilo linatumia teknolojia
ya kuzika taka ardhini (Sanitary Landfill) ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya
za wakazi wa maeneo ya karibu na dampo.
Mhandisi Faida alimjulisha
Mheshimiwa Mahenge kuwa, dampo hilo tayari limeanza kufanya kazi mapema mwaka
huu, na limejengwa kwa fedha za mradi wa Kuimarisha Miji ya Kimkakati Tanzania (TSCP)
unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kuratibiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
No comments:
Post a Comment