..............................................
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma inatarajia kuwapatia eneo wafanyabiashara zaidi ya 550 waliovunjiwa vibanda vyao na kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) katika stendi ya mabasi madogo ya Jamatini ili kupisha utekelezaji wa mradi wa Reli ya kisasa, ili waendelee kufanya biashara zao kama kawaida.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amewaeleza wafanyabiashara hao
kuwa, Manispaa iko katika hatua za mwisho kuandaa eneo la Makole D-Center kwa
kuweka miundombinu muhimu ikiwemo mfumo wa maji safi na maji taka ili
wafanyabiashara hao waanze kufanya shughuli zao mara moja na katika mazingira
rafiki na salama katika eneo hilo.
Aliyasema hayo
alipotembelea eneo la Jamatini na Stendi Kuu Novemba 6 mwaka huu, akiambatana
na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira Anthony Mavunde
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, pamoja na Naibu Meya wa Halmashauri ya
Manispaa hiyo Jumanne Ngede kwa lengo la kuwapa pole wafanyabiashara hao na
kuwajulisha hatua zilizochukuliwa na Viongozi mbalimbali katika kuhakikisha
tatizo linalowakabili linapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Aliwatoa hofu ya kuwa eneo hilo halitakuwa na
wateja wengi kama ilivyokuwa eneo la stendi ya Jamatini, ambapo aliwaambia
tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge ametoa maelekezo kwa
Manispaa na Sumatra kuhakikisha daladala zinakuwa na ruti inayopita katika eneo
hilo jipya la biashara ambapo abiria watakuwa na kituo cha kupanda na kushuka
na hivyo kuongeza mzunguko wa wateja katika eneo hilo, na kwamba utekelezaji wa
maelekezo hayo umeshaanza kufanyiwa kazi na Sumatra.
Akizungumza na
wafanyabiashara ya usafiri wa mabasi katika Stendi Kuu ya mabasi ya mikoani,
Mkurugenzi Kunambi aliwaambia kuwa, Manispaa kwa kushauriana na uongozi wa Mkoa
na wadau kama Sumatra imepanga kuhamishia Stendi hiyo katika eneo la Chaduru au
kwenye eneo la viwanja vya Nanenane vilivyopo Kata ya Nzuguni barabara kuu ya
Dodoma-Dar es Salaam.
Alisema Manispaa
itazungumza na uongozi wa wasafirishaji ili kupata mapendekezo yao juu ya eneo rafiki zaidi miongoni mwa maeneo
hayo mawili.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri Mavunde aliwataka wote walioathiriwa na zoezi hilo la bomoabomoa wawe
watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Mamlaka na Viongozi wakifanya juhudi
za makusudi kuwatafutia maeneo rafiki kwa shughuli zao huku Naibu Meya Ngede
akiwahakikishia kuwa Baraza la Madiwani litasimamia kikamilifu suala la
upatikaaji wa maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment