Shughuli za usafirishaji zikiendelea katika iliyokuwa Stendi Kuu ya Mabasi Mjini Dodoma kabla ya Stendi hiyo kuhamishiwa katika eneo la Nanenane kuanzia leo Machi 29, 2018. Picha: Mtandao. |
...............................................
HATIMAYE Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma imetekeleza azimio la Mamlaka na wadau wa Usafirishaji katika
ngazi ya Wilaya na Mkoa la kuhamishia Stendi Kuu ya mabasi katika eneo la
Nanenane Kata ya Nzuguni Barabara Kuu ya Dodoma-Dar es Salaam, ambapo kuanzia
leo Machi 29, 2018 huduma za mabasi hayo zimeanza kutolewa katika eneo hilo.
Uamuzi huo umefikiwa
kufuata eneo lililokuwa likitumika kwa muda mrefu kama Stendi Kuu kuchukuliwa na
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Nchini (RAHCO), kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafiri wa Reli.
Kufuatia hali hiyo, wadau
mbalimbali wa usafirishaji wakiwemo Jeshi la Polisi, Wafanyabiashara ya Usafirishaji,
Mamlaka inayosimamia usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA), Serikali ya Mkoa
na Wilaya, pamoja na Manispaa walijadili suala hilo kwa nyakati tofauti na
kukubaliana eneo la Nanenane litakidhi mahitaji ya huduma hiyo kwa sasa.
Awali, Mkurugenzi wa
Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi aliteua ‘timu’ ya kushughulikia suala hilo na
kumshauri eneo litakakidhi kutoa huduma ya usafiri wa Mikoani kwa Wananchi ili
lipendekezwe, kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu ya msingi kama Maji na Vyoo,
ambapo eneo la Nanenane lilipendekezwa kwani lilishawahi kutumika kama stendi
katika miaka ya nyuma.
Kaimu Mkuu wa Idara ya
Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Ludigija Ndatwa amesema kuanzia leo
mabasi yote ya Mikoani ni lazima yapakie na kushusha abiria wao katika stendi
hiyo teule na kwamba wadau wote wameahidi kutoa ushirikiano.
“Hivi tunavyoongea nipo
hapa Nanenane na wadau wote wapo hapa…wanatoa ushirikiano wa hali juu kwa kweli
na kila kitu kinaenda sawa… mpaka muda huu mabasi yote yako huku kwa ajili ya
kufanya safari zao” alisema Mhandisi Ludigija.