Monday, July 30, 2018

JIJI LA DODOMA LATOA MILIONI 950 KWA WANAWAKE NA VIJANA, WAZIRI JAFO AKABIDHI HUNDI





....................................................................

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 950 zilizotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoka katika Mfuko wa Wanawake, Vijana, na Walemavu kwa ajili ya vikundi 234 vya Wanawake na Vijana huku akitoa wito kwa Jiji hilo kutafuta masoko ya bidhaa  zinazozalishwa na vikundi hivyo kwani imekuwa moja ya changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Hafla ya kukabidhi hundi hiyo kwa Wanavikundi hao imefanyika hivi karibuni katika Viwanja vya Nyerere vilivyopo katikati ya Jiji la Dodoma.

‘’Viongozi muandae Mpango Mkakati wa kuwa na masoko ya kuuza bidhaa za wajasiriamali hawa, nimeona wana bidhaa nzuri sana ambazo unaweza usiamini kama zinatoka Dododma, lakini kila mmoja ukimuuliza soko anakwambia hana soko maalumu’’ Alisema Waziri Jafo.

Aliongeza ‘’Mbali na kuwapa fedha lakini pia nakuagiza Mkurugenzi wa Jiji (Godwin Kunambi ) na Mstahiki Meya (Profesa David Mwamfupe) mtafute eneo la kimkakati kwa ajili ya hawa mnaowapatia mkopo na vikundi vyote vilivyowezeshwa na Halmashauri hii, kwa kufanya hivi tunaweza kuwa na eneo moja maalumu ambalo litakuwa linafanya maonyesho kwa mwaka mzima’’ Alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alimweleza Waziri Jafo kuwa, fedha hizo zinatokana na ukusanyaji bora wa mapato ya ndani na kwamba kwa sasa Halmashauri inatoa mikopo mikubwa kuanzia Shilingi milioni moja hadi milioni kumi na kutoa wito kwa wajasiriamali kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kukidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.

Alisema fedha hizo zinatolewa kwa vikundi 234 vya Wajasiriamali, vikiwemo 168 vya Wanawake pamoja na vikundi 66 vya Vijana.


1 comment: