Friday, December 22, 2017

MKURUGENZI DODOMA KUWAKATIA BIMA YA AFYA 133 WANAOSAFISHA BARABARA MJINI, AWAPA ZAWADI YA KRISMASI NA MWAKA MPYA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (kulia) akimkabidhi mche wa sabuni mmoja ya wafanyakazi wanaosafisha barabara na mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma mara baada baada ya kuzungumza na wafanyakazi hao katika Viwanja vya Nyerere Mjini Dodoma jana. Mkurugenzi huyo aliwapatia wafanyakazi hao wapatao 133 zawadi ya Shilingi 10,000 na Mche mmoja wa sabuni kila mmoja ikiwa ni motisha hususan katika kipindi hiki cha Sikukuu za mwisho wa Mwaka.  PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI
Baadhi ya wafanyakazi wanaosafisha Barabara na Mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma wakifurahia hotuba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) wakati alipofanya nao mkutano katika Viwanja vya Nyerere Mjini Dodoma jana. 
 PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI

Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro (kushoto) akizungumza na wafanyakazi wanaosafisha barabara na mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi (katikati) kuzungumza na wafanyakazi hao. kulia ni msimamizi wa wafanyakazi hao John Lugendo.


Wafanyakazi 133 wanaosafisha barabara na mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma wakikabidhiwa Fedha taslim Shilingi 10,000 na mche wa sabuni kila mmoja ikiwa ni zawadi ya motisha iliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) jana katika Viwanja vya Nerere Mjini Dodoma. Wanaokabidhi ni Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafishaji Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro (wa pili waliokaa) na Afisa Mazingira ambaye ni Msimamzi wa Wafanyakazi hao John Lugendo (wa kwanza waliokaa). PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI
Sehemu ya wafanyakazi wanaosafisha Barabara na Mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (hayupo pichani) wakati alipofanya nao mkutano katika Viwanja vya Nyerere Mjini Dodoma jana. Kando ni maboksi ya sabuni ambapo kila mmoja alizawadia mche mmoja na fedha taslimu Shilingi 10,000 na Mkurugenzi huyo huku akiwaahidi kuwakatia Bima ya Afya.  PICHA: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI

.....................................................

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ameahidi kuwakatia Bima ya Afya wafanyakazi 133 wanaosafisha mitaa na barabara zote za Mji wa Dodoma ili wawe na uhakika wa matibabu wao na familia zao.

Alitoa ahadi hiyo jana alipofanya mkutano na wafanyakazi hao katika viwanja vya Nyerere katikati ya Mji wa Dodoma ambapo pia aliwapatia fedha taslimu Shilingi 10,000 na mche mmoja wa sabuni kila mmoja kama zawadi kuelekea mwisho wa mwaka 2017.

Mkurugenzi Kunambi alisema kuwa, yeye kwa niaba ya Uongozi wa Manispaa  ametoa zawadi na ahadi ya kuwakatia Bima ya matibabu baada ya kufurahishwa na uchapa kazi wao unaopelekea mitaa na barabara za Mji kuwa safi na kupendeza muda wote.

“Hiki tunachowapa leo hakina thamani yeyote kwa kazi kubwa mnayoifanya, bali ni kuonesha kuguswa kwetu tu kama Manispaa…ninyi ni kundi maalum na ni wafanyakazi muhimu sana” alisema Kunambi akizungumza na watumishi hao.

“Nimefurahi kukutana na kuzungumza na ninyi kipindi hiki cha mwisho wa mwaka…nawaahidi mapema mwakani Manispaa itawakatika Bima za Afya wote itakayomwawezesha kila mmoja kutibiwa yeye na wategemezi wake watatu” alifafanua.

Kwa upande wao, wafanyakazi hao ambao wengi wao ni akina Mama walimshukuru Mkurugenzi huyo kwa niaba ya Manispaa kwa kuwajali licha ya kuwa wao ni watumishi wa kada ya chini na wanaofanya kazi kwa mkataba isiyo ya kudumu.

“Tumefurahi sana leo Mkurugenzi wetu umekuja kuongea na sisi na kutupa zawadi na fedha tena katika kipindi cha Sikukuu za mwisho wa mwaka...umetujali sana na sisi tunakuombea kwa Mugu”… alisema mmoja ya akia mama hao akimshukuru Mkurugenzi wa Manispaa.



No comments:

Post a Comment