Friday, May 25, 2018

MKURUGENZI JIJI LA DODOMA ATANGAZA NEEMA KWA WATEJA WA VIWANJA


Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo ambapo ameongeza muda wa wateja wa Viwanja kulipa gharama za Viwanja vyao kutoka Mwezi mmoja wa awali hadi miezi mitatu sasa.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo ambapo ameongeza muda wa wateja wa Viwanja kulipa gharama za Viwanja vyao kutoka Mwezi mmoja wa awali hadi miezi mitatu sasa.

Mtaalamu wa Jiji la Dodoma akimuelekeza mteja kwenye ramani inayoonesha mgawanyo wa Viwanja ili aweze kuchagua kiwanja kwa mujibu wa mahitaji yake katika zoezi la uuzwaji wa Viwanja linaloendelea sasahivi katika Halmashauri ya Jiji hilo.
Ramani ya Tanzania ikionesha Jiji la Dodoma lilipo kutoka katika Mikoa mingine yote ya Tanzania.

..............................................................................


HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeongeza muda wa kulipia Viwanja kwa wateja wake wote walionunua Viwanja kuanzia Aprili 20, mwaka huu kutoka siku 30 yaani Mwezi mmoja hadi siku 90 yaani miezi mitatu.

Aidha, Halmashauri hiyo inatarajia kuendelea kuuza Viwanja vya eneo la Iyumbu kuanzia tarehe 5 Juni, 2018 kwani tayari imeshamaliza kazi ya kushughulikia malalamiko ya Wakazi wa Ngaloni walioibuka na kudai kutolipwa fidia hapo awali.

Hayo yametangazwa na Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi wakati akiongea na Waandishi wa Habari Jijini humo leo ambapo amesema Halmashauri imefikia uamuzi huo baada ya kuridhika na mwenendo wa wateja kulipia Viwanja vyao ambapo mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 4 zimeshalipwa kwa Wananchi kama fidia ya maeneo yao yaliyotwaliwa wakati wa upimaji.

Alitoa wito kwa wateja wote walionunua viwanja na wanaoendelea kununua kutumia muda ulioongezwa kama fursa ya kukamilisha malipo yao ili kuepuka usumbufu usio wa lazima baada ya muda huo kumalizika.

“Kwa wale wote waliokuwa wanasubiri Viwanja vya Iyumbu wafike katika eneo letu la kuuzia Viwanja ambalo ni Ofisi za Manispaa ya zamani jirani na Sabasaba siku ya tarehe 5 mwezi ujao…tutaanza kuviuza siku hiyo” alisema Kunambi.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa Jiji ametoa muda wa miezi mitatu kwa watu wote waliopewa Viwanja na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) katika maeneo ya Njedengwa, Miganga, Mkonze, Iyumbu New Town Center, na Mkalama na hawajakamilisha malipo ya Viwanja hivyo kukamilisha ndani ya kipindi hicho vinginevyo Halmashauri itavitwaa kwa mujibu wa Sheria na kuviuza kwa wateja wengine wenye mahitaji.  


No comments:

Post a Comment