Saturday, May 26, 2018

WAZIRI JAFFO: JIJI LA DODOMA NI MFANO NCHINI KUWATAMBUA WAZEE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali (TAMISEMI) Selemani Jaffo akimkabidhi kitambulisho rasmi cha kumtambua mmoja ya Wazee wa Kata ya Mkonze Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakati Waziri huyo alipozindua zoezi hilo mapema leo Mei 26, 2018. Wanaoshudia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi (kulia kwa Waziri) na Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi (mwenye shati jeupe). Kushoto kwa Waziri aliyevaa miwani ni Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Hamadi Nyembea.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali (TAMISEMI) Selemani Jaffo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na badhi ya Waze wa Kata ya Mkonze Jijini Dodoma baada ya kuzindua na kuwakabidhi vitambulisho rasmi vya kuwatambua  Wazee katika Halmashauri ya Jiji hilo mapema leo Mei 26, 2018. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi na kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi (mwenye shati jeupe). 
Baadhi ya Wazee wa Kata ya Mkonze Jijini Dodoma wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa utaoji wa vitambulisho vya Wazee uliofanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Selemani Jaffo leo Mei 26, 2018.
Diwani wa Kata ya Mkonze Jiji la Dodoma David Bochela akitoa neno wakati wa hafla ya uzinduzi wa utaoji wa vitambulisho vya Wazee uliofanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Selemani Jaffo leo Mei 26, 2018 katika Kata hiyo.

...........................................................................


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo amesema, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni ya mfano Nchini katika kuwatambua na kuwatengenezea vitambulisho maalum vya kuwatambulisha Wazee katika maeneo ya huduma mbalimbali ikwemo matibabu, akiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 inayolenga katika  kuhakikisha kuwa, Wazee wa Tanzania wanatambuliwa na wanapewa fursa ya kushiriki katika mambo yanayohusu maisha ya kila siku na kupata huduma zote za msingi.

Waziri Jaffo ameyasema hayo mapema leo Mei 26, 2018, alipokuwa akizindua rasmi zoezi la utoaji wa vitambulisho vya Wazee kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Kata ya Mkonze iliyopo umbali wa kilometa 4.7 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma.

Akizungumza wakati wa  hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi na Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi, Waziri huyo aliagiza Halmashauri za Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara  kuhakikisha zinawatambua Wazee katika maeneo yao na kuwasilisha taarifa kamili ya kila Mkoa kuhusu Wazee katika  Ofisi yake ifikapo Juni 30, mwka huu.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekeleaji wa zoezi hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, Mganga Mkuu wa Jiji hilo Hamadi Nyembea alisema Halmashauri ilianza zoezi hilo kwa kuwatambua Wazee katika Kata zote 41 za Jiji la Dodoma, na kwamba mpaka sasa jumla ya Wazee 15, 854 wameshatambuliwa kutoka katika Kata 33, sawa na asilimia 80.5.

Alisema, hatua iliyofuata ni kuwapiga picha Wazee waliotambuliwa na kuwatengenezea vitambulisho, zoezi lililoanza rasmi mwezi Februari Mwaka huu, ambapo jumla ya Wazee 1,118 wameshapigwa picha katika Kata za Mkonze, Mnadani, Uhuru, Madukani, Makole na Majengo na kwamba kazi hiyo inaendelea katika Kata zilizobaki.

“Jumla ya vitambulisho 564 vya Wazee vimeshakamilika na wahusika watakabidhiwa rasmi leo kwa ajili ya kuanza kuvitumia” alisema Mganga Mkuu huyo wakati akiwasilisha taarifa hiyo.


No comments:

Post a Comment