Thursday, May 17, 2018

LAAC YA UGANDA ZIARANI DODOMA, YAFURAHIA MJI WA SERIAKLI


Mwakilishi wa Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Emanuel Manyanga akiwasilisha taarifa ya Miradi iliyotekelezwa na itakayotekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Tanzanzia (TSCP) mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa ya Nchini Uganda ilipokuwa katika ziara ya kujifunza katika Manispaa hiyo jana. PICHA: OFISI YA MKURUGENZI
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa ya Nchini Uganda Reagan Okumu (kushoto) akizungumza wakati alipowaongoza wajumbe wa Kamati hiyo katika ziara ya kujifunza katika Manispaa ya Dodoma jana.
Mhandisi wa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesbu za Srikali za Mitaa ya Uganda ilipotembelea Halmashauri hiyo jana.
WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ya Bunge la Uganda wakifuatilia taarifa za miradi ya Ujenzi iliyokuwa akiwasilishwa na Mhandisi Emanuel Manyanga kutoka Idara ya Ujenzi ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma walipofanya ziara ya kujifunza juu ya utekelezaji wa miradi ya Kimkakati. 

............................................................

WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ya Bunge la Uganda wameishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa kuipatia Serikali ya Nchi hiyo kiwanja chenye ukubwa wa eka tano katika Kata ya Mtumba eneo utakapojengwa Mji wa Serikali.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Reagan Okumu alitoa Shukrani hizo jana wakati Kamati hiyo ilipotembelea Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma walipokuwa katika ziara ya siku moja ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama Dampo la kisasa la kuhifadhia taka kwa kuzifukia ardhini (Sanitary Land Fill) lililopo Kata ya Matumbulu ambalo ni moja ya miradi mikubwa katika eneo la usafi na utunzaji wa mazingira.

Awali akizungumza mbele ya Kamati hiyo, Mhandisi wa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi, aliwajulisha wajumbe hao kuwa, Halmashauri imetenga na kupima eneo litakalojengwa Mji wa Serikali hapa Dodoma na kwamba Serikali ya Uganda imepewa kiwanja chenye ukubwa wa eka tano kwa ajili ya matumizi ya kiofisi, ambapo pia walioneshwa ramani ya eneo hilo.

Wajumbe wa Kamati hiyo waliezea kufurahishwa kwao na hatua hiyo huku wakiahidi kufikisha taarifa hizo njema kwa Wananchi wa Uganda mara watakaporejea Nchini humo.
   

Saturday, April 28, 2018

MADIWANI MWANZA WAWEKA HISTORIA JIJINI DODOMA

Diwani wa Kata ya Nyamagana Jijini Mwanza ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji hilo Mhe. Bhiku Kotecha (wa pili kushoto-mbele) akiwa na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Halmashauri hiyo walipotembelea Dampo la kisasa la kuhifadhia takataka lililopo eneo la Chidaya Jijini Dodoma jana. Mbele kushoto ni Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida na kulia ni Afisa Habari wa Jiji la Mwanza Martin Sawema. PICHA:DCC
Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida na (kuhoto) akitoa maelezo kuhusu mradi wa Dampo la kisasa la Chidaya kwa Madiwani na Wataalam wa Jiji la Mwanza waliotembelea eneo hilo jana Aprili 27, 2018 kwa lengo la kujifunza. 


Operesheni za kuhifadhi takataka zikiendelea katika Dampo la kisasa la Chidaya Jijini Dodoma.
Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida na (kuhoto) akifuatilia  maswali kuhusu mradi wa Dampo la kisasa la Chidaya kutoka kwa Madiwani na Wataalam wa Jiji la Mwanza waliotembelea eneo hilo jana Aprili 27, 2018 kwa lengo la kujifunza. 
Muonekano wa sehemu ya Dampo la kisasa la Chidaya Jijini Dodoma ambayo bado haijaanza kutumika.


................................................................
MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wameingia kwenye historia ya kuwa wageni wa kwanza kufanya ziara ya kubadilishana uzoefu katika Halmashauri ya Jiji jipya la Dodoma mara baada ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kupandishwa hadhi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli wakati wa Sherehe za miaka 54 ya Muungano Aprili 26, mwaka huu zilizofanyika katika uwanja ya Jamhuri Jijini humo.

Madiwani hao wa jiji la Mwanza wakiongozwa na Naibu Meya Mhe. Bhiku Kotecha ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyamagana, walitembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana Aprili 27, 2018 ikiwa ni siku moja tangu iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kupewa hadhi ya Jiji.

Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kubadilishana uzoefu hususan katika suala la Usafi wa Mazingira, ambapo walitembelea Dampo la kisasa la kuhifadhia takataka kwa njia ya kuzifukia (Sanitary Land Fill) lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu nje kidogo ya Jiji la Dodoma.

Wakiwa katika eneo la Dampo, walipata maelezo ya kina juu ya mradi huo kutoka kwa Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida, ambaye aliwaeleza kuwa, mradi huo umetekelezwa kwa awamu kuanzia mwaka 2011 kwa Fedha za Serikali Kuu ikiwa ni mkopo wa Benki ya Duniani kupitia mradi wa kuimarisha Majiji ya Kimkakati (TSCP) na kwamba hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 7.1, huku ukiwa tayari umeanza kufanya kazi.


Monday, April 23, 2018

KAZI YA UUZAJI WA VIWANJA 10,864 YAZIDI KUSHIKA KASI


Wateja wakieleweshwa eneo vilipo viwanja
Wateja wakiwa katika eneo maalum la kupumzikia wakati wakiendelea na taratibu za ununuzi wa viwanja

Mkuu wa Idara ya Ardhi Mipango Miji na Maliasili Joseph Mafuru (katikati) akishughulikia changamoto ya mteja.

..........................................
KAZI ya uuzaji wa Viwanja 10,684 imeendelea leo Jumatatu Aprili 23, 2018 katika eneo la Ofisi Kuu ya zamani ya Manispaa zilizopo jirani na Sabasaba.

Zoezi hilo lilianza siku ya Ijumaa Aprili 20, 2018, ambapo jumla ya wateja 399 walipatiwa Viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Katika awamu ya kwanza leo, wateja wapatao 400 wanaotarajiwa kuhudumiwa wamepatiwa kuponi za namba ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kuhudumiwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ardhi Mipango Miji na Maliasili Joseph Mafuru, zoezi la uuzaji wa Viwanja litaendelea mpaka Viwanja vyote vitakapomalizika na kwamba Wananchi wote wanakaribishwa.

Saturday, April 21, 2018

MANISPAA YA DODOMA YA PILI NCHINI KWA KUKUSANYA MAPATO

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza wakati ukiwasilisha taarifa ya Mikakati na Mipango mbalimbali ya Maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa na Manispaa hiyo mbele ya Kamati ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma jana.
Wajumbe wakifuatilia uwasilishaji wa Taarifa.


Wajumbe waalikwa wakifuatilia uwasilishaji wa Taarifa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akizungumza wakati ukiwasilisha taarifa ya Mikakati na Mipango mbalimbali ya Maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa na Manispaa hiyo mbele ya Kamati ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma jana.

Wajumbe wakifuatilia uwasilishaji wa Taarifa.
Baadhi ya Wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wakifuatilia Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Dodoma uliopokea taarifa ya Utekeleza wa Ilani ya CCM kuanzia 2015 hadi 2017.

..................................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma inatarajia kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 67.1 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani vya mapato katika mwaka ujao wa Fedha.
Kati ya Fedha hizo, zaidi ya Shilingi bilioni 54.5 sawa na asilimia 81 zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi wakati ukiwasilisha taarifa ya Mikakati na Mipango mbalimbali ya Maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa na Manispaa hiyo mbele ya Kamati ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma jana.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Taifa Mjini Dodoma, kilikuwa maalum kwa ajili ya wajumbe kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kuanzia mwaka 2015 hadi 2017, ambayo awali iliwasilishwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Kunambi aliwaambia wajumbe wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo Robert Mwinje kuwa, endapo Manispaa ya Dodoma itafanikiwa kufikia lengo hilo la makusanyo, itakuwa ni Halmashauri ya pili Nchini Tanzania kwa kukusanya Fedha nyingi kutoka katika vyanzo vya ndani ikitanguliwa na Manispaa ya Ilala.

Alisema hatua hiyo itaifanya Manispaa ya Dodoma kujiongezea uwezo mkubwa wa kujitegemea ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi zaidi.

Aliema kuwa, katika kuimarisha ukusanyaji, baadhi ya mikakati itatiliwa mkazo zaidi ikiwemo matumizi ya vifaa na mifumo ya Kielektroniki katika kukusanya, kuwa na takwimu sahihi, usimamizi wa karibu kwa kila chanzo, uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato, na kufanya tathimini za mara kwa mara.

Monday, April 16, 2018

ZAIDI YA VIWANJA ELFU KUMI VYAINGIA SOKONI DODOMA




...............................................................
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma inatarajia kuuza Viwanja 10,864 kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo Makazi, Biashara, Makazi na Biashara, Taasisi na Viwanda.
 Akiongea na Waandishi wa Habari Mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi amesema kuwa, Viwanja hivyo vipo katika maeneo ya  Mtumba na Iyumbu kando ya barabara kuu ya Dodoma - Dar es Salaam.
Amesema Viwanja hivyo vitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa Aprili 20, 2018 kuanzia saa 2:00 asubuhi katika eneo la Ofisi za Manispaa (Ofisi kuu ya zamani ya Manispaa) zilizopo jirani na Sabasaba.

KWA TAARIFA YA KINA SOMA HAPA CHINI;
Bei za Viwanja zitakuwa kama ifuatavyo kwa mita moja ya mraba:
ENEO LA MTUMBA
UKANDA WA BARABARA YA LAMI
  • Makazi                          8,000/=
  • Makazi na Biashara      8,500/=
  • Biashara                     10,000/=
  • Taasisi                          7,000/=
  • Viwanda vidogo          20,000/=
UKANDA WA KATI
  • Makazi                          6,000/=
  • Makazi na Biashara      7,500/=
  • Biashara                       8,000/=
  • Taasisi                          5,000/=
  • Viwanda vidogo          15,000/=
UKANDA WA BARABARA YA KIKOMBO
  • Makazi                         3,000/=
  • Makazi na Biashara     5,500/=
  • Biashara                      6,000/=
  • Taasisi                         5,000/=
  • Viwanda vidogo         10,000/=
ENEO LA IYUMBU
  • Makazi                         6,000/=
  • Makazi na Biashara     8,000/=
  • Biashara                    15,000/=
  • Taasisi                         7,000/=
  • Viwanda vidogo         20,000/=
Mauzo ya Viwanja yatafanyika kuanzia Ijumaa ya tarehe 20/04/2018. Utaratibu wa mauzo utakuwa kama ifuatavyo:
Kwa wananchi walioomba viwanja Manispaa watafika kwenye eneo la ofisi za zamani za Halmashauri na kuhakiki majina yao ambayo yatakuwa yamebandikwa kwenye mbao za matangazo. Ni lazima mwananchi afike na kitambulisho cha kumtambulisha. Kabla ya kuchagua kiwanja mwananchi anatakiwa kulipa Tshs. 20,000/= za fomu.
Mwananchi akishachagua kiwanja atapewa hati ya madai ya kiwanja hicho na kutakiwa kulipa fedha zote ndani ya siku Thelathini (30) tangu tarehe aliyopokea hati ya madai.
Kwa watumishi wa Umma wanaohamia Dodoma watapelekewa hati ya madai kupitia Makatibu Wakuu wa Wizara zao na watatakiwa kufanya malipo ndani ya siku Thelathini (30).

Wednesday, April 11, 2018

MANISPAA YAZIDI KUING’ARISHA MAKAO MAKUU


Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro akikagua moja ya vifaa vipya vilivyowekwa katika Mtaa wa Kuu kwa ajili kutunza uchafu ikiwa ni juhudi za Manispaa hiyo kuhakikisha Mji unakuwa safi wakati wote.

Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro (kulia) akisimamia uwekaji wa vifaa vipya vya kutunzia uchafu ikiwa ni juhudi za Manispaa hiyo kuhakikisha Mji unakuwa safi wakati wote. Kushoto ni Afisa Mazingira Ally Mfinanga.



Moja ya vifaa vya kutunzia taka kilichopo mkabala na Viwanja vya Nyerere katikati ya Mji.

..................................................

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma kupitia Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafi kwa kuongeza vifaa vya  kutunza uchafu katika mitaa kadhaa ya Mji ili kuhakikisha Wananchi hawatupi taka ovyo wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku.

Akizungumza wakati wa uwekji wa vifaa hivyo, Mkuu wa Idara hiyo Dickson Kimaro alisema Manispaa inatarajia  kuongeza  ‘vitunza uchafu’ 11 katika mitaa mbalimbali ili kuweka mazingira rafiki ya kutunza uchafu kwa Wakazi wa Mji wanaokuwa katika shughuli zao za kila siku.

“Hizi ni juhudi za makusudi ili kuhakikisha Mji wetu unakuwa safi muda wote…natoa wito kwa Wakazi wa Manispaa yetu watumie vifaa hivi kuhifadhia uchafu mdogo wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku” alisema Kimaro.

Alisema mbali na vifaa hivyo, tayari Manispaa ilishasambaza vifaa vikubwa vya kukusanyia taka za aina zote (Skip Bucket) 61 katika Kata mbalimbali zinazotumika kama vituo vya kukusanyia taka kabla ya kubebwa na Mitambo ya Manispaa na kupelekwa katika Dampo la Kisasa lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu nje kidogo ya Mji.