Thursday, July 28, 2016

MANISPAA YA DODOMA YAFANYA VIZURI KWENYE MAKUSANYO YA KODI

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imefanikiwa kukusanya asilimia 80.28 ya mapato kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya ndani katika mwaka wa fedha 2015/2016 uliomalizika Juni 30 mwaka huu.

Katika mwaka huo wa fedha Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ilipanga kukusanya shilingi 4,566,075,181 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani (own sources) ambapo mpaka mwisho wa mwaka huo makusanyo halisi ni 3,665,699,279 sawa na asilimia 80.28 ya makisio.

Akizungumza katika kikao cha mwaka cha Baraza la Halmashauri ya Manispaa hiyo, Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo kuwa, mafanikio hayo yametokana na uchapaji kazi wa watendaji na madiwani wa Manispaa hiyo.

Mstahiki Mwanyemba aliwapongeza wote waliohusika kwa namna yeyote katika kufikia hatua hiyo huku akitoa wito kwa Ofisi ya Mkurugenzi na Madiwani wa kuimarishwa kwa juhudi zaidi katika ukusanyaji katika mwaka wa fedha 2016/2017.

"Mwaka mpya wa fedha umeshaanza hivyo Mkurugenzi na watendaji wako anzeni kukusanya kodi mapema...na waheshimiwa madiwani tuongeze nguvu katika kusimamia vyanzo vya mapato katika maeneo yetu" alisema.

Aidha, katika mkutano huo ambao kwa mujibu wa kanuni unakuwa na ajenda mbili tu ambazo ni kujadili taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa Halmashauri kwa mwaka uliopita na kupitia na kupitisha ratiba ya vikao vya Halamshauri kwa mwaka unaofuata, wajumbe walipitisha ratiba ya vikao vya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 .   

No comments:

Post a Comment