Halmashauri
ya Manispaa ya Dodoma na jiji la Linz la nchini Austria zimesaini hati ya
makubaliano (Memorandum of Understanding) ya ushirikiano katika nyanja za Utunzaji
wa Mazingira, kuimarisha huduma za kijamii, uwekezaji wa kibiashara, kuimarisha
miundombinu na teknolojia, na kuimarisha huduma ya kupambana na majanga ya moto
na uokozi.
Maeneo
mengine ambayo mamlaka hizo mbili zimekubaliana kushirikiana ni pamoja kutoa
mafunzo mbalimbali wa watumishi wake na Madiwani wa pande zote mbili,
kubadilishana watumishi pamoja na kushirikiana katika jambo lolote litakaloonekana
kuwa na manufaa kwa wananchi wa pande zote.
Makubaliano
hayo yalifikiwa hivi karibuni wakati wa
ziara ya siku moja ya Naibu Meya
wa jiji la Linz Detlef Wimmer na ujumbe wake katika Manispaa ya Dodoma ambapo
alitembelea maeneo kadhaa ikiwemo Dampo la kisasa la takataka lililopo katika
kijiji cha Chidaya kata ya Ntyuka Manispaa ya Dodoma na shamba la zabibu katika
kata ya Mtumba ili kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Akisaini
makubaliano hayo kwa niaba ya Manispaa ya Dodoma, Meya wa Manispaa hiyo
Mstahiki Jaffar Mwanyemba alisema ushirikiano huo umekuja wakati muafaka na
kwamba utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa miji hiyo huku akitoa wito kwa marafiki
na wawekezaji wengine kujitokeza kwani
mji wa Dodoma kwa sasa umefunguka na kwamba ni wakati muafaka wa kuwekeza
Dodoma.
Kwa upande wake Naibu Meya wa jiji la Linz
Detlef Wimmer ambaye alisaini hati hiyo kwa niaba ya mamlaka ya jiji hilo
alielezea kuvutiwa kwake na mji wa Dodoma na kwamba amejifunza mengi katika
ziara yake huku akiahidi ushirikiano wa dhati katika maeneo waliyokubaliana.
Mkurugenzi
wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alisema ushirikiano kati ya Manispaa ya
Dodoma na Jiji la Linz ni mwanzo tu wa juhudi zinazofanywa na Manispaa katika
kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji
mbalimbali ili kuhakikisha Manispaa hiyo inakua kwa kasi huku huduma za kijamii
zikipewa kipaumbele kwa manufaa ya wakazi wake na hata wa mikoa ya jirani.
No comments:
Post a Comment