Tuesday, July 25, 2017
Monday, July 24, 2017
NAIBU WAZIRI TAMISEMI SELEMANI JAFFO AKABIDHI HUNDI YA MILIONI 70 KWA VIJANA NA WANAWAKE, AIPONGEZA MANISPAA YA DODOMA , ATAKA HALMASHAURI ZINGINE KUIGA MFANO
................................................................
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais
TAMISEMI Selemani Jaffo ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa
kutekeleza Sera na maelekezo ya Serikali kwa vitendo ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kuwa, asilimia 10 ya fedha
zinazotokana na mapato ya ndani zinatengwa na kutumika kwa ajili ya kuwawezesha
Wanawake na Vijana.
Naibu Waziri Jaffo ametoa
pongezi hizo wakati akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 70
zilizotolewa na Manispaa hiyo kwa ajili vikundi vya Vijana na Wanawake katika
hafla fupi ya makabidhianao iliyofanyika leo katika ukumbi wa Manispaa ya
Dodoma.
Alisema Halmashauri ya Manispaa
ya Dodoma imeonesha mfano kwa vitendo na kwamba Halmashauri zingine zijifunze
na kuiga, ambapo amedai hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri wa kazi uliopo
kati ya Madiwani, Mkurugenzi, Wakuu wa Idara na Watumishi wote.
Akizungumza wakati wa hafla
hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alisema fedha hizo zinatarajiwa kuvinufaisha
vikundi 66, vikiwemo 18 vya vijana na 48 vya wanawake.
Alisema, Halmashauri hiyo
imekuwa akitumia fedha za Mapato ya ndani kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali
ambapo pamoja na kutoa asilimia 10 kwa ajili ya vijana na wanawake, pia
asilimia 30 inaelekezwa katika katika miradi ya Maendeleo ambapo mpaka sasa
Kata 25 zimepatiwa sehemu ya fedha kwa ajili miradi ya maendeleo.
Aidha, Kunambi alisema kwa
sasa Halmashauri hiyo inaanza kusajili vikundi vya walemavu ambavyo kwa mujibu
wa Sera na Maelekezo ya Serikali vinatakiwa kupatiwa asilimia mbili ya Makusanyo
ya fedha zinatokana na vyanzo vya ndani.
Wednesday, July 19, 2017
PROFESA MWAMFUPE MEYA MPYA MANISPAA YA DODOMA
HALMASHAURI ya Manispaa ya
Dodoma imepata Meya mpya kufuatia uchaguzi uliofanyika leo Julai 19, 2017
katika Ukumbi wa Manispaa hiyo ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa
Davis George Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo.
Profesa Mwamfupe ameshinda
nafasi hiyo kwa kupata kura 50 kati ya kura zote 58 zilizopigwa na wajumbe 58,
dhidi ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Kikombo katika Manispaa hiyo Yona Kusaja aliyepata kura 8.
Awali, Mkurugenzi wa
Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi
aliwaeleza wajumbe utaratibu mzima wa kupiga kura kwa njia ya siri kwa kutumia
karatasi maalum za kupigia kura, na kwamba wajumbe halali watakaopiga kura kwa
mujibu wa sheria ni Madiwani wa Manispaa ya Dodoma tu.
Baada zoezi la kupiga na
kuhesabu kura kukamilika, Msimamizi wa Uchaguzi Godwin Kunambi kwa Mamlaka
aliyonayo kisheria, alimtangaza rasmi Profesa Mwafupe kuwa mshindi na kwamba
ndiye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma.
Uchaguzi huo ulihudhuriwa
na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Anthony Mavunde, Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma
Felister Bura, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde,
wataalam wa Manispaa ya Dodoma na Wakazi wa Manispaa wa Dodoma.
Profesa Mwamfupe anachukua
nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Meya
mheshimiwa Jaffar Mwanyemba ambaye aliondolewa madarakani na Baraza la
Madiwani Aprili 3 mwaka huu kwa kupigiwa kura za kutokuwa na imani naye
kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi.
Thursday, July 13, 2017
WATUMISHI WA ILIYOKUWA CDA WAPANGIWA VITUO VIPYA VYA KAZI SERIKALINI, WAZIRI WA TAMISEMI AWASOMEA TAASISI WALIZOPANGIWA
SERIKALI imewapangia vituo
vipya vya kazi watumishi 260 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma
(CDA) baada ya Mamlaka hiyo kuvunjwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dokta John Magufuli Mei 15 mwaka huu.
Rais Dokta Magufuli
alilazimika kuivunja Mamlaka hiyo ili kuondoa mkanganyiko wa kimajukumu kati ya
Mamlaka hiyo na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma hususan katika masuala ya umilikishaji
wa ardhi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais TAMISEMI George Simbachawene alikutana na watumishi hao wakati wa ziara
yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma jana na kuwasomea vituo
walivyopangiwa katika taasisi mbalimbali za serikali.
Kwa kujibu wa Waziri
Simbachawene, watumishi 150 wamehamishiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma,
idadi ambayo ni zaidi ya nusu ya watumishi wote 260.
Watumishi 66 wamepangwa
katika Mikoa na Wilaya mbalimbali Nchini, watumishi 16 wamehamishiwa katika
Ofisi ya Rais TAMISEMI, mtumishi mmoja amepangwa katika Ofisi ya Rais Utumishi,
na watumishi watatu wamehamishiwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Taasisi zingine ni Ofisi ya
Waziri Mkuu ambayo imepangiwa watumishi watatu, Wizara ya Ardhi watumishi
wawili, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepangiwa mtumishi mmoja, watumishi
wanne wamehamishiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Manispaa ya
Dodoma na watumishi 14 wamehamishiwa katika kampuni inayosimamia mradi wa
mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam (DART).
Kwa Mujibu wa Waziri Simbachawene,
Watumishi wote waliopangiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa watakuwa
wameshakabidhiwa barua zao za Uhamisho kufikia Julai 12 mwaka huu, ambapo wale
waliopangiwa Serikali Kuu watakabidhiwa barua zao muda wowote kuanza sasa kabla
ya kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi na kuendelea na majukumu
watakayopangiwa.
Wednesday, July 12, 2017
WAZIRI SIMBACHAWENE KUOMBA JIJI LA DODOMA KWA RAIS JOHN MAGUFULI
![]() |
| Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Lusako Kilembe (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene wakati wa ziara ya siku moja ya Waziri huyo katika Manispaa hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme. |
Alitoa ahadi hiyo jana
wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Dodoma katika Ukumbi wa Shule ya
Sekondari ya Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Manispaa hiyo,
iliyojumuisha pia ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo.
Aidha, amewataka watumishi
wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao (CDA) kumshukuru Rais kwa uamuzi wa
kuivunja Mamlaka hiyo kwa sababu hatua hiyo imeondoa mkanganyiko uliokuwepo katika
kuhudumia wananchi hususani katika sekta ya ardhi na mipango miji ambako
Manispaa ya Dodoma pia ilikuwa na jukumu hilo.
Pia aliwaeleza watumishi
hao wapatao 260 kuwa, sasa watapata fursa pana zaidi ya kuitumikia nchi yao
katika mikoa mbalimbali watakayopangiwa kuendelea kutumikia wananchi kwani wao
ni watumishi wa umma na wana haki na wajibu wa kufanya kazi sehemu yeyote
nchini.
Thursday, June 22, 2017
Thursday, June 8, 2017
'KITIMOTO' MARUFUKU MAKAO MAKUU DODOMA
Katika kipindi cha zuio:
- Hakuna mnyama yeyote jamii ya nguruwe (Ngiri, nguruwe pori au nguruwe wa kufugwa) ataruhusiwa kuingia, au kutoka nje ya eneo la Wilaya ya Dodoma pasipokuwa na ruhusa ya maaandishi kutoka kwa Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Dodoma.
- Pia hakuna bidhaa inayotokana na nguruwe, ikiwemo mbolea, kinyesi, mkojo na damu kitakacho ruhusiwa kuingia au kutoka nje ya Wilaya ya Dodoma pasipokuwa na ruhusa ya maandishi kutoka kwa Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Dodoma Mjini.
- Aidha, hakuna mnyama yeyote wa jamii iliyotajwa hapo juu atakayekusanywa kwa ajili ya biashara pasipokuwa na ruhusa ya maandishi kutoka kwa Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Dodoma.
- Uchinjaji wa nguruwe ndani ya Wilaya ya Dodoma, utafanyika chini ya usimamizi madhubuti wa mtaalam wa afya za mifugo mwenye dhamana.
Subscribe to:
Posts (Atom)



