HALMASHAURI
za Manispaa na Wilaya katika mikoa ya Kanda ya Kati unayoundwa na mikoa ya Dodoma na Singida kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wanaounga mkono shughuli za kilimo, mifugo na
uvuvi wameshauriwa kubuni njia rahisi inayoweza kuwafikishia kwa wakulima na wafugaji elimu
inayopatikana kwenye viwanja vya Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane.
Rai hiyo
imetolewa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe kufuatia maenesho ya Nanenane yaliyomalizika
hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo amesema bado Maonesho hayo hususan Kanda ya Kati hayajafanikiwa
kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwa kiasi kinachoridhisha na
kuwawezesha kubadili shughuli zao na kuzifanya kuwa na tija inayoridhisha.
Alisema
Maonesho ya Nane Nane yamekuwepo kwa miaka mingi katika Kanda mbalimbali nchini
na yamekuwa na mambo ya kuvutia sana hususani Teknolojia na mbinu bora za
uzalishaji katika kilimo na mifugo ambazo zinauwezo wa kuleta tija kubwa lakini
bado changamoto kubwa ni kwamba mambo yote bora na mazuri yanayopatikana kwenye
Maonesho hayajaweza kumfikia mkulima kwenye ngazi za msingi kwa maana ya ngazi
ya kaya na vijiji.
Alisema
kuwa, unaweza kutoka umbali usiozidi kilomita mbili tu kutoka kituo (Uwanja)
cha Maonesho kilipo utashangaa kukuta mkulima analima kilimo cha kienyeji
ambacho hakina manufaa.
“Teknolojia inayooneshwa kwenye Maonesho haya bado haijaweza kuwafikia
wakulima na wafugaji wetu kwenye vijiji vyao wanakoendesha shughuli zao za
kilimo na mifugo” alisema Profesa Mwamfupe na kuongeza kuwa, bado teknolojia na
ubunifu unaopatikana kwenye Maonesho haya unahitaji kuwafikia wakulima wa chini
kabisa.
Alitoa
wito kwa Mamlaka zinazohusika kuhakikisha Kiwanja cha Maonesho ya Nane Nane
Kanda ya Kati kilichopo katika Kata ya Nzuguni Manispaa ya Dodoma kinakuwa kituo cha Shamba Darasa la kilimo
mifugo na uvuvi cha kudumu ili wataalamu
wa kilimo na mifugo wawepo kituoni hapo kipindi chote cha mwaka wakisimamia shughuli
za kilimo na mifugo kituoni hapo na Halmashauri zilete Wakulima na Wafugaji wao
kujifunza na kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili katika shughuli zao
za uzalishaji.
Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe (wa kwanza kulia) akishuhudia mmoja ya banda la maonesho alipotembelea Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati katika Viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment