HALMASHAURI ya Manispaa ya
Dodoma imepata Meya mpya kufuatia uchaguzi uliofanyika leo Julai 19, 2017
katika Ukumbi wa Manispaa hiyo ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa
Davis George Mwamfupe ameshinda nafasi hiyo.
Profesa Mwamfupe ameshinda
nafasi hiyo kwa kupata kura 50 kati ya kura zote 58 zilizopigwa na wajumbe 58,
dhidi ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Kikombo katika Manispaa hiyo Yona Kusaja aliyepata kura 8.
Awali, Mkurugenzi wa
Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi
aliwaeleza wajumbe utaratibu mzima wa kupiga kura kwa njia ya siri kwa kutumia
karatasi maalum za kupigia kura, na kwamba wajumbe halali watakaopiga kura kwa
mujibu wa sheria ni Madiwani wa Manispaa ya Dodoma tu.
Baada zoezi la kupiga na
kuhesabu kura kukamilika, Msimamizi wa Uchaguzi Godwin Kunambi kwa Mamlaka
aliyonayo kisheria, alimtangaza rasmi Profesa Mwafupe kuwa mshindi na kwamba
ndiye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma.
Uchaguzi huo ulihudhuriwa
na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Anthony Mavunde, Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma
Felister Bura, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde,
wataalam wa Manispaa ya Dodoma na Wakazi wa Manispaa wa Dodoma.
Profesa Mwamfupe anachukua
nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Meya
mheshimiwa Jaffar Mwanyemba ambaye aliondolewa madarakani na Baraza la
Madiwani Aprili 3 mwaka huu kwa kupigiwa kura za kutokuwa na imani naye
kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi.
No comments:
Post a Comment