SERIKALI imewapangia vituo
vipya vya kazi watumishi 260 wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma
(CDA) baada ya Mamlaka hiyo kuvunjwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dokta John Magufuli Mei 15 mwaka huu.
Rais Dokta Magufuli
alilazimika kuivunja Mamlaka hiyo ili kuondoa mkanganyiko wa kimajukumu kati ya
Mamlaka hiyo na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma hususan katika masuala ya umilikishaji
wa ardhi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais TAMISEMI George Simbachawene alikutana na watumishi hao wakati wa ziara
yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma jana na kuwasomea vituo
walivyopangiwa katika taasisi mbalimbali za serikali.
Kwa kujibu wa Waziri
Simbachawene, watumishi 150 wamehamishiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma,
idadi ambayo ni zaidi ya nusu ya watumishi wote 260.
Watumishi 66 wamepangwa
katika Mikoa na Wilaya mbalimbali Nchini, watumishi 16 wamehamishiwa katika
Ofisi ya Rais TAMISEMI, mtumishi mmoja amepangwa katika Ofisi ya Rais Utumishi,
na watumishi watatu wamehamishiwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Taasisi zingine ni Ofisi ya
Waziri Mkuu ambayo imepangiwa watumishi watatu, Wizara ya Ardhi watumishi
wawili, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepangiwa mtumishi mmoja, watumishi
wanne wamehamishiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Manispaa ya
Dodoma na watumishi 14 wamehamishiwa katika kampuni inayosimamia mradi wa
mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam (DART).
Kwa Mujibu wa Waziri Simbachawene,
Watumishi wote waliopangiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa watakuwa
wameshakabidhiwa barua zao za Uhamisho kufikia Julai 12 mwaka huu, ambapo wale
waliopangiwa Serikali Kuu watakabidhiwa barua zao muda wowote kuanza sasa kabla
ya kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi na kuendelea na majukumu
watakayopangiwa.
No comments:
Post a Comment