.................................................................................................
MKURUGENZI wa Manispaa
ya Dodoma Godwin Kunambi ametoa wito kwa wakazi wa Manispaa hiyo kuacha mara
moja uvamizi wa maeneo ya wazi na yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za misitu
ambapo watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha amewataka
wanaojenga nyumba za makazi au za biashara katika maeneo yasiyo rasmi na ambayo
hayakupimwa kusitisha shughuli za ujenzi na kubomoa majengo hayo kwa hiyari yao
vinginevyo Halmashauri ya Manispaa itayabomoa.
Alisema hayo jana wakati
akizungumza wa wamiliki wa nyumba za kupanga na Maofisa Watendaji wa Kata wa
Manispaa ya Dodoma katika ukumbi wa Dodoma Sekondari, ambapo alisema kujenga
katika maeneo yasiyopimwa ni kinyume na sheria na Manispaa ya Dodoma imejipanga
kusimamia hilo kikamilifu.
Alisema Manispaa ya
Dodoma imejipanga kuanza upimaji wa viwanja kwa kasi ili kuwawezesha wananchi hususan wakazi wa Dodoma kujenga kwa
kuzingatia sheria za Mipango Miji na kwamba upimaji huo utaenda sambamba na
utoaji wa vibali vya ujenzi katika kipindi kisichozi siku saba kwa mmiliki wa
kiwanja.
Kwa upande wa wamiliki
wa nyumba za kupanga, aliwataka kuungana na kuwa na umoja na uongozi wao ili
kuepukana na madalali ambao baadhi yao sio waaminifu, huku akiwapa changamoto
ya kujenga nyumba zaidi za makazi na kuziimarisha zilizopo huku akiwajulisha
kuwa, hivi karibuni watumishi wa
Serikali zaidi ya 2,000 wanatarajiwa kuhamia Mjini Dodoma ikiwa ni awamu ya
pili ya Serikali kuhamia Dodoma hivyo mahitaji ya nyumba za kuishi yatakuwa
makubwa.
No comments:
Post a Comment