..........................................
WAFANYABIASHARA wadogo
maarufu kama Machinga katika Manispaa ya Dodoma wanatarajiwa kupewa eneo
lililotengwa rasmi na Halmashauri ya
Manispaa hiyo kwa ajili ya biashara zao lililopo katika Kata ya Makole mjini
humo.
Halmashauri ya Manispaa ya
Dodoma chini ya Mkurugenzi Godwin Kunambi imekamilisha uwekaji wa miundombinu
muhimu katika eneo hilo maarufu kama ‘Makole D-Center’ ikiwemo choo, ambapo
wakati wowote wafanyabiashara hao watahamishiwa kwa utaratibu utakaoratibiwa na
Manispaa kwa kushirikiana na uongozi wa wafanyabiashara hao.
Katika hatua za awali za
maandalizi ya eneo hilo, Halmashauri
pamoja na mambo mengine, iliondoa makazi ya Bibi Elizabeth Sonyo aliyekuwa
akiishi katika eneo hilo kinyume cha Sheria.
Hata hivyo, kutokana na
Bibi huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 75 kutokuwa na uwezo wa
kujenga, Manispaa ilibeba jukumu la kumjengea makazi mapya na bora zaidi katika
eneo jingine, ambapo amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa kitendo hicho kwani
hakuwa na uhalali wa kisheria wa kuishi katika hilo na kwamba angeweza
kuondolewa bila kupewa msaada wowote.
Kwa mujibu wa Kaimu
Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Ludigija Ndwata, kazi
iliyobaki ni kuweka mawe maalum (gravels) katika eneo hilo ili livutie zaidi na
liwe rafiki kwa wafanyabiashara na wateja, kabla ya matumizi kuanza.
Halmashauri ya Manispaa pia
inaandaa eneo la ‘Chaduru D-center’ kwa ajili ya kulirasimisha kwa matumizi ya wafanyabiashara
wadogo hususan akina mama wanaouza vyakula, mbogamboga, na matunda.
No comments:
Post a Comment