...............................................
WANANCHI 8570 wakazi wa
Kata ya Mkonze katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wananufaika na huduma
ya maji safi ya bomba kufuatia kukamilika kwa mradi wa Maji katika Kata hiyo
ulitekelezwa na Manispaa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi iliyowasilishwa kweye
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), mradi huo uliotekelezwa
chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya kwanza, ulianza
kujengwa Septemba, 2012 na kukamilika Machi, 2014 kwa gharama ya Shilingi 497,263,970
ukiwa na vituo 15 vya kutolea maji.
Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAAC) ilitembelea mradi huo jana na kuishauri Halmashauri
ya Manispaa ya Dodoma kuharakisha taratibu za kukabidhi mradi huo kwa Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) ambayo kwa mujibu wa sheria ndiyo
yenye dhamana ya kutoa huduma ya Maji mjini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa
Vedasto Ngombale aliwaogoza wajumbe wa
Kamati yake katika ziara ya kukagua ufanisi wa mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya
Kamati katika eneo la mradi, Mheshimiwa Ngombale ambaye pia ni Mbunge wa jimbo
la Kilwa Kaskazini, alisema ni muhimu mradi huo kuwa chini ya DUWASA kwani
umeshakamilika na uko eneo la mjini, badala ya kuwa chini ya Manispaa na
kusimamiwa na Jumuiya ya Watumiaji Maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi aliahidi kutekeleza ushauri
na maelekezo yote ya Kamati hiyo kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kusogeza
huduma muhimu karibu na wananchi yakamilike.
Tayari Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma iko katika hatua za mwisho za kukakabidhi mradi mwingine wa maji
kwa DUWASA uliotekelezwa katika Kata ya Ng’hong’ona ukiwa katika hatua ya
mwisho ya ukamilishwaji ambapo wananchi 8318 watanufaika na mradi huo wenye
vituo 20 vya kutolea maji.
Hongera sana Manispaa ya Dodoma kwa kuwajali wanachi. Mimi ni mkazi wa Mkonze; juhudi zenu zinaonekana wazi katika maendeleo ya wananchi. Kila la heri katika umoja na mshikamano katika maendeleo
ReplyDelete