.................................
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma
imeweka mkakati kabambe utakaowezesha kufikia lengo la ufaulu wa asilimia 100
kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi kuanzia mwaka 2018.
Hayo yamebainishwa katika taarifa
ya Manispaa hiyo iliyowasilishwa na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Manispaa ya
Dodoma Mwikongi Kigosi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge alipofanya
ziara ya kukagua maendeleo ya Elimu na Afya hivi karibu katika Manispaa hiyo.
Kwa kujibu wa taarifa hiyo,
miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wote wanamudu
stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu katika madarasa ya chini kabla
ya kujiunga na madarasa yanayofuata.
Kigosi alisema mkakati mwingine ni kusimamia mahudhurio ya
Walimu na Wanafunzi pamoja na kudhibiti matumizi ya simu kwa Walimu wawapo
darasani.
Aidha, alisema Idara ya
Elimu Msingi itateua shule 25 za serikali ambazo zitashindanishwa na shule za
binafsi ili kubadilishana uzoefu na kuinua ufaulu katika Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma.
Vilevile alisema Idara
imejipanga kuimarisha ufuatiliaji wa ufundishaji na kusimamia utendaji kazi wa
walimu, sambamba na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri.
“Pia tutakuwa na mitihani, mazoezi
na majaribio ya kufikirisha, pamoja na kambi za masomo… haya yote tutayafanya
na tunaamini yatatupa matokeo tunayotarajia” alisema Kigosi.
Kwa mwaka 2017 jumla ya
Wanafunzi 9,509 wakiwemo Wavulana 4,500 na Wasichana 5,009 walifanya
mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi katika Manispaa ya Dodoma ambapo Wanafunzi 6,488
wakiwemo Wavulana 3034 na Wasichana 3454
walifaulu, sawa na asilimia 68.
No comments:
Post a Comment